Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya sera, bunge na uratibu Dkt. Jim Yonazi amewakumbusha
watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa
ushirikiano, upendo, furaha na amani ili kuyafikia malengo ya ofisi hiyo.
Dkt. Yonazi ametoa kauli hiyo
wakati akizungumza na Watumishi Ofisi yake wakati wa mkutano wake na watumishi
hao uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
iliyopo Njedengwa Jijini Dodoma.
Dkt. Yonazi amesema ipo haja
ya kila mtumishi kujifanyia tathmini katika utendaji wake wa kazi huku
akizingatia miongozo na kanuni za utumishi wa umma na kusema kuwa, kila
mtumishi anawajibika katika kuhakikisha ofisi inapata matokeo iliyoyakusudia na
kwa ufanisi.
“Ni wakati sahihi kila mmoja
kuilinda furaha aliyonayo awapo mahali pa kazi, isingefaa utoke nyumbani huna
furaha na ufike eneo la kazi ukose furaha, ni vyema kuja eneo la kazi na
kuipata furaha mara mbili kwa kuzingatia
mazingira yaliyorafiki katika kutekeleza majukumu,” alisema Dkt. Yonazi
Aliongezea kuwa kila mtumishi
wa umma awe na desturi ya kuheshimu nafasi ya mwingine bila kujali tofauti
zinazoweza kuwepo miongoni mwa watumishi hao.
“Ni vyema kila mtu akajali
mwingine na ikumbukwe hakuna mtu mwenye uwezo mdogo wa kufanya kazi, jambo la
msingi ni kuhakikisha ule uwezo uliopewa na Mwenyezi Mungu na Mafunzo
mbalimbali unatumia vizuri na kuhakikisha unaleta matunda mazuri na kuleta
maendeleo kwa Nchi yetu” alisema Dkt, Yonazi.
Sambamba na hilo aliwaeleza
watumishi hao kuwa kila mmoja ni kiongozi katika eneo lake la kazi hivyo abebe
dhamana hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa.
“.....kila mtumishi aliyepo
hapa ndiye Katibu Mkuu kwenye eneo lake, kwa kubeba imani ya kwamba ni Katibu
Mkuu anapaswa kuwa na nidhamu na bidii katika kazi ikiwa ni pamoja na kuwa
mwaminifu,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. James Kilabuko katika neno lake la utangulizi amewaasa
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi na
kuzingatia sheria za utumishi wa Umma huku akiwasihi kuimarisha umoja na
mshikamano ili kuiletea Serikali maendeleo yake.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi
la Ofisi ya Waziri Mkuu Bi, Numpe Mwambenja ameomba watumishi kuendelea
kujitathimini mienendo yao katika utumishi wa Umma kwa kufanya kazi vizuri na
nidhamu na kuheshimu viongozi huku wakiheshimiana wao kwa wao.
Bi. Numpe alitumia nafasi hiyo
kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna unavyojali maslahi ya
watumishi na ustawi wao kwa ujumla na kuwasihii watumishi kuendelea kutimiza
wajibu kwa kuzingatia kauli ya “hakuna haki bila wajibu”.
Read More