Monday, August 21, 2017

WAZIRI MKUU AWATAKA WATANZANIA KUIMARISHA UZALENDO



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Agosti 20, 2017) wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.

Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa Taifa ni jambo muhimu.

 “Uzalendo ni muhimu sana kwa sababu tumekosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.”

Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa.

Alisema Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili kufanikisha adhma hiyo.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara wamalizapo masomo yao.

Alisema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo yao.

 “Nawaomba msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe wengine.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii.

Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema Mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina tofauti tofauti.

Awali Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Bw. Goodchance Tarimo alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao nchini humo.

Alisema wao wanaimani kubwa na Serikali na wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika  kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.