Thursday, December 7, 2017

WAZIRI MKUU AFUNGUA JENGO LA UMOJA WA MATAIFA

  •  
    Ni taasisi ya kwanza ya Kimataifa kuwa na Ofisi Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua ofisi ya Umoja wa Mataifa na kusema uamuzi huo ni hatua muhimu ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamsi, Desemba 7, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa taasisi za Umoja wa Mataifa waliohudhuria hafla ya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Dodoma, katika eneo la Mlimwa, Manispaa ya Dodoma.
             
“Wote mtakubaliana nami kwamba uzinduzi wa ofisi hii ya Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu sana ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Pia, inafungua mlango mpya utakaowezesha ofisi zote za kibalozi na mashirika ya kimataifa kujenga ofisi zao hapa Dodoma na kuhamia mapema,” alisema.

Alisema anatambua kwamba kwamba wapo viongozi na watendaji wenye hofu ya kuhamia na kuanza maisha mapya Dodoma. “Baadhi ya watendaji wanaogopa changamoto za kuhamisha watoto wao na wenza wao ili kuanza maisha mapya. Napenda kuwatoa hofu kwamba Dodoma ni mahali pazuri pa kuishi na kuna fursa nyingi,” alisema.

Alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu iliyopo ya huduma za jamii na miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano ili iwe bora zaidi. Alitumia fursa hiyo kuwasihi waombe maeneo ya ujenzi kwa ajili ya ofisi na makazi.

Aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuiteua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza mfumo mpya wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuungana na kutekeleza shughuli zake kwa pamoja kama familia moja ya Umoja wa Mataifa yaani “UN Delivering as One”.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga alisema Umoja wa Mataifa unayo mashirika 50 na kwamba mashirika 23 kati ya hayo, yanafanya kazi zake hapa nchini.

Alisema wizara yake kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma, watahakikisha kuwa mashirika hayo yanapatiwa viwanja vya kutosha ili kujenga ofisi zao mapema iwezekanavyo.


Mapema, Mwakilishi Mkazi wa UNDP na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania; Bw. Alvaro Rodriguez alisema wamefurahi kupata fursa ya kuwa taasisi ya kwanza ya  kimataifa kuwa na Ofisi yake kwenye makao makuu ya nchi hapa Dodoma

“Tumefurahi kujumuika kwa pamoja hapa Dodoma, lakini tunaahidi kuwa na sisi tutahamia kwa awamu kama ambavyo Serikali imekuwa ikifanya. Hili litategemea upatikanaji wa viwanja na majengo kwa ajili ya ofisi, kwa hiyo wafanyakazi wetu nao watahamia taratibu,” alisema.

Read More

WAZIRI MKUU AMALIZA MGOGORO WA LOLIONDO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa takriban miaka 26.

Hatma hiyo imefikiwa jana (Jumatano, Desemba 6, 2017) kwenye kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake Mlimwa, Manispaa ya Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.

“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,” alisema.

Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti pamoja na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.

“Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60 waliohudhuria kikao hicho.

Vilevile, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa Serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili wadau waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.

Aliwataka Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo wafanye ziara ya kutembelea eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo. Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.
         
Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwepo mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo. Januari 2017, aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo.

Washiriki wa kikao hicho waliopata fursa ya kutoa maoni, walipongeza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini katika kutafuta suluhu la mgogoro huo.

Akichangia kwa niaba ya NGOs, Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Bi. Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.

“Huko nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai imesema vile, lakini kwa awamu hii, tumeweza kuitwa kwenye vikao mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.

Aliomba hata katika chombo kipya kitakachoundwa, kuwe na uwakilishi wa wananchi kutoka ngazi ya chini ili waweze kushiriki kikamilifu katika kupanga namna bora ya kuendeleza eneo hilo.

Kwa upande wa wawekezaji, Bw. Scott Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji wanataka kuhakikishiwa kuwepo kwa utalii wa kesho. “Hatuwezi kuwa na utalii wa kesho kama hatutunzi mazingira ya sasa,” alisema.
Read More

MAJALIWA AONGOZA KIKAO ,KUHUSU UTATUZI WA MGOGORO WA PORI TENGEFU LA LOLIONDO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (katikati) na Mkurugenzi  wa  Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Manda Ngoitika baada ya kikao kilichowahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na  Kamati Shirikishi ya Jamii kuhusu utatuzi wa Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kilichofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Desemba 6, 2017.
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao  kilichowahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na  Kamati Shirikishi ya Jamii kuhusu utatuzi wa Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kilichofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Desemba 6, 2017.

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao  kilichowahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na  Kamati Shirikishi ya Jamii kuhusu utatuzi wa Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kilichofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Desemba 6, 2017.

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao  kilichowahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na  Kamati Shirikishi ya Jamii kuhusu utatuzi wa Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kilichofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Desemba 6, 2017.

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao  kilichowahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha na  Kamati Shirikishi ya Jamii kuhusu utatuzi wa Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo kilichofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu, mjini Dodoma Desemba 6, 2017.


Read More

MAAGIZO 5 YA WAZIRI MHAGAMA KWA PROGRAMU YA MIVARF KUOGEZA THAMANI YA BIASHARA ZA MIFUGO WILAYANI LONGIDO

Waziri wa Nchi Ofisi  ya Waziri Mkuu  (Sera, Bunge, Ajira ,Kazi,  Vijana na Watu wenye Ulemavu ) Mhe.Jenista Mhagama ameielekezaProgramu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), kuongeza Thamani Biashara za Mifugo wilayani Longido kwa kutatua  kero zote  za wafanyabiashara wa mifugo wilayani humo.

Mhagama ametoa maagizo hayo baada ya kukagua  Soko la kimkakati lililojengwa na Serikali kupitia Ofisi Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF). Soko hilo litawanufaisha wananchi wapatao 14,2000  wa wilayani Longido ambapo asilimia 95 ni wafugaji na wanaojishughulisha na biashara za mifugo.


Soko  hilo la kimkakati ambalo halijafunguliwa rasmi , tayari halmashauri ya wilaya hiyo imeweza kukusanya mapato ya kiasi cha shilingi milioni 106 kwa mwaka  2016/2017 ambapo kwa makusanyo hayo yamewezesha halmashauri hiyo kuvunja rekodi ya miaka kumi iliyopita kwa kukusanya shilingi bilioni 1.3 kwa mara ya kwanza  kwani awali mapato yake yalikuwa chini ya bilioni moja. Aidha umuhimu wa soko hiloumejidhihirisha pale Halmashauri ilivyoweza mwezi Novemba kutoa asilimia 10ya mapato yake kwa wananwake na Vijana ikiwa nikwa asilimia5 kwakilakundi na hii ikiwa nimara ya kwanza kwa Halmashauri hiyo kuweza kutekeleza hilotangu kuanzishwa kwake.





MIVARF;  ni Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini  iliyobuniwa  na serikali ya Tanzania  kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo yaani (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).   Programu hii inatekelezwa  katika mikoa 29 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani  tangu mwaka 2011.
Read More

Wednesday, December 6, 2017

WAZIRI MKUU AKAGUA MAKAZI YA MAKAMU WA RAIS

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Kaimu Meneja wa TBA-Dodoma, Steven Simba (kulia) wakati alipokwenda kukagua ofisi na makazi ya muda ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma Desemba 6, 2017 (kushoto) ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi, na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ukarabati wa makazi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma Desemba 6, 2017. 


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea maelezo ya ujenzi kutoka kwa Msanifu Majengo, Edward Kayombo (kulia) wakati alipoenda kukagua ofisi na makazi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma Desemba 6, 2017 wa pili kulia ni Kaimu Meneja wa TBA-Dodoma, Steven Simba (kushoto) ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi, na wapili kushoto ni Waziri wa Nchi Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa maelezo ya mpangilio wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Msanifu Majengo, Edward Kayombo (kulia) wakati alipokwenda kukagua ofisi hiyo mjini Dodoma Desemba 6, 2017 (katikati) ni Waziri wa Nchi Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan pindi atakapohamia Dodoma.

Waziri Mkuu amefanya ukaguzi huo leo mchana (Jumatano, Desemba 6, 2017) katika eneo la Kilimani, mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Waziri wa Nchi (OWM) anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Wenye Ulemavu na Vijana, Bibi Jenista Mhagama alisema Kikosi kazi cha kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kilibaini kuwa mahali alipokuwa akiishi awali siyo sahihi kwa ajili ya makazi ya kudumu ya Mhe. Makamu wa Rais.

“Pale palikuwa panafaa kwa ajili ya ziara za kikazi alipokuwa akija Dodoma, kwa hiyo tumeamua tufanye ukarabati hapa, ili aweze kuishi kwa viwango vinavyostahili.”

Alisema kazi ya matengenezo kwenye makazi yake itagharimu sh. bilioni 1.5 wakati kazi ya kutenganisha ofisi za watumishi na wasaidizi wa Makamu wa Rais itagharimu sh. milioni 680.

Waziri Mkuu pia alikagua matengenezo ya Ofisi inayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais ambayo itakuwa eneo la Ndejengwa.

Wakati huohuo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Bw. Steven Simba ambaye anasimamia ujenzi huo, alimweleza Waziri Mkuu wanataraji kuwa kazi hiyo itakamilika kabla ya Desemba 30, mwaka huu.


Read More

Tuesday, December 5, 2017

MAJALIWA AREJEA DODOMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary  wakiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Benilith Mahenge wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Desemba 5, 2017. Mheshimiwa Majaliwa amerejea Dodoma  baada ya safari katika mikoa ya Singida, Lindi na Dar es salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa mkoa wa Dodoma wakati alipowasili   kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Desemba 5, 2017, baada ya safari ya Singida, Lindi na Dar es salaam.  Kulia kwake ni mkewe Mary.



Read More

Monday, December 4, 2017

MPANGO WA SHILINGI BILIONI 1 WA KUSAIDIA WATU WENYE ULEMAVU NCHINI WAZINDULIWA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama akifafanua umuhimu wa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye Ulemavu kwa Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jassem Al-Najem, wakati ubalozi huo ulipozindua mpango wa kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini katika Chuo cha Ufundi kwa watu wenye Ulemavu, Yombo jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Novemba, 2017.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi kwa watu wenye Ulemavu, Yombo jijini Dar es Salaam wakipokea sehemu ya vifaa vya kuwasaidia watu wenye ulemavu kutoka  kwa Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jassem Al-Najem, wakati ubalozi huo ulipozindua mpango wa kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini, tarehe 30 Novemba, 2017.

Kama inavyoeleweka kila tarehe 3 Desemba ya kila mwaka jamii ya kimataifa ikiwemo Tanzania huadhimisha siku ya watu wenye ulemavu Duniani. Kwa kutambua hilo serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Kuwait wamezindua Mpango wa kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini.

Mpango huo utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni moja utafadhiliwa na serikali ya Kuwait na utatekelezwa Tanzania Bara na Tanzania visiwani kwa kuyashirikisha mashirika yasiyokuwa ya serikali na asasi za kijamii.

Akiongea wakati wa kuzindua mpango huo leo tarehe 30, Novemba 2017, katika Chuo cha Ufundi Yombo kwa Watu wenye Ulemavu, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alifafanua kuwa serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuboresha ustawi wa watu wenye ulemavu nchini kwa kushirikiana na wadau wote.

“Ninatoa wito kwa Taasisi za serikali na zisizo za serikali kila ziendelee kushirikiana na wizara yangu pale wanapo ona wana nafasi kidogo katika kuwasaidia watu wenye Ulemavu nchini ili waweze kuishi na kuhudumiwa katika shughuli zote ambazo ni haki zao kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu” alisema Mhagama

Mhagama aliishukuru nchi ya Kuwait kwa dhamira yake ya kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini ambapo wamezindua mpango huo kwa kutoa vifaa vya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika Chuo cha Ufundi Yombo kwa Watu wenye Ulemavu.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jassem Al-Najem alifafanua kuwa nchi yake inatambua juhudi za serikali ya awam ya tano katika kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na kwa kulitambua hilo wameamua kuwa na mapango huo ili kutambua mchango wa watu wenye ulemavu.

“Leo nazindua mpango kwa kutoa msaada wa kwanza kwa wanafunzi wenye ulemavu katika kituo hiki kwa kusaidia viti vya maringi, magongo vifaa vya kusaidia watu wenye udhaifu wa kusikia  na miwani na fimbo kwa wasiiona, ni matumaini yangu kuwa mpango huu utakuwa na manufaa kwa wote” alisema Al-Najem.

Awali akiongea katika makabidhiano ya vifaa hivyo Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Yombo kwa Watu wenye Ulemavu, Mariam Chelangwa alieleza kuwa anashukuru kwa kuwa watu wa kwanza wa kunufaika na mpango huo kwa kupata msaada wa vifaa vya kuwasaidia wanafunzi ambavyo vitawasaidia kupata mafunzo bora.


Serikali imeendelea na juhudi za kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki stahiki nchini ambapo tangu mwaka 2004 serikali iliandaa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa watu wenye Ulemavu, pamoja na sheria na. 9 ya mwaka 2010 inaweka msisitizo wa haki za watu wenye ulemavu katika ajira, afya na shughuli za kiuchumi. 
Read More

WABUNGE TUMIENI MICHEZO KUIMARISHA USHIRIKIANO WA EAC-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji wa timu ya Bunge la Burundi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya timu ya Bunge ya Tanzania .Waziri Mkuu alifungua mashindano ya timu hizo mbili  ambayo yamefanyika  kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo Desemba 4, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji wa timu ya Bunge la Tanzania muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi dhidi ya timu ya Bunge ya Burundi. Waziri Mkuu alifungua mashindano ya timu hizo mbili ambayo yamefanyika  kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo Desemba 4, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabunge wanaoshiriki mashindano ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wayatumie kuimarisha ushirikiano.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Desemba 4, 2017) wakati akifungua mechi ya mpira wa miguu iliyozikutanisha timu za Tanzania na Burundi kwenye Uwanja wa Taifa. 

Mashindano hayo ya Nane ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yalifunguliwa jana (Jumapili, Desemba 3, 2017) na Spika wa Bunge Job Ndugai

Waziri Mkuu amesema nchi zote zinashiriki mashindano hayo ni  ndugu hivyo ni vema wakayatumia katika kuimarisha ushirikiano wa Mabunge ya Jumuiya hiyo. 

Pia Waziri Mkuu amewataka wachezaji hao kuhakikisha kucheza mpira mzuri na wazingatie viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). 

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema katika mashindano hayo kila timu inahitaji kupata ushindi, hivyo amewataka wanatumie vizuri ujuzi wao ili waibuke na ushindi.

Katika ufunguzi huo Waziri Mkuu aliambatana na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Akson, Katibu wa Bunge la Tanzania Stephen Kagaigai.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt.  Harrison Mwakyembe.

Katika mashindano hayo timu ya Tanzania imeibuka kidedea baada ya kushinda magoli matatu na Burundi ilipata magoli mawili.


Read More

Saturday, December 2, 2017

MAJALIWA AMFARIJI MOHAMMED CHILAMBO AMBAYE NYUMBA YAKE ILICHOMWA MOTO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwafariji Katibu  wa CCM wa Kata ya Mnacho , Mohammed Chilambo  (kushoto kwake) ambaye nyumba yake imechomwa moto kwa sababu zinazodaiwa kuwa za kisiasa katika kijiji cha Chimbela B wilayani Ruangwa Desemba 2, 2017.




Read More

MARY MAJALIWA: WAZAZI WEKEZENI KWENYE ELIMU YA WATOTO

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewaomba wazazi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wahakikishe wanatumia sehemu ya kipato chao katika kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao.

Amesema elimu ndiyo jambo pekee linaoweza kumsaidia mtoto katika kutimiza ndoto zake za maisha pamoja na kumtoa katika kundi la wategemezi.

Mama Mary aliyasema hayo jana (Jumamosi, Desemba 2, 2017), katika maafali ya shule ya awali na msingi ya Wonder Kids, iliyopo wilayani Ruangwa, Lindi.


Mke wa Waziri Mkuu alialikwa katika maafali hayo kama mdau wa elimu. Maafali hayo yaliyohusisha watoto wa awali ambao wanaingia darasa la kwanza.

“Walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanafunzi hao wanajua kusoma vizuri, hivyo wazazi watumie kipato chao kuwekeza katika elimu kwani faida watakuja kuiona baadaye.”

Alisema kitaaluma yeye ni mwalimu hivyo anatambua kuwa walimu wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanafunzi hao wanajua kusoma vizuri na wanakuwa na tabia nzuri, hivyo wazazi hawana budi kushirikiana nao.

Pia Mama Mary alitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi wawatie moyo walimu kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa. “Wote ni mashahidi watoto wetu tulivyowaleta na sasa ni tofauti.”

Alisema ni vizuri wazazi wakashiriki kikamilifu katika suala la elimu kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya masomo yao badala ya kuwaachia walimu peke yao.

Kwa upande wake ,mgeni rasmi katika maafali hayo ambaye ni Muwakilishi Mkazi wa Children in Crossifire Bw Craig Ferla aliwapongeza wanafunzi hao kwa  kutimiza moja ya hatua katika safari yao ya elimu na aliwasihi waendele kupenda kwenda shule na kusoma kwa bidii.

Pia aliwapongeza wazazi kwa kutambua umuhimu wa elimu ya awali na kuwapeleka watoto wao kwenye shule hiyo ya Wonder Kids. “Wonder Kids ni mahali sahihi ambapo mtoto anapata  elimu na malezi bora.

Alisema elimu ya awali ninzuri kwa mtoto kwa kuwa inawawezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, hivyo aliwaeleza Wanaruangwa kutumia vizuri fursa ya uwepo wa shule  hiyo katika wilaya yao.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bibi Nancy Tausi alisema  Wonder Kid ilianzishwa Januari, 2017 ikiwa na wanafunzi 117 ambao ni wa kuanzia darasa la awali hadi darasa la tatu.


Alisema lengo la kuanzisha shule hiyo ni kuhakikisha watoto wanapata kujua kusoma vizuri na kwamba wanatarajia kuanzisha darasa la kompyuta kwa ajili ya watoto kujifunza TEHAMA pamoja na kuanza kufundisha lugha ya Kifaransa.
Read More

MAMA MARY MAJALIWA ASHIRIKI MAHAFALI YA SHULE YA AWALI NA MSINGI YA WONDER KIDS MJINI RUANGWA

Watoto wa Shule ya Msingi na Awali ya Wonder Kids wakiimba wimbo wa Shule yao katika Mahafali ya Kwanza ya Shule hiyo iliyopo Ruangwa Mjini Desemba 2, 2017. 

Wahitimu wa  darasa la Awali wa Shule ya Wonder Kids  wakiimba  katika Mahafali ya Kwanza ya Shulel hiyo iliyopo Ruangwa Mjini Desemba 2, 2017.

 Wahitimu wa  wa Shule ya Msingi na Awali ya Wonder Kids wakicheza ngoma ya asili  katika Mahafali ya Kwanza ya Shulel hiyo iliyopo Ruangwa Mjini Desemba 2, 2017.

 Mgeni Rasmi katika Mahafali ya kwanza ya Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya mjini Ruangwa , Bw. Craig Ferla ambaye pia ni Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Children in Crossfire akimkabidhi cheti  kwa mhitimu wa Mafunzo ya Awali katika shule hiyo, Jasmine Madamba, Desemba 2, 2017.Wapili kuil ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa.

Baadhi ya wazazi na waalikwa wa Mahafali ya Kwanza ya Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya Mjini Ruangwa wakimsikiliza Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa wakati alipozungumza katika Mahafali hayo Desemba 2, 2017.

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akizungumza katika mahafali ya kwanza ya Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya Mini Ruangwa, Desemba 2, 2017. 

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akizungumza na watoto wakati alipotembelea bwalo la chakula la Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya mjini Ruangwa katika mahafali ya shule hiyo, Desemba 2, 2017.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akizungumza na watoto wakati alipotembelea Bwalo la chakula la Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya mjini Ruangwa katika mahafali ya shule hiyo, Desemba 2, 2017.Kulia kwake ni binti yake, Zuleikha Kassim Majaliwa. 

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akizungumza na watoto wakati alipotembelea Bwalo la chakula la Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids ya mjini Ruangwa katika mahafali ya shule hiyo, Desemba 2, 2017.Kulia kwake ni binti yake, Zuleikha Kassim Majaliwa. 

Read More

Friday, December 1, 2017

BALOZI SEIF: WAISLAM IMARISHENI UADILIFU

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amewataka Waislam nchini kote kuwa waadilifu kama alivyokuwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Amesema ni vema wakatumia wakati huu wa Maulid kutathmini mienendo ya maisha yao kwa kujiuliza kama maisha wanayoishi  yanafanana na yale aliyoishi Mtume Muhammad.

Balozi Seif ameyasema hayo leo (Ijumaa, Desemba Mosi, 2017) alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi.

“Kuna vigezo vingi mja anaweza kuvitumia wakati anapojitathmini, ambavyo ni pamoja na tabia ya Bw Mtume ya uadilifu na  wake. Tujiulize kati yetu hapa ni wangapi waadilifu na waaminifu kama alivyokuwa Bw. Mtume.”

Amesema kupungua kwa uaminifu na uadilifu ndiko kulikomfanya Rais Dkt. John Magufuli mara baada ya kuingia madarakani kuanzisha vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, hivyo wanatakiwa kumuunga mkono.


Balozi Seif amesema Waislam waka kila sababu ya kushirikiana na Rais Dkt. Magufuli katika mapambano hayo kwa sababu kupinga vitendo vya rushwa na ufisadi ni ibada kwao.

“Mtume (S.A.W) aliikemea sana rushwa na akasema kuwa amelaaniwa na Mwenyezi Mungu mwenye kutoa na kupokea rushwa na hata Yule mpiga debe. Pia tunaamini kuwa dini zote duniani zinapinga rushwa, hivyo tuiiepuke”

Pia amewaomba viongozi wa dini zote nchini waendelee kushirikiana na Seikali kwa kuhubiri  amani, utulivu na mshikamano ili kujenga umoja kwa Watanzania wote. “Siku zote mmekuwa mkitusaidia sana kupitia mahubiri yenu kwa kujenga umoja kwa Watanzania wote bila ya kujali dini zao,rangi wala kabila. Nawaomba muendelee na moyo huo.”

Awali, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Bin Zubeiry alisema aliwaasa Watanzania wote waendelee kuidumisha na kuitunza amani kwa sababu hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana bila ya kuwepo kwa amani.

Alisema suala la kudumisha amani, kuheshimiana na kushirikiana miongoni mwa waislamu na wasiokuwa waislam limehimizwa sana katika dini ya kiislam na dini nyingine, hivyo wananchi hawana budi kuendeleza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza Sheikh Mkuu kwa uongozi wake mzuri wa  Baraza la WaislamTanzani (BAKWATA) ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na dini zote bila Ubaguzi.

Alisem serikali itaendelea kufanya kazi na dini zote na kwamba Rais Dkt. Magufuli amezipa kipaumbele shughuli za dini zote ziendelee kufanyika nchini.

Baraza hilo lilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Zubeiry, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya.

 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Maji Bw. Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Nishati Bibi Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri, Bibi Stellah Ikupa Alex, Naibu Waziri wa Madini Bw. Stansilaus Nyongo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bibi Maimuna Tarishi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania, Bibi Shamim Khan, Mkunge wa Kibiti Bw. Ally Ungando, Mbunge wa Liwale Bw. Zubeiry Kuchauka, Mbunge wa Nachingwea Bw. Hassan Masalla, Mbunge wa Lindi Mjini, Hassan Kaunje Mbunge wa Viti Maalumu Bibi Hamida Abdallah.

Wengine ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Bruno Ngonyani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Alhikma, Kiongozi Mkuu wa Kiroho wa Dhehebu la Shia Ithnasheri, masheikh wa mikoa yote pamoja na wananchi wa Lindi pamoja na mikoa mbalimbali nchini.
Read More

BALOZI SEIF IDDI MGENI RASMI BARAZA LA MAULIDI RUANGWA

Baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipohutubia   kwenye uwanja wa  Shule ya Msingi ya  Likangala wilayani   Ruangwa Desemba 1, 2017.

 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya (wapili kushoto) na kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake Waislaam, Shamim Khan wakati alipowasili kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala kushiriki katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad  (S. A.W). Mgeni Rasmi kaaika Baraza hilo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kuingia kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi  ya Mtume Muhammad (S.A.W),Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali  Iddi kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani RUangwa Desemba 1, 2017.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Baraza la Maulidi ya  Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Rungwa Desemba 1, 2017. Mgeni Rasmi katika Maulidi hayo alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.


Baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipohutubia   kwenye uwanja wa  Shule ya Msingi ya  Likangala wilayani   Ruangwa Desemba 1, 2017.

Askofu Mkuu, Bruno Ngonyani wa Jimbo Katoliki la Lindi akizungumza katika  Baraza la Maulidi ya Mtume Muhammad  (S.A.W) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani Ruangwa, Desemba 1, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mgeni Rasmi katika Baraza la Maulidi  ya Mtume Muhammad (S.A.W),Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali  Iddi  kwenye  uwanja wa Shule ya Msingi ya Likangala wilayani RUangwa Desemba 1, 2017. Kushoto ni Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubacary Zubeiry Ally.

Read More