*Aitaka isimamie zao hilo na kutafuta masoko, iache kutoa vibali vya ununuzi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tumbaku ni siasa na tumbaku ni uchumi na ameitaka Bodi ya Tumbaku itakayoundwa ijipange kumlinda mkulima.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Agosti 13, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya za mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia kilimo, Eng. Mathew Mtigumwe na baadhi ya wakurugenzi kutoka wizara hiyo.
Alisema wajumbe wa bodi hiyo walishatajwa lakini kwa sasa hivi wanasubiri uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo. Hata hivyo, Waziri alimwelekeza Katibu Mkuu wa Kilimo awaite wajumbe wa bodi hiyo wakutane na kumchagua Makamu Mwenyekiti wa muda ili waanze kazi ya kukutana na WETCU zao.
“Kwa sababu bodi ni ya nchi nzima, ni vema wakakutana na WETCU zao na AMCOS zao ili waanze kukusanya taarifa ya tumbaku kutoka Chunya, Namtumbo, Serengeti na mahali mengine ili wapeleke message hii ya msimu ujao,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema ili kuongeza ufanisi kwenye zao hilo, itabidi baadhi ya majukumu ya bodi yapunguzwe ikiwemo kazi ya utoaji vibali vya kusafirisha na kununua tumbaku. “Hivi kama kibali cha kuuza tumbaku ya Namtumbo kinatolewa na Bodi ambayo makao makuu yake yako Tabora, sasa utawezaje kufuatilia kutoka Tabora? Ka nini kazi hiyo isifanywe na chama kikuu cha ushirika kilichopo huo?” alihoji Waziri Mkuu.
Alionya kwamba endapo bodi itaachiwa iingie kila mahali, haitaweza kulaumiwa pindi jambo likiharibika. “Ninyi kazi yenu kubwa iwe ni usimamizi kuanzia kwenye WETCU na AMCOS zake. Simamieni masoko, hakikisheni wanaokuja kununua wako tayari kufuata mfumo uliowekwa na Serikali,” alisema.
Waziri Mkuu alisema bodi ijayo inalo jukumu pia la kushirikiana na vyuo vya utafiti ili kuhakikisha kuwa tafiti zinafanyika na kupata mbegu bora zenye kustahimili magonjwa na hali ya hewa.
Akizungumzia kuhusu upangaji wa madaraja kwenye zao la tumbaku, Waziri Mkuu alisema kuna hatua imefanyika kwani hivi sasa madaraha yamepunguzwa kutoka zaidi ya 100 yaliyokuwepo na kufikia 39. Hata hivyo, alisema wingi wa madaraja bado ni changamoto kwenye upangaji wa bei.
“Bodi na wizara lazima mzungumze na makampuni ya ununuzi na mkubaliane mfumo gani utatumika kuhusu madaraja ya tumbaku. Kazi yetu kubwa na kumlinda mkulima.”
“Wenzenu wa korosho walikuwa na madaraja mengi lakini sasa yamebakia mawili, grade 1 na grade 2 na bei ya kila daraja inajulikana kwa hiyo rahisi kumuibia mkulima,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Mzee Hassan Wakasuvi akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu kwa ziara yake alisema wameyapokea maelekezo hayo na hawatasita kuwasukuma watendaji wanaochelewa kutimiza wajibu wao.
“Miaka miwili iliyopita, tumbaku ilikuwa ni zao linaloongoza kwa kuingiza fedha za kigeni hapa nchini. Lakini hivi tumeshuka, na tumeiacha korosho ndiyo inaongoza, tumedhamiria kurudi kwenye nafasi yetu, na hatutasita kuwaweka pembeni watendaji wa Serikali wataotuchelewesha kufikia azma yetu hiyo,” alisema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku nne na ameahidi kurudi kumalizia wilaya za Nzega, Igunga na Tabora Manispaa ambazo hakuzitembelea.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.