Home
All posts
Wednesday, August 16, 2017
WAZIRI MKUU AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Balozi Benedict Mashiba, ambapo amemtaka kuimarisha mahusiano baina ya nchi zote mbili.
Amekutana na Balozi Mashiba leo (Jumatano, Agosti 16, 2017) katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam, ambapo amemtaka balozi huyo kuhakikisha anaboresha shughuli za Kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi.
Pia Waziri Mkuu amemtaka Balozi huyo kuhakikisha anatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ukiwemo mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususan katika sekta ya viwanda.
Waziri Mkuu amesema licha ya kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii pia amemtaka kuboresha biashara baina ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli mbili za mizigo za Mv. Ruvuma na Mv. Njombe alizozizindua hivi karibuni.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amemtaka Balozi Mashiba kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio nchini Malawi na kuwasisiza kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi husika. Pia kuwaunganisha pamoja na kuwashauri waje kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Balozi Mashiba amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi.
Sunday, August 13, 2017
WAZIRI MKUU NA MKEWE WAMJULIA HALI MBUNGE WA VITI MAALUM (CCM)KIGOMA
WAZIRI MKUU: ACHENI KUAJIRI WATOTO KWENYE MASHAMBA YA TUMBAKU
*Ahimiza elimu kwa mtoto wa kike, akemea mimba za utotoni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.
“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari.
“Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara yake ya siku nne moani Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30.
Pia aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika kushirikiana na waoaji.
WAZIRI MKUU AWABANA MAAFISA USHIRIKA, KILIMO
*Ataka wasimamie zao la tumbaku kwa umakini ili kumkoboa mkulima
*Ataka wajipange kutumia vyombo vya habari kuelimisha wakulima
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa kilimo na maafisa ushirika wa mkoa wa Tabora wasimamie kwa umakini ukuzaji wa zao la tumbaku kuanzia msimu ujao.
"Mkakati wetu wa kuinua zao hili unaanza msimu ujao, ninaondoka Tabora lakini nataka kila mmoja wenu atumie nafasi yake kuelezea suala hili kwa kina kwa wakulima wa zao la tumbaku ili tubadilishe mfumo na tuweze kuwakomboa," alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe na baadhi ya watendaji kutoka wizara hiyo.
Aliwataka watendaji hao watumie vyombo vya habari vya ndani ya mkoa na vya kitaifa kuelezea mkakati mpya ambao serikali inao wa kuinua zao la tumbaku. “Tumieni vyombo vya habari kila mmoja apange ratiba kuelezea atafanya nini, toeni elimu kwa sababu vyombo hivi vinasikika hadi kwenye mikoa ya jirani,” alisisitiza.
“Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue una wakulima wangapi, je wakulima wako kila mmoja analima ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana mahitaji ya pembejeo kiasi gani?” alisema.
“Afisa ushirika wa wilaya nawe hakikisha unasajili idadi ya vyama vya msingi (AMCOS) vilivyoko kwenye eneo lako, lazima ujue AMCOS ziko ngapi na zina wanachama wangapi. Afisa kilimo na afisa ushirika muanze kazi hiyo mara moja,” alisisitiza.
“Ulizeni mahitaji yao ni yapi, kwa kila mwanachama na kila AMCOS, kisha muziwasilishe kwa Mkuu wa Mkoa ili naye azifikishw kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Pale wizarani, tunataka Mkurugenzi wa Pembejeo ajue mahitaji ya kila mkoa ili pembejeo ziweze kuwasilishwa kwa wakulima miezi miwili kabla msimu wa kilimo haujaanza, kama ambavyo tumeagiza,” alisema.
Akifafanua kuhusu uagizaji wa mbolea, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanzisha mfumo wa pamoja wa mbolea (bulk procurement) na akawataka wataalamu wa wizara ya kilimo wamalize mgogoro wa siku nyingi uliokuwepo baina yao na kiwanda cha mbolea cha Minjingu.
“Kumekuwa na maneno maneno kuhusu mbole ya NPK, lakini wakati sisi tunaidharau, wenzetu wa nchi jirani wanaongoza kwa kuagiza mbolea nyingi kutoka Minjingu. Acheni kuagiza mbolea hiyo kutoka nje ya nchi, tukachukue pale Minjingu,” alisisitiza.
Alisema mwenye kiwanda ameahidi kwamba akipewa oda ya mbolea, yeye atazisafirisha hadi kiwandani. “Hakuna haja ya kuwaumiza wakulima na mbolea za bei mbaya wakati tunayo hapa nyumbani na tena ya bei nafuu. Wenye makampuni ya kununua tumbaku wanauza mfuko mmoja kwa dola 70 sawa na sh.150,000 hii ya Minjingu yenye ubora uleule inauzwa sh. 60,000 kwa mfuko mmoja, tena zikiwa zimefikishwa wilayani.”
“Ninawasihi viongozi wa ushirika na wa wilaya tusaidiane kumuondoa mkulima kwenye utegemezi wa mikopo ya benki na badala yake tuwaelimishe wajiwekee akiba ya kumudu pembejeo za msimu unaofuata,” alisisitiza.
Alisema kama kutakuwa na ulazima wa kuingia kwenye mikopo, viongozi hao hawana budi kuhakikisha kuwa wanaisimamia kwa kikamilifu. “Kama mtaingia kwenye mikopo, lazima mjipange kuisimamia mikopo hiyo ili isije ikawarudisha nyuma wakulima wetu kwenye mfumo ambao ulikuwa unawaumiza,” aliongeza.
Akifafanua kuhusu ununuzi wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema AMCOS ndizo zenye tumbaku na kwa maana hiyo ndiyo zitahusika na uuzaji. Katika kila wilaya, wekeni mfumo wa usimamizi kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama. Malori yakikamatwa na marobota yaliyouzwa nje ya mfumo, ni lazima hatua kali zichukuliwe,” alisisitiza.
“Ninasema hakuna mazungumzo tena nje ya AMCOS, ni kwa kampuni ya ununuzi au kwa mtu binafsi. Na kuanzia sasa, Associations za tumbaku zimefutwa. Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya hakikisheni hakuna associations kwenye zao la tumbaku, tunataka kila mmoja akanunue kwenye AMCOS na kila mkulima asajiliwe kwenye AMCOS,” alisisitiza.
Alisema Serikali ilivunja Chama Kikuu cha Ushirika Kanda ya Magharibi (WETCU) kutokana na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na viongozi wa chama hicho na kwamba hivi sasa kutakuwa na WETCU mbili ambapo ya kwanza (WETCU I) itahusika na wilaya za Kaliua na Urambo na ile ya pili (WETCU II) itahudumia wilaya za Sikonge, Uyui, Nzega na sehemu ndogo ya Tabora Manispaa.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuwe na vyama vikuu viwili vyenye AMCOS chache lakini zenye uwezo wa kuwafikia wakulima, kusikiliza mahitaji yao na kutatua matatizo yao. WETCU ya zamani ilikuwa na AMCOS 214 na haikuweza kuwafikia wakulima wote.
WAZIRI MKUU ATAKA BODI IJAYO YA TUMBAKU IJIPANGE
*Aitaka isimamie zao hilo na kutafuta masoko, iache kutoa vibali vya ununuzi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tumbaku ni siasa na tumbaku ni uchumi na ameitaka Bodi ya Tumbaku itakayoundwa ijipange kumlinda mkulima.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe na baadhi ya wakurugenzi kutoka wizara hiyo.
Alisema wajumbe wa bodi hiyo walishatajwa lakini kwa sasa hivi wanasubiri uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo. Hata hivyo, Waziri alimwelekeza Katibu Mkuu wa Kilimo awaite wajumbe wa bodi hiyo wakutane na kumchagua Makamu Mwenyekiti wa muda ili waanze kazi ya kukutana na WETCU zao.
“Kwa sababu bodi ni ya nchi nzima, ni vema wakakutana na WETCU zao na AMCOS zao ili waanze kukusanya taarifa ya tumbaku kutoka Chunya, Namtumbo, Serengeti na mahali mengine ili wapeleke message hii ya msimu ujao,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema ili kuongeza ufanisi kwenye zao hilo, itabidi baadhi ya majukumu ya bodi yapunguzwe ikiwemo kazi ya utoaji vibali vya kusafirisha na kununua tumbaku. “Hivi kama kibali cha kuuza tumbaku ya Namtumbo kinatolewa na Bodi ambayo makao makuu yake yako Tabora, sasa utawezaje kufuatilia kutoka Tabora? Ka nini kazi hiyo isifanywe na chama kikuu cha ushirika kilichopo huo?” alihoji Waziri Mkuu.
Alionya kwamba endapo bodi itaachiwa iingie kila mahali, haitaweza kulaumiwa pindi jambo likiharibika. “Ninyi kazi yenu kubwa iwe ni usimamizi kuanzia kwenye WETCU na AMCOS zake. Simamieni masoko, hakikisheni wanaokuja kununua wako tayari kufuata mfumo uliowekwa na Serikali,” alisema.
Waziri Mkuu alisema bodi ijayo inalo jukumu pia la kushirikiana na vyuo vya utafiti ili kuhakikisha kuwa tafiti zinafanyika na kupata mbegu bora zenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa.
Akizungumzia kuhusu upangaji wa madaraja kwenye zao la tumbaku, Waziri Mkuu alisema kuna hatua imefanyika kwani hivi sasa madaraha yamepunguzwa kutoka zaidi ya 100 yaliyokuwepo na kufikia 39. Hata hivyo, alisema wingi wa madaraja bado ni changamoto kwenye upangaji wa bei.
“Bodi na wizara lazima mzungumze na makampuni ya ununuzi na mkubaliane mfumo gani utatumika kuhusu madaraja ya tumbaku. Kazi yetu kubwa na kumlinda mkulima.”
“Wenzenu wa korosho walikuwa na madaraja mengi lakini sasa yamebakia mawili, grade 1 na grade 2 na bei ya kila daraja inajulikana kwa hiyo rahisi kumuibia mkulima,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Mzee Hassan Wakasuvi akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu kwa ziara yake alisema wameyapokea maelekezo hayo na hawatasita kuwasukuma watendaji wanaochelewa kutimiza wajibu wao.
“Miaka miwili iliyopita, tumbaku ilikuwa ni zao linaloongoza kwa kuingiza fedha za kigeni hapa nchini. Lakini hivi tumeshuka, na tumeiacha korosho ndiyo inaongoza, tumedhamiria kurudi kwenye nafasi yetu, na hatutasita kuwaweka pembeni watendaji wa Serikali wataotuchelewesha kufikia azma yetu hiyo,” alisema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku nne na ameahidi kurudi kumalizia wilaya za Nzega, Igunga na Tabora Manispaa ambazo hakuzitembelea.
WAZIRI MKUU: ACHENI KUAJIRI WATOTO KWENYE MASHAMBA YA TUMBAKU
*Ahimiza elimu kwa mtoto wa kike, akemea mimba za utotoni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.
“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari.
“Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara yake ya siku nne moani Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30.
Pia aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika kushirikiana na waoaji.
WAZIRI MKUU AHITIMISHA ZIARA YAKE LEO KATIKA MKOA WA TABORA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana katika Uwanja wa Ndege wa Tabora leo August.13.2017 . na Mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora .Agrey Mwandi .Baada ya kumaliza ziara ya siku Nne katika Mkoa wa Tabora ,katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Queen Mwashinga.
|
| Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwapungia Mkono wa kwaheri Viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Tabora ambao walifika kumuaga katika Uwanja wa Ndege wa Tabora baada yakumaliza ziara ya siku Nne ya kikazi katika Mkoa wa Tabora leo August 13,2017. |
Saturday, August 12, 2017
WAZIRI MKUU AKIWA WILAYA YA UYUI MKOA WA TABORA KWA ZIARA YA KIKAZI
| Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya CCM Taifa na Mkuu wa Wilaya Mstaafu Bwana Jackson Masome .walipo kutana katika mkutano wa hadhara leo August 12.2017 katika Wiaya ya Uyui Tabora. |
| Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkewe Mama Majaliwa wakiwasalimia wananchi katika Uwanja wa Nsololo jimbo la Igalula Wilaya ya Uyui mara baada yakuwasili leo August 12.2017 na Waziri Mkuu kufanya mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Uyui Mkoa wa Tabora. |
SERIKALI ITALIPA MADENI YOTE YA WATUMISHI – WAZIRI MKUU
*Asisitiza uadilifu, uwajibikaji na uaminifu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali.
“Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli alisitisha malipo sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo imeshakamilika, yale yaliyobainika kuwa ni halali yatalipwa. Tunataka watumishi mfanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa bidii,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.
Akiwa katika wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa na baadhi ya wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao walihamishwa kutoka manispaa kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza watumishi wa wilaya hizo kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
“Hivi sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu,” alisema.
Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.
Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
“Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo,” alisema.
“Mimi nimekuwa kwenye utumishi wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi kuona kama kuna watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume taarifa zao mapema (kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye mfumo huu, kisha wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.
“Napenda kusisitiza kuwa malengo ya Serikali ni kuimarisha utendaji wa watumishi lakini pia Serikali hii haitamvumilia mtu mdanganyifu, mzembe, asiye mwadilifu na mla rushwa. Tukikukamata hatuundi tume kwa sababu tume nazo zinamaliza fedha tu. Tukiwa na ushahidi wa kutosha, tunamalizana hapohapo,” aliongeza.
WAZIRI MKUU AKEMEA MAAFISA MISITU
*Ataka waache kutoa hovyo vibali vya uvunaji misitu
*Ahimiza utunzaji misitu, mazingira
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutoa vibali vya uvunaji mbao inayofanywa na maafisa misitu wa TFS ambao wako chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumamosi, Agosti 12, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliofanyika kata ya Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kumhoji Afisa Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Kazimoto na Afisa Misitu wa Wilaya, Bw. Jared Nzilorera na kubaini kuwa hawafanyi kazi kwa kushirikiana.
"Hapa kuna uvunaji mkubwa wa misitu. Je kuna mtu anafuatilia kama wanavuna kwa usahihi?" alihoji Waziri Mkuu.
Akijibu swali la Waziri Mkuu, Bw. Kazimoto alisema Uyui hakuna uvunaji lakini wanaovuna wanatoka Sikonge na kuja kuuza mbao Uyui.
Alipoulizwa Afisa Misitu wa Wilaya, ni kwa kiasi gani wanapeana taarifa na mwenzake wa TFS ambao wanaletwa na wizara, alitoa majibu ya kujichanganya hali iliyomfanya Waziri Mkuu aamue kukemea tabia yao ya kutoa vibali bila kuwahusisha wenzao wa Halmashauri.
"TFS mmejiingiza kwenye kuvuna misitu, na mnawaover-power DFOs (wale wa Halmashauri). Hawa walioko kwenye Halmashauri ndiyo wanaolinda misitu yote ambayo iko ndani ya wilaya husika."
"Tatizo hili liko nchi nzima, ni la ushindani kati ya maafisa misitu wa TFS na wale wa Halmashauri. Misitu yetu inakwisha sababu mnaimaliza nyie kwa kutoa vibali bila kuwashirikisha wenzenu.
Alimwagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bi. Queen Mlozi asimamie suala hilo. "DC wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, simamia jambo hili na usisitize utunzaji wa mazingira na upandaji miti," alisema.
Alisema ukataji miti ovyo umechangia kukauka kwa vyanzo vingi vya maji. "Mhandisi wa Maji anahangaika kuchimba visima lakini hakuti maji sababu miti imekatwa ovyo na ardhi tepetevu imekauka. Watumishi wote nendeni vijijini mkahamasishe utunzaji wa mazingira," alisema.
Kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, kila mkoa una Afisa Misitu wa Mkoa, kila wilaya imeajiri Afisa Misitu wa Halmashauri, lakini Wizara pia imeajiri Maafisa wa Misitu kutoka TFS katika ngazi za mkoa na wilaya.
Friday, August 11, 2017
WAZIRI MKUU: SERIKALI KUFUFUA MAZAO MAKUU MATANO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kufufua mazao matano ambayo yanaingiza kwa wingi fedha za kigeni nchini.
Amesema mbali ya korosho, Serikali imeamua kuboresha mazao ya tumbaku, chai, kahawa na pamba.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana na leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maeneo mbalimbali akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora.
Alisema kuanzania sasa serikali imepiga marufuku matumizi ya dola za Marekani kwenye ununuzi wa zao la tumbaku kwa sababu mazao mengine makuu hapa nchini yananunuliwa kwa fedha za Kitanzania.
“Ni kwa nini tumbaku inunuliwe kwa dola za Marekani ilhali mazao mengine yananunuliwa kwa fedha za Tanzania? Korosho, pamba, chai na kahawa wakulima wetu kote huko wanalipwa kwa fedha za Tanzania, kwa nini tumbaku iwe tofauti?” alihoji.
Alisema wenye makampuni wanaweza kukaa kwenye vikao vyao na kupanga bei zao kwa dola za Marekani lakini pindi wanapoingia nchini, watalazimika kufanya malipo kwa kutumia fedha ya Tanzania kwani mfumo malipo kupitia dola za Marekani umekuwa ukiwaibia wakulima kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amewataka watendaji na watumishi wa Halmashauri na wilaya za mkoa wa Tabora wasimamie zao la tumbaku ili kuinua kilimo cha zao hilo na kuwanufaisha wakulima.
"Maafisa kilimo na maafisa ushirika mnapaswa kulisimamia zao hili na siyo kuwaachia maafisa wa makampuni yanayonunua tumbaku."
“Kwa muda mrefu mlizembea na kuwaachia maafisa wa makampuni ya ununuzi ndiyo washughulike na wakulima. Nataka mbadilike, kuweni karibu na wakulima na muwasaidie kulima kisasa na kwa kutumia pembejeo," alisema.
"Wasaidieni wakulima watoke kwenye mfumo wa kukopa pembejeo, wahimizeni wajiwekee akiba ili msimu ukianza wawe na fedha ya kununua pembejeo. Wakulima wanalaliwa sababu ya mikopo ya pembejeo. Makato yanakuwa mengi kiasi kwamba mkulima ahambulii chochote," alisema.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kaliua ambako atazungumza na wananchi.
WAZIRI MKUU AKEMEA MATUKIO YA UHALIFU ULYANKULU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu waache kujihusisha na matukio ya uhalifu.
Ametoa onyo hilo leo mchana (Ijumaa, Agosti 11, 2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya VETA, wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Amesema matukio ya ujambazi, mauaji na umiliki wa silaha yanayofanyika kwenye tarafa hiyo ni mengi ikilinganishwa hali ilivyo kwenye maeneo mengine ya mkoa huo.
"Taarifa nilizonazo zinaonyesha katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na matukio ya mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki wa silaha nao unatisha. Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four mbili."
"Tulikamata pia risasi 714 za SMG zikiwa kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka mafuta ya mawese. Pia risasi mbili za Mark Four zilikamatwa," amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewataka wakazi hao ambao baadhi yao wamepewa uraia na wengine bado ni wakimbizi waonyane wanapokutana kwenye vikao vyao kwa sababu matendo yao yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi. "Ni vema mkikutana kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana," amesema Waziri Mkuu.
"Ninawasihi matukio haya myadhibiti la sivyo mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo wenu. Bunduki na risasi zinakuja kufanya nini wakati nyie mko maeneo salama? Mauaji ya nini? Kama kuna tatizo limekupata, muone mwenyekiti wa kijiji, atakusaidia," alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi yao ambao wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila kufuata utaratibu. "Hatuzuii mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni lazima mfuate taratibu. Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini pia tudumishe urafiki wa nchi zetu mbili za Burundi na Tanzania," aliongeza.
Mapema, Mbunge wa jimbo la Ulyankulu, Bw. John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba wasaidiwe ili kata tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
WANANCHI WALIOPEWA URAIA MUHESHIMU SHERIA ZA NCHI ,MAJALIWA
| Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa kitongoji cha Mwamnange kilichopo Wilaya ya Kaliua leo Agosti 11 2017 .Wananchi hao walisimamisha msafara wake ili kumuomba serekali iwasaidie kupata Umeme. Waziri Mkuu yupo Mkoani Tabora kukagua shughuli za maendeleo. |
| Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihotubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Veta Jimbo la Ulyankulu wilayani Kaliua Mkoani Tabora leo August 11.2017, ambapo amewataka wananchi waliopewa uraia kuheshimu sheria za nchi vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria. |
SERIKALI YASITISHA UTOAJI WA MAENEO MAPYA YA UTAWALA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imesitisha zoezi la kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.
"Kwa sasa tumesitisha kutoa maeneo mapya ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na Halmashauri mpya, zikitengamaa tutafanya maamuzi mapya, " alisema.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Agosti 11, 2017) katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Ulyankulu na Kaliua, wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Alikuwa akijibu maombi ya wabunge wa majimbo ya Ulyankulu na Kaliua ambao walisema kuna haja ya kuigawa wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa.
Akizungumzia kuhusu migogoro baina ya wanavijiji na maeneo ya hifadhi, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na ikikamilisha zoezi hilo itatoa taarifa.
Ili kuharakisha zoezi hilo, Waziri Mkuu amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi, wasifanye upanuzi wowote hadi zoezi la kuhakiki mipaka ya hifadhi litakapokamilika.
"Tumeamua kuweka beacons katika maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita wapi. Wananchi mkiwaona watu wa hifadhi wanapita huko msigombane nao. Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya mipaka. "
"Niwasihi wanavijiji wote, vijiji vilivyomo kwenye hifadhi visiendelee kupanua maeneo yake. Mbaki hivyo hivyo hadi Serikali itakapoamua vinginevyo, " alisema.
Alisema zoezi la uhakiki wa mipaka ya hifadhi likikamilika na taarifa kutolewa, Serikali itatoa uamuzi juu ya vijiji vilivyobainika kuwa ndani ya maeneo ya Hifadhi.
Akiwa Kaliua, Waziri Mkuu alielezwa na Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Magdalena Sakaya kuwa wananchi wanashindwa kujenga makazi ya kudumu katika maeneo waliyopo kwa sababu wanatishiwa kwamba wapo hifadhini.
Waziri Mkuu alisema Serikali inafanya mapitio na ikilazimu itabidi ifanye marekebisho ya Sheria inayohusu Misitu ya Hifadhi pamoja na Sheria inayohusu masula ya Wakimbizi.
Subscribe to:
Posts (Atom)
MITANDAO YA KIJAMII
Popular Posts
-
Na. OWM, Dodoma. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, imefanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 y...
-
Wataalamu wa Afya moja wakiwa katikapicha ya pamoja wakati wa mkutano wa wataalamu wa Afya moja uliojikita katika ulinzi na usalama...
-
Na. OWM, ARUSHA Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri...
-
Washiriki wa Mkutano wa mwaka wa Wataalamu wa Maabara wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara w...
-
TAMOBA wafanya wasilisho la mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama wa Bodaboda na BajajiKampuni ya Tanzania Motorcycle and Bajaj Association (TAMOBA) imefanya wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa ...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ambaye ndiye anayesimamia Kamati ina...
-
*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sik...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo ya namna mashine zinavyochakata mifuko chakavu na ...
-
Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu H...
-
Katibu wa Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia Dodoma Bw.Meshach Bandawe akiuliza jambo kwa Kaimu Meneja wa Uwa...
Formulir Kontak
Contributors
Powered by Blogger.