Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imesitisha zoezi la kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.
"Kwa sasa tumesitisha kutoa maeneo mapya ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na Halmashauri mpya, zikitengamaa tutafanya maamuzi mapya, " alisema.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Agosti 11, 2017) katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Ulyankulu na Kaliua, wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Alikuwa akijibu maombi ya wabunge wa majimbo ya Ulyankulu na Kaliua ambao walisema kuna haja ya kuigawa wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa.
Akizungumzia kuhusu migogoro baina ya wanavijiji na maeneo ya hifadhi, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanya uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na ikikamilisha zoezi hilo itatoa taarifa.
Ili kuharakisha zoezi hilo, Waziri Mkuu amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi, wasifanye upanuzi wowote hadi zoezi la kuhakiki mipaka ya hifadhi litakapokamilika.
"Tumeamua kuweka beacons katika maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita wapi. Wananchi mkiwaona watu wa hifadhi wanapita huko msigombane nao. Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya mipaka. "
"Niwasihi wanavijiji wote, vijiji vilivyomo kwenye hifadhi visiendelee kupanua maeneo yake. Mbaki hivyo hivyo hadi Serikali itakapoamua vinginevyo, " alisema.
Alisema zoezi la uhakiki wa mipaka ya hifadhi likikamilika na taarifa kutolewa, Serikali itatoa uamuzi juu ya vijiji vilivyobainika kuwa ndani ya maeneo ya Hifadhi.
Akiwa Kaliua, Waziri Mkuu alielezwa na Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Magdalena Sakaya kuwa wananchi wanashindwa kujenga makazi ya kudumu katika maeneo waliyopo kwa sababu wanatishiwa kwamba wapo hifadhini.
Waziri Mkuu alisema Serikali inafanya mapitio na ikilazimu itabidi ifanye marekebisho ya Sheria inayohusu Misitu ya Hifadhi pamoja na Sheria inayohusu masula ya Wakimbizi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.