![]() |
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu Prof. Faustin Kamuzora (Sera na Uratibu) akimsikiliza kwa makini Balozi wa
Philippine Ariel Norman R. Garibay akisisitiza jambo kuhusu masuala ya maafa
walipokutana ofisini kwake tarehe 22 Januari, 2018.
|
Home
All posts
Monday, January 22, 2018
BALOZI WA UFILIPINO AFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA NA URATIBU) KUHUSU MASUALA YA MAAFA
Sunday, January 21, 2018
MAJALIWA AHITIMISHA ZIARA YA MKOA WA MARA
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua mabweni mawili ya Magufuli na Majaliwa katika Shule ya Sekondari ya Bumagi wilayani Butiama Januari 20, 2018. Watatu kulia ni mkewe Mary. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhungo katika mkutano wa hadhara aliouhutubia kwenye kijiji cha Muragi Januari 21, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza alikopitia akitoka Musoma kwenda Dar es salaam Januari 21, 2018. |
Saturday, January 20, 2018
WAZIRI MKUU ATEMBELEA SHAMBA LA JKT RWAMKOMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua shamba la uzalishaji wa mbegu bora za mihogo aina ya mkombozi linalomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Rwamkoma wilayani Butiama.
Amekagua shamba hilo linalomilikiwa na Kikosi cha JKT Rwamkoma leo (Jumamosi, Januari 20, 2018) alipowasili wilayani Butiama akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara. Kikosi hicho kimewezeshwa na Halmashauri ya Butihama.
Waziri Mkuu amewakipongeza kikosi cha JKT Rwamkoma kwa uamuzi huo wa kuzalisha mbegu bora za mihogo ambazo baadae zitasambazwa kwa wakulima wa zao hilo wilayani hapa.
Pia amewataka wakazi wanaoishi karibu na shamba la kikosi hicho hilo kulitumia kama shamba darasa kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kulima zao hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi hicho Luteni Kanali David Msakulo alisema shamba hilo linaukubwa wa ekari 60, na mbegu zitakazozalishwa zitatosha kupanda ekari 900.
Mkuu huyo wa kikosi hicho aliongeza kuwa mbegu hizo zinazozalishwa katika shamba hilo zitagawanywa kwa wakulima katika kata zote 18 za wilaya ya Butihama.
Alisema mbali ya kuzalisha mbegu pia wanatarajia kuanzisha kiwanda cha kuchakata zao la mihogo ili kuweza kuliongezea thamani.
Mbali na shamba la mbegu bora za mihogo pia kikosi hicho kina shamba lingine la pamba lenye ukubwa wa ekari 57, ambapo wanatarajia kuvuna tani 57 za pamba. Mwakani wanatarajia kuongeza ukubwa wa shamba na kufikia ekari 300.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea shamba darasa la mkoa wa Mara la zao la pamba lililopo Kisangwa wilayani Bunda akiwa njiani kuelekea wilayani Butihama, kuendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima alisema shamba darasa hilo ni moja ya jitihada za Mkoa wa Mara kuelimisha wakulima wa zao hilo mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.
MAJALIWA AMTEMBELEA MAMA MARIA NYERERE NA KUTOA HESHIMA KWENYE KABURI LA BABA WA TAIFA
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakizungumza na Mama Maria Nyerere wakati walipomtembelea nyumbani kwake Mwitongo, Butiama Januari 20, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakizungumza na Mama Maria Nyerere wakati walipomtembelea nyumbani kwake Mwitongo, Butiama Januari 20, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama Januari 20, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Mwenge katika kijiji cha Butiama Januari 20, 2017. |
WAZIRI MKUU AMUAGIZA RAS MARA KUKAGUA HALMASHAURI YA BUTIAMA
*Ni kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalumu katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama.
Amesema Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kutumia fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo zinazotolewa na Serikali katika shughuli nyingine jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Januari 20, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Bitiama katika ukumbi wa chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere cha Mara.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchunguzwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Butiama Bw Solomon Ngiliule pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri Bw. Masanja Sabuni na Ofisa Manunuzi wa Halmashauri hiyo Bw. Robert Makendo.
Alisema viongozi hao wanatakiwa wachunguzwe kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali zikiwemo sh. milioni 12 walizotumia kuandaa profile ya Halmashauri hiyo.
Waziri Mkuu alisema fedha zingine ni pamoja na sh. milioni 70 za elimu maalumu, sh. milioni 288 za mradi wa maji Butiama ambazo zote hazijulikani zimetumikaje. “Hatuwezi kuvumilia vitendo hivi fanyeni uchunguzi na naomba taarifa yake mara mtakapokamilisha.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara imkamate na kumuhoji Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoani Mara, Mhandisi Peter Salim baada ya kushindwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Butiama.
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali ilitoa sh milioni 600 Aprili, 2017 kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya wilaya hiyo lakini hadi sasa wakala huo haujafanya kazi yoyote.
Katika maelezo yake Mhandisi Salim alisema ujenzi wa ofisi hiyo hadi kukamilika utagharimu sh. bilioni tatu, kati ya sh. milioni 600 zilizotolewa na Serikali sh milioni 400 zimetumika kujengea msingi, kauli ambayo ilipingwa na Mkuu wa wilaya hiyo Bibi Anna-Rose Nyamubi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu siyo kweli kwamba kuna kazi inayoendelea bali kilichopo pale ni mashimo ambayo hayajulikani ni ya nini. Pia kuna jengo moja lilijengwa kwa mabati kama stoo na hakuna mafundi wanaoendelea na kazi"
Waziri Mkuu alisema kuwa Serikali iko katika mchakato wa kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi za watumishi na kwamba haitamvumilia mtu yeyote atayekwamisha juhudi hizo.
Waziri Mkuu baada ya kuwasili wilayani Butiama akiambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa walizuru kaburi la Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere, katika Kijiji cha Mwitongo na kufanya mazungumzo na mjane wa Baba wa Taia, Mama Maria Nyerere.
Baada ya kuwasili katika eneo alilozikwa Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu na Mkewe waliweka shada la maua juu ya kaburi na kisha walishirikiana na wananchi kufanya maombi yaliyoongozwa na Chifu wa Wazanaki, Japheth Wanzagi.
Pia Waziri Mkuu alihutubia wakazi wa wilaya ya Butiama kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwenge, ambapo alitumia fursa hiyo kueleza juhudi mbalimbali za kuwaletea maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.
Friday, January 19, 2018
SERIKALI YAKATAZA KULIMA PAMBA KWA MKATABA-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imekataza kilimo cha pamba cha mkataba kwa sababu kinawanyonya wakulima.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua zahanati ya Hunyari wilayani Bunda, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.
“Ni marufuku kwa wanunuzi wa pamba kulima pamoja na wakulima kwa sababu wakulima wanakosa uamuzi wa kupanga bei. Kuanzia sasa zao hilo litauzwa kwa njia ya mnada.”
Amesema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa kilimo cha zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Kilimo katika wilaya hiyo wawafuate wakulima vijijini kwa ajili ya kutoa elimu itakayowawezesha wakulima kulima kwa kufuata njia bora za kisasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo lao.“Marufuku kulisha mifugo katika mashamba ya watu.”
Amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mfugaji yeyote atakayelisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima kwani tabia hiyo huchangia migogo baina yao.
WAZIRI MKUU AMKABIDHI MKURUGENZI WA MUWASA KWA TAKUKURU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameamuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mara kumkamata na kumuhoji Mkurugenzi Mtendani wa Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA) Mhandisi Gantala Said kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji Bunda.
Mbali na Mkurugenzi huyo pia TAKUKURU inawashikilia wakandarasi wanaojenga mradi huo ambao ni Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Nyakirang'anyi Bw Mauza Mmangi ambaye ndiye mkandarasi anajenga mradi huo unaotoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye eneo la Nyabehu hadi Bunda mjini.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na Mhasibu wa Kampuni ya Ujenzi ya Nyakirang'anyi Bw. Amon Gideon pamoja na viongozi wa kampuni nyingine ya ujenzi ya Fortrss Bw. Juvenari Chirianga na Ephraim Mpeko ambao nao walishiriki katika ujenzi wa mradi huo.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo jana jioni (Ijumaa, Januari 19, 2018) baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kueleza sababu zilizosababisha mradi wa maji Bunda kutokamilika pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi.
Akizungumza katika kikao maalumu cha kujadili changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, alichokiitisha mjini Bunda, Waziri Mkuu alisema alimua kuitisha kikao hicho baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo hususan inayosimamiwa na MUWASA .
Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.
Waziri Mkuu amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kupitiwa upya kwa mradi huo kwa sababu hafurahishwi na ujenzi wake.” Kama Mkurugenzi wa MUWASA anasema mradi umekamilika kwa asilimia 98 sasa kwa nini wananchi walalamikie kukosa huduma hiyo.”
Alisema Mkurugenzi huyo amekuwa akimlipa mkandarasi fedha kabla ya kufanya kazi ambapo hadi sasa tayari mkandarasi anayenga mradi huo ameshalipwa zaidi ya sh. bilioni saba na mradi haujakamilika na wananchi wanaendelea kutumia maji ambayo siyo salama.
Waziri Mkuu alisema viongozi hao wahojiwe na wakibainika kuhusika na ubadhilifuu wa fedha za mradi huo, wachukuliwe hatua kali za kisheria.”Serikali imedhamiria kuimarisha huduma za maji, hivyo hatuhitaji mtu atakayeenda kinyume na mpango huo.”
Mradi wa kupeleka maji kwenye mji wa Bunda maji kutoka ziwa Victoria katika eneo la Nyabeho ulisanifiwa mwaka 2006 na ulikuwa unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha za maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Malima aliagiza kufungwa na ofisi za MUWASA na kuwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutoruhusiwa kuingia ofisini hadi hapo uchungi utakapokamilika.
Thursday, January 18, 2018
SERIKALI KUMALIZA MGOGORO WA NYAMONGO-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria
kumaliza mgogoro ulipo kati ya wananchi wa Kata ya Nyamongo na muwekezaji wa
mgodi wa North Mara.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi pamoja na
mwekezaji wa mgodi huo wanaishi na kuendesha shughuli zao za kimaendeleo kwa
kufuata sheria za nchi.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 18, 2018) wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya
Nyamongo, wilayani Tarime.
Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi na
wawekezaji wakigombana, inataka kumaliza mgogoro huo ili pande zote zifanye kazi
zake kwa amani.
Katika kuhakikisha mgogoro huo unakuwa historia Waziri Mkuu
ameitisha kikao kitakachowakutanisha wawakilishi wa wananchi , viongozi wa
mgodi na mbunge wa jimbo la Tarime Bw. John Heche.
Amesema katika hicho kitakachofanyika Januari 28, 2018 Ofisini
kwa Waziri Mkuu mjini Dodoma, ambapo aliwakikishia wananchi hao kwamba Serikali
italinda maslahi yao.
Awali, Waziri Mkuu
alitembelea kata ya Nyamwaga na kukagua kituo cha afya cha Nyamwaga, ambapo
amesema kinatosha kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya.
Hivyo amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Francis
Mwanisi aanze mchakato wa kupeleka vifaa katika kituo hicho ili wananchi wa
Halmashauri ya Tarime waanze kutibiwa.
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Magufuli ameongeza bajeti ya
ununuzi wa dawa na kufikia sh. bilioni 269 ili kuhakikisha hakuna mgonjwa
anayekwenda hospitali na kukosa dawa.
Amesema mbali na kuongeza bajeti katika ununuzi wa dawa, pia
ameziagiza halmashauri zote kuhakikisha suala la utoaji wa vitambulisho kwa
wazee ili watibiwe bure linatekelezwa.
WANAOISHI MAENEO HATARISHI KUHAMISHWA CHEMBA
SERIKALI wilayani Chemba mkoani Dodoma imesema kuwa imepanga kuwahamisha watu wanaoishi maeneo hatarishi ya kupata mafuriko kutokana zaidi ya kaya 2,000 zimezungukwa na maji katika kata ya Mrijo hadi hivi sasa.
Akiongea wakati akitoa taarifa kwa waratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliokwenda kufanya tathimini ya maafa yaliyotokana na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo, mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga alibainisha kuwa mkakati wa muda mrefu walionao ni kuwatafutia wakazi hao maeneo salama.
Odunga Alisema kuwa kwa sasa kamati za maafa zimechukua hatua ya kukabili maafa ya mafuriko kutokana na idadi ya nyumba zilizozungukwa na maji imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivyo wameanzisha kambi maalum kwa watu ambao nyumba zao zimeanguka kutokana na maafa hayo.
Aliongeza kuwa msaada wa haraka unahitajika kutokana na waathirika hao wa mafuriko kutumia baadhi ya majengo ya madarasa ambayo yanapaswa kutumiwa na wanafunzi ambao wanajiunga na masomo mwaka huu.
“kwa sasa tunahitaji sana mahema, mataulo, mashuka , chakula pamoja na madawa kwajili ya kuwahudumia hawa watu ambao tunao hapa na tukipata vifaa hivyo basi tutaondoka hapa na kwenda kutengeza kambi sehemu nyingine ambayo tumeiandaa maaluum kwajili ya kuwahifadhi hawa watu na kuacha haya madarasa kwajili ya matumizi ya wanafunzi” alisema Odunga.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa tayari wilaya imeshaunda kamati mbalimbali ambazo zinahusika katika kusaidia wahanga hao kuwa salama kiafya kwa kuchukua tahadhari zinazoweza kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Naye mratibu wa maafa kutoka ofisi ya waziri mkuu Ally Mwatima, alisema kuwa mahitaji yote ambayo yameanishwa na mkuu huyo wa wilaya wameyachukua na watayawasilisha ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema iwezekanavyo.
“Kwanza niwapongeze kwa kukabili maafa kwa mujibuwa sheria,kanuni namiongozo ya menejimentiya maafa, hali hii imesaidia kuokoa maisha ya hawa wenzetu na mahitaji yote mliyobainisha ni ya msingi sana hivyo tutakwenda kuonana pia na kamati ya maafa mkoa ili kuweza kuona na sisi tunaongeza nguvu katika vitu gani vya msingi ambavyo vitawasadia hawa wenzetu”alisema Mwatima.
| Baadhi ya nyumba ambazo zimezungukwa na maji katika kata ya Mrijo wilayani Chemba kutokana na maafa ya mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyenya wilayani humo. |
| Baadhi ya waathirika wa maafa ya mafuriko wakiwa katika kambi ya muda iliyo andaliwa na kamati ya maafaya wilaya ya Chemba kutokana na thari za maafa ya mafuriko wilayani humo. |
Wednesday, January 17, 2018
WAZIRI MKUU ASIMAMISHA UUZAJI WA MALI ZA KNCU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro Bibi Anna Mghwira asitishe uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika
cha Kilimanjaro (KNCU).
Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa
Serengeti, wilayani Tarime.
Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa
ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza
sharti la mtaji la Benku Kuu ya Tanzania (BoT).
Benki hiyo ya KCBL inatakiwa kutimiza sharti la kuwa na mtaji kamili
unaotosha wa shilingi bilioni tano (5) katika
kipindi cha miezi sita tangu kutolewa kwa tangazo hilo.
Waziri Mkuu alisema ni marufuku kuuza mali za Ushirika huo, hususan
katika kipindi hiki ambacho Serikali inafanya uhakiki wa mali za vyama mbalimbali
vya Ushirika nchini.
Alisema
Serikali imedhamiria kuimarisha Ushirika nchini na sasa inafanya uhakiki wa mali
za vyama vya Ushirika na watakaobainika kuhusika na ubadhilifu watachukuliwa
hatua.
Januari
4, 2018 BoT ilizipa miezi sita benki tatu ili ziweze kuongeza kiwango cha mtaji
unaohitajika kutokana na matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji kamili wa
kutosha.
Benki
hizo ni Kilimanjaro Co-Operative Bank Limited, Tanzania Women Banki Plc na
Tandahimba Community Bank Limited, zitakaposhindwa kutekeleza agizo
zitachukuliwa hatua.
BoT ni
itazifutia leseni na kusimamisha shughuli za kibenki chini ya ufilisi, iwapo
benki hizo zitashindwa kutekeleza agizo hilo ihadi kufikia Juni 30, 2018.
WANAUME WA TARIME ACHENI UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa wanaume wa wilaya ya Tarime
kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuachana
na kilimo cha bangi.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa
Serengeti, wilayani Tarime.
Waziri Mkuu alisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na
watoto pamoja na kilimo cha bangi vinaitia doa wilaya hiyo, hivyo hawana budi wakaepukana
navyo.
“Serikali inakemea vitendo vya ukatili, achaneni navyo. Mtu
unamchapa mtoto makofi hadi anazimia, kitendo hicho hakiwezi kuvumilika na pia
kinaitia doa wilaya yenu.”
Wakati Huo huo, Waziri Mkuu alimuagiza
Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Glorious Luoga kuendelea na msako wa mashamba ya bangi
na mirungi na kuchukua hatua kwa watakaobainika kuendesha kilimo hicho.
Alisema ardhi ya wilaya hiyo ni nzuri na inahimili kilimo cha mazao
mbalimbali ya chakula na biashara kama mahindi, mihogo, ndizi, kahawa, pamba,
ni marufuku kulima bangi.
Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchukuliwa hatua kwa wakandarasi
waliotekeleza ujenzi wa maji mkoani Mara kwa sababu miradi hiyo wameijenga
chini ya kiwango.
Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya
wananchi kupitia mabango wakidai kutonufaika na miradi ya maji katika maeneo
yao licha ya Serikali kutoa fedha.
SIJARIDHISHWA NA UJENZI WA KITUO CHA SIRARI-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.
Kufuatia hali hiyo amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) afike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma akiwa na mkandarasi aliyejenga kituo hicho.
“Serikali haiwezi kuvumilia ujenzi wa hovyo kiasi hiki, namtaka Kamishna wa TRA aje ofisini kwangu Januari 25, 2018 pamoja na mkandarasi aliyejenga kituo hiki akiwa na nyaraka zote za ujenzi wa jengo hilo.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) mara baada ya kumaliza kukagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Waziri Mkuu amesema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.
Waziri Mkuu amejionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia sheria na wajiepusha na biashara za magendo.
Waziri Mkuu amesema magendo yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa nchini kwa njia za magendo itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri kilichotumika.
Pia Waziri Mkuu ametembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Borega, ambapo amewasisiza wananchi wasimamie elimu ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.
Amesema Serikali imeweka sheria kali kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au kumoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.
WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA MIAKA MITATU
*Ni wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambao umedumu kwa miaka mitatu.
Ametoa uamuzi huo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Amesema amesitisha mpango huo wa ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kwa kuwa imepangwa kujenga katika eneo ambalo lipo mbali na wananchi.
“Ninazo taarifa kuwa mnataka kujenga katika eneo ambalo litaigharimu Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya fidia na pia lipo mbali na makazi ya wananchi.”
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuruhusu ujenzi huo ufanyike katika eneo ambalo ni mbali ya makazi ya wananchi kwa kuwa watashindwa kufuata huduma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itapeleka wataalamu watakaofanya uchunguzi na bainisha eneo sahihi la kujenga Halmashauri hiyo kwa kutumia ramani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kutotamani fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesisitiza kwamba wasipokuwa makini na fedha hizo zitasababisha wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini. ”Je mpo tayari kuchukuliwa hatua.?
Amesema Serikali inapeleka fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi na si kuwanufaisha watu binafsi.
Pia amewataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe wabunifu na wajue halmashauri zao zinahitaji nini ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo.
Waziri Mkuu ambaye leo ameendelea na ziara yake Mkoani Mara kwa kutembelea wilaya ya Tarime ambapo baada ya kuzungumza na watumishi alikagua hopitali ya Tarime na kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha Sirari.
Tuesday, January 16, 2018
WAHUJUMU WA MIRADI YA MAJI MARA KUCHUKULIWA HATUA-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhujumu ujenzi wa miradi ya maji mkoani Mara.
Hatua hiyo imetokana na kutoridhishwa na utekelezwaji wa ujenzi miradi ya maji katika baadhi ya halmashauri za mkoa huo,hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma hiyo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 16, 2018) wakati alipokagua mradi wa maji wa Utegi uliopo katika kijiji cha Mika wilayani Rorya.
Amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Waziri Mkuu amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
“Nitafuatilia katika maeneo yote ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji kinalingana na thamani halisi ya miradi husika.”
Waziri Mkuu amesema anakerwa na Halmashauri ya wilaya ya Rorya kutosimamia vizuri miradi ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutozingatia sheria.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya wanaoshi wilayani Tarime wawe wamehamie Rorya ifikapo Februari 15, 2018.
“Atakayeng’ang’ania kuishi Tarime hadi siku hiyo atakuwa amejiondoa kazini mwenyewe. Lazima watumishi wote waishi kwenye vituo vyao vya kazi Rorya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”
Pia Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ulimaji wa bangi pamoja na uvuvi haramu na badala yake wafanye shughuli halali za kuwaingizia vipato.
WAZIRI MKUU AMKABIDHI MHANDISI WA MAJI KWA NAIBU WAZIRI TAMISEMI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Mhandisi Obetto Sasi kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Josephat Kandege baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Ametoa uamuzi huo jana jioni (Jumanne, Januari 16, 2018) wakati aliposimamishwa na umati wa wananchi kwenye mji Mdogo wa Shitari alipokuwa njiani kuelekea kwenye kijiji cha Bubombi wilayani Rorya.
“Hatuwezi kuwa na mtumishi wa aina hii ambaye kila eneo tunakutana na changamoto za maji huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya Serikali kutoa fedha, hivyo namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa alete mhandisi mwingine wa maji.”
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Rorya na kukagua mradi wa maji katika mji Mdogo wa Shirati na kuona namna ya kuutekeleza.
Amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Maliwa alimueleza Waziri Mkuu kwamba changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa huo inatokana na watendaji wa idara hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kiutendaji.
Wilaya ya Rorya inatekeleza miradi 11 ya maji ya bomba kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RWSSP) katika vijiji vya Kinesi, Randa, Utegi, Mika,Kirogo, Nyihara, Kisumwa,Nyamkonge, Nyambori, Gabimori na Marasibora.
Monday, January 15, 2018
ATAKAYEBAINIKA KUTAFUNA SH. MILIONI 320 ZA IMARA SACCOS ACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Musoma Bibi Yunia Wiga kufuatilia upotevu wa sh. milioni 320 za Imara SACCOS na atakayebainika kuhusika ashughulikiwe.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 15, 2018) alipopokea malalamiko ya wanachama wa SACCOS hiyo kupitia mabango waliyoyawasilisha katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini Musoma.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku sita, alimuagiza ofisa huyo kukutana na uongozi na wanachama wa SACCOS hiyo leo mchana na kisha kumpa majibu juu ya upotevu wa fedha hizo pamoja na sh. milioni 40 za hisa ifikapo Januari 20, 2018.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bibi Fidelica Myovella kuhakikisha anatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi mbalimbali waliopisha miradi ya maendeo katika Manispaa hiyo.
Waziri Mkuu alisema siyo vizuri kwa halmashauri kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kama barabara, standi na kisha kukaa muda mrefu bila ya kuwalipa fidia zao.
Aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha daladala cha Bweri ambao hawajalipwa fidia zao tangu mwaka 2013. Mkurugenzi huyo aliahidi kuanza kulipa madeni hayo kuanzia mwezi Januari, 2018.
Awali, Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini, Bw Vedastus Mathayo aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza baadhi ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni ikiwemo ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Bw. Mathayo alisema wananchi wa jimbo hilo kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ahadi hiyo.
Mbali na mradi wa maji pia Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo ya ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami pamoja na ukarabati wa kiwanja cha ndege unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Waziri Mkuu alisema ahadi zote zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 na zile zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli zitatekelezwa, hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
MAJALIWA:SERIKALI KUTASUBIRI KUWAUNDIA TUME WEZI, MAFISADI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini wasijihusishe na vitendo vya wizi, ufisadi kwani Serikali haitosubiri kuwaundia tume za kuwachunguza bali itawashughulikia hapo hapo.
Amesema Serikali haikotayari kuwavumilia watumishi wanaojihusisha na wizi, ubadhilifu, rushwa na uzembe, hivyo ni vema viongozi waliopewa dhamana wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Musoma mkoani Mara akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani hapa.
“Fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinalenga kutatua kero za wananchi na si kuwanufaisha wachache wenye tamaa. Kama ni za ujenzi wa zahanati ijengwe na atakayezitafuna Serikali haitosita kumchukulia hatua.”
Waziri Mkuu asiwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa sharia kwa sababu vitendo vya wizi, uzembe vinachangia kupunguza kasi ya kuwaletea maendelea maendeleo Watanzania.
Alisema lengo ni kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan ni wale wa hali ya chini inatimia, hivyo aliwaagiza viongozi wa halmashauri wakiwemo Madiwani kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.
Pia Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa idara na watendaji wengine wa halmashauri kuacha tabia ya kukaa ofisini na dabala yake waende vijijini kwa ajili ya kuwafuata wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Waziri Mkuu alisema watendaji hao wanatakiwa waachane na tabia ya kuwasubiri wananchi wawapelekee malalamiko yao kwa sababu baadhi yao hawana uwezo wa kufika katika ofisi zao.
Subscribe to:
Posts (Atom)
MITANDAO YA KIJAMII
Popular Posts
-
Na. OWM, Dodoma. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, imefanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 y...
-
Wataalamu wa Afya moja wakiwa katikapicha ya pamoja wakati wa mkutano wa wataalamu wa Afya moja uliojikita katika ulinzi na usalama...
-
Na. OWM, ARUSHA Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri...
-
Washiriki wa Mkutano wa mwaka wa Wataalamu wa Maabara wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara w...
-
TAMOBA wafanya wasilisho la mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama wa Bodaboda na BajajiKampuni ya Tanzania Motorcycle and Bajaj Association (TAMOBA) imefanya wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa ...
-
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia sukari, alipotembelea kiwanda cha Kilombero Sugar, kilichopo katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Mo...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ambaye ndiye anayesimamia Kamati ina...
-
*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sik...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo ya namna mashine zinavyochakata mifuko chakavu na ...
-
Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu H...
Formulir Kontak
Contributors
Powered by Blogger.






