Tuesday, August 29, 2017

WAZIRI MKUU AWATAKA WAWEKEZAJI KUFUATA SHERIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watu wote wenye nia ya kutaka kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 29, 2017) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais (Uendelezaji Bishara) wa kampuni ya PIRIOU, Bw. Michel Perrin.

Waziri Mkuu amekutana na Bw. Perrin jijini Paris nchini Ufaransa kupitia ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa. Kampuni ya PIRIOU inataka kuja nchini kuwekeza katika utengenezaji na ukarabati wa meli.

Akizungumza na muwekezaji huyo Waziri Mkuu alimshukuru kwa nia yake ya kutaka kuwekeza nchini, ambapo alimtaka afuate sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji nchini.

“Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa sababu kuna fursa nyingi. Pia ni nchi yenye amani na utulivu wa kisiasa pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo nakukaribisha sana.”

Kwa upande wake Bw. Perrin amesema ameamua kuja kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi salama na kwamba anauhakika wa kupata soko ndani ya nchi pamoja na mataifa jiraji.

Amesema anaamini uwekezaji wake nchini Tanzania utakuwa na tija, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali na pia atahakikisha anafuata sheria zote za nchi.

Pia Bw. Perrin alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Balozi Samwel Shelukindo kutokana na ushirikiano anaompa kuhusu masuala ya uwekezaji nchini.

Naye Balozi Shelukindo amesema atahakikisha anaendelea kutafuta wafanyabiashara mbalimbali na kuwashawishi waje kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.