Thursday, November 1, 2018

WAZIRI MKUU: TUTAHAKIKISHA WANANCHI WOTE WANAPATA MAJI


*Aagiza vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli vibainishwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha wananchi katika vijiji vyote nchini wanapata huduma ya safi na salama wakiwemo na wa jimbo la Bumbuli.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mhandisi wa Maji wa Halmashauri  ya Bumbuli, wilayani Lushoto, Charles  Boy afanye utafiti na kubainisha vijiji vyenye shida ya maji Bumbuli.
Amesema baada ya kuvibaini vijiji hivyo, anatakiwa aweke mpango wa kuhakikisha navyo vinapata huduma ya maji safi ili kuwaondolea wananchi tatizo hilo la ukosefu wa  maji.
Alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 1, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mponde jimbo la Bumbuli, Lushoto.

Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, aliwapongeza wakazi wa wilaya ya Lushoto kwa kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yenye changamoto hiyo nchini.

Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo aliwataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.
Awali,Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi, ukarabati wa miradi ya maji, ambapo mkoa wa Tanga umetengewa sh. bilioni 13.
Aweso alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wakandarasi wanajenga miradi ya maji wazingatie viwango vya ubora kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika kugharamia miradi hiyo.
“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji alafu mnazitumia kujengea majumba na kununua magari, safari hii mtazitapika tunataka miradi itekelezwe kwa kuzingatia viwango.”
Waziri huyo aliahidi kufuatilia kwa kina ujenzi wa miradi yote ya maji nchini ili kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika miradi hiyo.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.