Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji thamani na Huduma za Kifedha Vijijini(MIVARF), imefanikiwa kupunguza umasikini wa kipato na kuimarisha uhakika wa chakula katika Halmashauri 73 zinazotekeleza program hiyo kwa Tanzania Bara na Visiwani.
Akiongea wakati wa Mkutano wa wadau wa MIVARF wa siku mbili tarehe 29 hadi 30, Agosti, 2017 mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya uratibu wa shughuli za serikali Ofisi ya Wazir Mkuu, Obey Assery alifafanua kuwa lengo la Program hiyo inalenga kuongeza uzalishaji na tija kwa walengwa.
“Program imelenga kuwajengea uwezo wazalishaji ambao huwa katika vikundi kwa kuvifiki vikundi 2,331 vyenye walengwa 81,677. Kimsingi Programu imelenga kumuwezesha mkulima aweze kufanya kilimo cha kibiashara” alisema Assery.
Naye Mratibu wa Program Kitaifa, Walter Swai alibainisha kuwa Program imelenga kuwajengea uwezo walengwa kuyafikia masoko ya uhakika ili waweze kupunguza umasikini wa kipato.
“Programu imelenga kuboresha 1,000km za barabara hadi sasa 9991.8km zimeshakamilika sawa na asilimia 92. Lakini pia kwa upande wa miundo mbinu ya masoko tunajenga maghala, hadi sasa kati ya maghala 29 yaliyo kwenye malengo tayari tumekamilisha maghala 24 sawa na asilimia 83 ” alisistiza Swai.
Swai aliongeza kuwa Program hiyo imepanga kukarabati maghala 6 ambapo tayari yote yamekamilika, pia tumelenga kujenga masoko 16 ambapo hadi sasa masoko 7 yamekamilika ambayo ni asilimia 44.
MIVARF; ni Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini iliyobuniwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo yaani (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.