Friday, August 4, 2017

BILIONI 10 KUTUMIKA KUBORESHA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA


Serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya kufanya uboreshaji wa daftari hilo utakaojikita katika kufanya mapitio ya mifumo ya menejimenti ya Uchaguzi.

Akiongea mara baada ya kufanya mazungumzo na watendaji wa Tume hiyo na kufanya ziara katika bohari ya kuhifadhi vifaa vya uandikishaji wapiga kura na uendeshaji shughuli za kupiga kura, tarehe 4 Agosti, 2017, jijini Dar es Salaam,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (Mb) alibainisha kuwa ameridhishwa na maandalizi ambayo Tume hiyo imeyafanya.
Uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini, unazingatia katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ibara ya 5 (3) ambapo uazishwaji wa Daftari laKudumu la Wapiga Kura nchini unatambuliwa, lakini Ibara ya 74 (6) kinaipa tume hii madaraka ya kuchukua jukumu la kuandikisha wapiga kura wa Tanzania, pia kifungu cha 15 (3) cha sheria ya Tume ya Uchaguzi kinaipa madaraka Tume hii kutengeneza mfumo na utaratibu kuandikisha wapiga kura pamoja na uboreshaji wa mifumo hiyo, kifungu hicho kinasisitiza kuwa Daftari hilo lazima liboreshwe mara mbili kabla ya uchaguzi mkuu.” Alisema Mhagama

Mhagama alifafanua kuwa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu inaelekea katika Uchaguzi mkuu mwaka 2020 hatunabudi kuzingatia matakwa ya katiba ya nchi yetu na sheria ya Tume ya Uchaguzi ambayo inasimamiwa na Tume ya Uchaguzi nchini ambapo serikali inahakikisha tume hiyo inapata mahitaji yake ya kimsingi.

Tume hii ni huru, hivyo Bunge limepitisha fedha hizo kwa ajili ya Tume kuanza kufanya maadalizi ya kuboresha Daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa mara ya kwanza na itafanyika tena mara ya pili kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Lazima Tume ipitie upya mifumo yake na kuiboresha lakini pia kuangalia na vifaa ilivyonavyo. Nimeridhika na  mpango kazi wa tume wa kukamilisha kazi hiyo kwa ufanisi na weledi mkubwa, sisi kama serikali tutawasaidia katika maeneo yote ambayo kikatiba tunaruhusiwa kushirikiana nao katika utekelezaji wa majukumuyao”alisistiza Mhagama.

Mkurugenzi wa Uchaguzi,Tume ya  Uchaguzi Tanzania, Ramadhani Kailima alibainisha kuwa Tume hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa inaboresha daftari la wapiga kura kwa wakati lakini na kwa kutumia mifumo bora ya uandikishaji. Aliongeza kuwa kwa kipindi hicho Tume itatoa kadi mpya ya mpiga kura kwa watakaoandikishwa upya, waliopoteza kadi na kadi zilizoharribika, kwa wanaohamisha taarifa zao ikiwemo waliohamia Dodoma, na kufuta wapiga kura waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura.

“Tumeshaanza maandalizi ya awali ya kuboresha Daftari la Wapiga kura ambapo tunatekeleza jukumu hili kwa kuzingatia mpango kazi ambao tumeuweka katika tume yetu hivyo tunaamini mara tu serikali itakapo tupatia kiasi cha fedha ambacho imekitenga kwa shughuli hii sisi tutaendelea kutekeleza majukumu yetu ya menejimenti ya uchaguzi  hasa kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa kufanya mapitio ya mifumo ya uandikishaji na kuchakata picha” alisema Kailima

Kailima aliongeza kuwa pamoja na uboreshaji waDaftari la Kudumu la Wapiga Kura, tume hiyo inaamini kuwa kila mwananchi ana haki ya kuelimishwa hivyo imeandaa mpango mkakati wa kutoa elimu kwa mpiga kura utakaolenga kutoa elimu shuleni kwakuwa wanafunzi hao ndio wapiga kura wa baadae.

Awali akiongea katika ziara hiyo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Maimuna Tarishi alibainisha kuwa ofisi ya Waziri Mkuu inadhamana ya kuisaidia Tume kwa misingi ya kikatiba tu, hivyo itahakikisha kuwa taasisi za serikali ambazo zinawajibika kuisaidia Tume hiyo zinatekeleza majukumu yake zinawajibika ipasavyo ili mpango kazi wa Tume iliojiwekea unatekelezeka kwa ukamilifu.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni miongoni mwa Taasisi ambazo zipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi hiyo ni Taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 1993 chini ya Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.