Saturday, August 23, 2025

SERIKALI KUGHARAMIA MAZISHI YA WALIOFARIKI KATIKA AJALI YA MGODI NYANDOLWA.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi, amemfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, salamu za pole kufuatia ajali ya kufukiwa kwa mafundi katika Mgodi wa Dhahabu wa Nyandolwa, iliyotokea tarehe 11 Agosti 2025 katika Mkoa wa Shinyanga.

Waziri Lukuvi ameeleza kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo, na kwa niaba ya Rais Samia, ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika tukio hilo la kusikitisha. Aidha, ameeleza kuwa Serikali itagharamia kikamilifu gharama za mazishi kwa waathirika wa ajali hiyo pamoja na matibabu kwa waliofikwa na tukio hilo.

Akizungumza na wanandugu wa marehemu na wale waliokwama mgodini, Mhe. Lukuvi amewatia moyo na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Ametoa wito kwa timu za uokoaji kuongeza juhudi na kasi ya uokoaji ili kuwaokoa mafundi waliokwama kwa haraka na usalama zaidi.

“Tunaamini kuwa kazi kubwa imefanyika lakini bado tunahitaji jitihada zaidi. Serikali inatambua uzito wa tukio hili na itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa kuhakikisha kila jitihada zinafanyika kwa ufanisi,” amesema Lukuvi.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mgodi huo, Fikiri, ameiambia Serikali kuwa ndani ya kipindi cha siku tatu hadi nne zijazo, zoezi la kuwaokoa wahanga waliokwama litakuwa limekamilika. Ameeleza kuwa vifaa vya kutosha vimeletwa eneo la tukio na wataalamu wanaendelea na kazi kwa umakini mkubwa kuhakikisha mafanikio ya haraka.

Kabla ya kuwasili katika eneo la mgodi, Mhe. Lukuvi alifanya ziara katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambapo alipokea taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya sekta ya madini katika mkoa huo pamoja na hali ya sasa ya shughuli za uokoaji zinazoendelea katika mgodi wa Nyandolwa.

Akizungumza kwa niaba ya ndugu wa wanasubiri waliofukiwa na kifusi Bw.Furaha Enock aliishukuru Serikali kwa namna ilivyoratibu zoezi na inavyowahudumia katika kipindi chote toka tukio kutokea na kueleza kuwa imefanya jambo la kipekee, la heshima na la uungwana kuwashika mkono na kuhudumia kwa hali na mali na kuwasihi wanandugu kuendelea kuwa na utulivu.

"Kipekee ninaipongeza Serikali Yetu imetufanyia wema na imetupa faraja kwa namna wanavyoratibu tukio zima, tunakosa neno zaidi ya Asante sana kwa Rais Dkt. Samia pamoja na uongozo wake wote," alisema Enock

AWALI

Ziara ya Waziri Lukuvi ni sehemu ya juhudi za Serikali za Uratibu na kutoa maelekezo kwa karibu katika kipindi hiki cha majonzi, huku ikilenga kuimarisha utendaji wa shughuli za uokoaji na kuhakikisha haki na heshima kwa waathirika wote wa ajali hiyo.

Read More

Thursday, August 21, 2025

SERIKALI YAENDELEA NA JITIHADA ZA UOKOAJI MGODI WA NYANDOLWA


Imeelezwa kuwa, jitihada za kuendelea kuokoa maisha baada ya ajali ya mgodi kutokea eneo la Nyandolwa Mkoani Shinyanga zinaendelea usiku na mchana ambapo hadi kufikia Leo Agosti 21,2025 mafundi 10 kati ya 25 waliokuwa wamekwama chini ya ardhi wameokolewa, huku wanne wakiwa hai, mmoja kati yao akifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini, na saba wakikutwa wamefariki dunia.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mkoani humo ambapo amethibitisha taarifa hizo na kusema kuwa tukio hilo lilitokea takribani siku 10 zilizopita, likisababisha shughuli za uokoaji kuendelea kwa muda mrefu katika mazingira magumu.

Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya ardhi kutitia ghafla na kusababisha kifusi kuporomoka katika mashimo (maduara) matatu tofauti yaliyokuwa yakikarabatiwa na mafundi ndani ya mgodi huo, unaomilikiwa na kikundi cha Wachapakazi chini ya leseni ya uchimbaji mdogo.

"Tunaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama. Hili ni tukio la huzuni kubwa kwa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla," amesema Mhe. Mhita.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko, ametoa wito kwa timu ya uokoaji kuongeza kasi na juhudi katika shughuli za uokoaji, akisisitiza kuwa kila sekunde ina maana katika kuokoa maisha ya waliobaki chini ya kifusi.

“Natoa pongezi kwa kikosi kizima cha uokoaji kwa moyo wao wa kujitolea, lakini ni muhimu sasa kuongeza kasi bila kuhatarisha usalama wa waokoaji wenyewe,” amesema Dkt. Kilabuko.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amefika eneo la tukio na kutoa salamu za pole kwa familia za marehemu na wote walioathirika na ajali hiyo. Ametoa rai kwa waokoaji kuendelea kuwa na umakini mkubwa na kutanguliza usalama katika operesheni ya uokoaji.

“Hii ni ajali ya kusikitisha mno. Tume ya Madini inatoa pole kwa familia za wahanga, na tutaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha taratibu zote za usalama katika migodi zinasimamiwa ipasavyo ili kuepusha ajali kama hizi siku za usoni,” amesema Dkt. Lekashingo.

Aliongezea kuwa, Timu za uokoaji zinajumuisha maafisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi, Tume ya Madini, Wizara ya Madini, wachimbaji wenzao, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Shinyanga, ambao wote wanaendelea kushirikiana kuhakikisha mafundi waliobaki wanatolewa salama.

Hadi sasa, juhudi za uokoaji bado zinaendelea katika eneo hilo la mgodi, huku matumaini yakiwa bado hayajapotea kwa familia na ndugu wa mafundi waliobaki chini ya kifusi. Serikali imeahidi kutoa usaidizi wa karibu kwa waathirika na kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika kubaini chanzo cha ajali hiyo.



Read More

SERIKALI YA ZAMBIA YAPATA MAFUNZO KUTOKA TANZANIA: YAPONGEZA UJENZI WA MJI WA SERIKALI DODOMA


Maofisa waandamizi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Zambia wametembelea Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kutekeleza mradi mkubwa wa kitaifa wa kuhamishia shughuli za serikali katika mji huo.

Wakiwa katika ziara hiyo, maofisa hao walipokelewa na Mratibu wa Ujenzi wa Mji wa Serikali, Bw. Noel Mlindwa, ambaye alieleza kuwa Tanzania imeweka historia kwa kuanzisha na kutekeleza kwa mafanikio makubwa ujenzi wa mji wa serikali, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Bw. Mlindwa alifafanua kuwa mji huo umejengwa kwa kuzingatia mipango bora ya kisasa, usimamizi makini wa rasilimali na matumizi ya teknolojia, hali iliyowavutia wageni hao kutoka Zambia.

Kwa upande wao, maofisa wa Zambia waliipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga na walisisitiza kuwa Mji wa Serikali Dodoma si tu ni kielelezo cha maendeleo, bali pia ni kivutio cha kiutalii na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine barani Afrika.



Read More

Saturday, August 16, 2025

UZINDUZI WA MFUMO WA ANUANI ZA MAKAZI ZANZIBAR WAFANA


Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga, ameshiriki katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa anuani za makazi, unaolenga kutoa huduma ya barua ya utambulisho wa mkazi kwa njia ya kidijitali.

Uzinduzi huo umefanyika leo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar, ukiongozwa na Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Ummy amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada zao za kuimarisha huduma za kijamii kupitia mifumo ya kidijitali.

"Niwapongeze kwa kuendelea kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi kupitia teknolojia. Mfumo huu utarahisisha utambuzi wa makazi na uboreshaji wa utoaji wa huduma mbalimbali serikalini," alisema Mhe. Ummy.

Aidha, amezipongeza wizara zote za kisekta kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wao uliowezesha utekelezaji wa mfumo huo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.



Read More

Thursday, August 14, 2025

MAKATIBU WAKUU WATETA MIKAKATI YA KUENDELEZA SAFARI CHANNEL YA TBC


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. James Kilabuko, ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kilichofanyika leo jijini Dodoma kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha uendeshaji wa Tanzania Safari Channel chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kilabuko amesema chaneli hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii vilivyopo nchini, hivyo ni muhimu kwa taasisi zote za serikali kushirikiana katika kuiendeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha, akiwasilisha taarifa kuhusu chaneli hiyo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusaini sheria mpya ya TBC, ambayo imefungua milango ya maboresho ya kiutendaji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma.

Chaneli ya Tanzania Safari Channel imekuwa chombo mahsusi cha kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vya kipekee duniani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimkakati kukuza sekta ya utalii.

Read More

Tuesday, August 12, 2025

ZANZIBAR YACHOTA UZOEFU DODOMA: YAJIANDAA KUJENGA MJI WA SERIKALI KISAKASAKA

 



Kamati ya wataalamu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ikiingozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum imetembelea miradi mikubwa jijini Dodoma ikiwemo Mji wa Serikali Mtumba na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, kujifunza utekelezaji wa Ujenzi wa Mji wa Serikali.

Ziara hiyo inalenga kuandaa mazingira ya ujenzi wa ofisi za Serikali na Baraza la Wawakilishi eneo la Kisakasaka, Zanzibar.

Viongozi hao wamempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuimarisha maendeleo ya Makao Makuu ya Nchi kupitia miradi ya kimkakati.



Read More

Monday, August 4, 2025

HELEN KELLER INTERNATIONAL KUSHIRIKIANA NA OFISI YA WAZIRI MKUU KUIMARISHA URATIBU WA LISHE NCHINI


Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Stella Mwaisaga, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kimataifa la Helen Keller International, Bw. William “Bill” Toppeta.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na shirika hilo katika utekelezaji wa masuala ya lishe, ambapo Bw. Toppeta aliipongeza Serikali kwa juhudi kubwa katika kusimamia na kuratibu lishe, huku akisisitiza dhamira ya Helen Keller International kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha jamii inapata huduma bora za lishe.

“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa usimamizi wake imara katika masuala ya lishe. Tutaendelea kuwa wadau wa karibu katika kusaidia juhudi hizi muhimu kwa afya ya wananchi,” alisema Bw. Toppeta.

Ujumbe huo wa Helen Keller International upo nchini kwa ziara ya kukagua na kutathmini utekelezaji wa miradi ya shirika hilo, hususan katika sekta ya lishe, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu mkuu wa kitaifa wa masuala hayo.

Read More