Sunday, January 7, 2018

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA KUPOZEA UMEME NJIA YA MAKAMBAKO - SONGEA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea na kuahidi kuwa Serikali itaendelelea kuwasambazia umeme wananchi wote.

Ametoa ahadi hiyo leo (Jumapili, Januari 7, 2018) wakati Akizungumza na wananchi wa eneo la Unangwa nje kidogo ya mji wa Songea, mara bada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.

Waziri Mkuu amesema ujenzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Joseph Magufuli ya kuwataka Watanzania wapate umeme kwa urahisi. “Mheshimiwa Rais ameshusha gharama za umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000. Zamani ulikuwa unalipia fomu za kuomba umeme, sasa hivi nazo amesema zitolewe bure. Nguzo za umeme zilikuwa zinatozwa sh. 150,000, sasa hivi amesema zitolewe bure,” alisema.

Waziri Mkuu amesema zamani mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma, Songwe, Mtwara na Lindi ilikuwa na matatizo sufu ya kupata umeme lakini hivi sasa mikoa ya Mbeya na Iringa imepata suluhisho baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa kilovoti 400 wa kutoka Iringa hadi Shinyanga.

“Sasa hivi tunaingia Njombe na Ruvuma na baadaye tutaenda Mtwara na Lindi,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wanaoishi jirani na mahali kituo hicho kinapojengwa, wawe walinzi wakuu wa mali za mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika mapema. “Eneo hili lina saruji, nyanya na nondo, si vema watu wachache wjiokeze na kuiba vifaa vya ujenzi. Saidieni kulinda eneo hili, na mali za mkandarasi ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisisitiza.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema mradi huo utakapokamilika utaunganisha vijiji 120 na wateja 22,700.


Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za TANESCO mjini Songea ambalo litagharimu sh. bilioni 2.27. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2018.

Akimkaribisha kuzungumza na watumishi wa TANESCO na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri wa Madini, Dk. Medard Kalemani alisema jengo hilo ni moja ya majengo makubwa saba nchini ambayo yatakuwa makao makuu ya kimkoa ya TANESCO.

Majengo mengine yatajengwa kwenye mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Mtwara, Njombe, Pwani, Geita na Kigoma. “Kukamilika kwa ofisi hizi haimaanishi wafanyakazi wakae ofisini na kufaidi viyoyozi. Ni lazima waende nje kuwafuata wateja,” alisisitiza.

Dk. Kalemani alisema chini ya mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Serikali imeamua kujenga vituo vya kupozea umeme huko Makambako, Madaba na Songea ambavyo vitakamilika Agosti 30, 2018.

“Kukamilika kwa mradi huo kutaiepusha TANESCO na mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi kununua mafuta mazito ambao pia utapunguza gharama za umeme kwa watumiaji. Kabla ya hapa, TANESCO ilikuwa inatumia sh. milioni 900 kwa siku kugharimia mafuta hayo,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema ujenzi wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 78, unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 31, mwaka huu.

“Gharama za ujenzi kwa jengo zima ni sh. bilioni 2.198 na gharama za mshauri ni sh. milioni 78 na gharama zote zinafikia sh. bilioni 2.276. Fedha hizi zimetolewa na Serikali,” alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, wakati alipowasili kwenye Mradi wa ujenzi wa Kituo cha kupoozea umeme, eneo la Unanga, katika Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Joyce Mndeme na kulia ni Meneja Mradi Didas Lyamuya. Januari 7, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi katika Mradi wa Kituo cha kupoozea umeme, eneo la Unanga, katika Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Januari 7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe, wakati akizindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tanesco Mkoa wa Ruvuma, lililopo katika Wilaya ya Songea Mjini, Mkoani Ruvuma. Januari 7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na wananchi, baada ya akizindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tanesco Mkoa wa Ruvuma, lililopo katika Wilaya ya Songea Mjini, Mkoani Ruvuma. Januari 7, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na wananchi, baada ya akizindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tanesco Mkoa wa Ruvuma, lililopo katika Wilaya ya Songea Mjini, Mkoani Ruvuma. Januari 7, 2018. 

Read More

Saturday, January 6, 2018

WAZIRI MKUU AWAONYA DC NA DED NYASA

*Asema waache kuwavuruga watumishi, madiwani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Bi. Isabella Chilumba na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Oscar Mbyuzi waache malumbano ambayo yanawavuruga watendaji walio chini yao.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 6, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Amesema katika ziara zake zote za mikoani, amekuwa akipata malalamiko mengi kwenye Halmashauri na mabaraza ya madiwani lakini katika wilaya ya Nyasa amekuta hali ni shwari  isipokuwa kuna migogoro midogo kwenye uongozi wa juu.

“Tatizo ni dogo huku juu, bado mnavurugana Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi. Ninyi ni viongozi wa juu, acheni kuvurugana, fanyeni kazi. Mkigombana wanaoumia ni wananchi,” alisema.

“Mkuu wa Wilaya anaweza kuingia kwenye kikao chochote cha Halmashauri na kudai apewe taarifa, mpeni. Yeye siyo mjumbe wa kikao hicho lakini anayo mamlaka ya kushiriki.”

“Mkurugenzi wewe ni mtendaji mkuu, tumekukabidhi watumishi uwaongoze. Tumekukabidhi fedha kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hii. Mtu akizitamani, mwambie hizi fedha zina maelekezo rasmi, hazipaswi kwenda kokote,” alisisitiza.

Aliwataka madiwani wasijenge tabia ya kuongeza siku za vikao kwa makusudi ili tu wapate posho za ziada. “Msitengeneze siku za ziada na kumpa presha Mkurugenzi. Kama kikao ni cha siku moja, basi kiishe. Siyo kulaza ajenda ili mmalizie kesho yake. Mkurugenzi akiwanyima fedha, msianze kugombana naye kwa sababu yeye hana fedha za kumgawia mtu,” alisisitiza.

Read More

WAZIRI MKUU AENDELEA NA ZIARA MKOA WA RUVUMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Nyasa, katika Hoteli ya Mt. Vicent iliyopo Mbambabay, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Nyasa, katika Hoteli ya Mt. Vicent iliyopo Mbambabay, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyasa, eneo la Kilosa Bambabay katika Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati akifungua Bwalo la Chakula katika Shule ya Sekondari Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia ngoma ya mganda,katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi, kutoka kwa Bibi Cecilia Manyai, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, Januari 6, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi, kutoka kwa Mzee Gidion Ndembeka, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, Januari 6, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya ungo, kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, Januari 6, 2018.


Read More

WAZIRI MKUU AAGIZA VIONGOZI NCHINI WATOE TAARIFA YA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO



                      *Ni kuanzia Mawaziri hadi Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri wote, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wakurugenzi watoe taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 6, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

“Kuanzia sasa ninaagiza, viongozi wote wa ngazi za juu wakiwemo Mawaziri hadi Wakurugenzi na hata ninyi wakuu wa idara mnawajibika kutoa taarifa za fedha tunazopeleka kwenye miradi kwa sababu wananchi wana haki ya kujua utekelezaji wa ahadi za Serikali,” alisema.

Alisema kila wanapoenda kwenye ziara ya kikazi vijijini, waelezee thamani za kazi zilizofanyika na waeleze ni lini miradi hiyo itakamilika.

“Mnapopata fursa ya kupanda jukwaani, tumieni wasaa huo kueleza kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali. Elezeni Serikali imeleta fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani na kwa kufanya hivyo, mtasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni,” alisema.

Alisema wananchi wana haki ya kupatiwa taarifa za utendaji wa Serikali yao na akawataka viongozi hao wasisubiri ziara za viongozi wa kitaifa. “Nendeni mkaongee na wananchi, msiwaachie Wakuu wa Wilaya au Wabunge peke yao ndiyo waseme na wananchi,” alisema.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kukagua kituo cha kufua umeme kilichopo Unangwa, kuweka jiwe la msingi la ofisi ya TANESCO, kuzungumza na wananchi na kisha kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Songea.

Read More

Friday, January 5, 2018

WAZIRI MKUU AKIWA ZIARANI MKOA WA RUVUMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia mche wa Kahawa, wakati alipotembelea kituo cha utafifti wa zao la kahawa (TACRI) kilichopo kwenye kijiji cha Ugano Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Ruvuma, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dkt. Deusdedit Kilambo. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia sampuli za kahawa kwenye, wakati alipotembelea kiwanda cha kahawa cha Mbinga Coffee kilichopo Mbinga Mjini Wilayani Songea, Mkoani Ruvuma, kulia ni Meneja Uzalishaji Rabiel. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia kahawa kwenye mashine ya kusagia kahawa, wakati alipotembelea kiwanda cha kahawa cha Mbinga Coffee kilichopo Mbinga Mjini Wilayani Songea, Mkoani Ruvuma, kushoto ni Meneja Uzalishaji Rabiel Ulomi na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme. Januari 5, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya Mbinga, Mkoani Ruvuma, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Ruvuma. Januari 5, 2018. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya Mbinga, Mkoani Ruvuma, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tano Mkoani Ruvuma. Januari 5, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia mkono wananchi wa Mbinga Mjini, wakati akiwasili kwenye mkutano wa hadhara aliyouitisha kwenye Uwanja wa Michezo Mbinga Mjini Wilayani Songea, Mkoani Ruvuma. Januari 5, 2018. 

Read More

WAZIRI MKUU AAGIZA MAAFISA KILIMO WASAMBAZWE

*Ataka takwimu za kahawa ziwe tayari ifikapo Feb. 28

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mji na Wilaya za Mbinga wahakikishe kuwa wanaunda kanda za kilimo na kuwasambaza maafisa kilimo wao badala ya kuwaacha wakae maofisini.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Januari 5, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mbinga, kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Mbinga.

“Mkurugenzi wa TC na DC chuja maafisa kilimo ulionao na uhakikishe wanabakia watatu tu. Abaki DALDO, mtu wa horticulture na mthamini, wengine wote wasambaze kwenye kanda ili wasimamie wakulima wakiwa huko huko. Hili litekelezwe na Mkuu wa Wilaya ulisimamie” alisema.

Aliwataka maafisa kilimo wa zao la kahawa waende vijijini na kufanya sensa ili waweze kubaini wana wakulima wangapi wanaozalisha kahawa. “Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue kijiji kina wakulima wangapi wa kahawa, na wana ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana miche mingapi? Hii itaisaidia Serikali ijue inahitaji dawa za aina gani, mbolea kiasi gani na miche mingapi kwa wakulima wake,” alisema.

“Ninataka hizi takwimu ziwe zimekamilika ifikapo tarehe 28 Februari, mwaka huu,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka maafisa ushirika wa wilaya hiyo wakasimamie uundwaji wa AMCOS mpya na kuimarisha zile za zamani ambazo zinafanya kazi vizuri.

“Maafisa ushirika ninataka nipate takwimu ya AMCOS very strong (ambazo ziko imara) kwenye wilaya yako. Iifikapo tarehe 28 Febriari, takwimu hizi ziwe zimekamilika. Kama kuna AMCOS nzuri ziimarisheni, itisha uchaguzi ili uanze na uongozi mpya,” alisisitiza.

Aliwaeleza watumishi na madiwani kwamba Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kurudisha heshima ya zao hilo ambapo zamani iliweza kusomesha watoto kadhaa kwenda sekondari kutokana na mfuko wa kahawa.


“Zamani zao la kahawa lilikuwa likisomesha watoto wa wakulima, sasa hivi hakuna hata anayefaidika na zao hili. Tunataka zao hili liwanufainishe wakulima, iinue uchumi wa wanaMbinga, isomeshe watoto na iwezeshe wakulima kujenga majumba,” alisema.

Alisema kuanzia msimu ujao wa Mei, Juni na Julai 2018, ununuzi wa kahawa utafanywa na vyama vya msingi vinavyotambulika kwa maafisa ushirika.

Aliwaonya watumishi wa Halmashauri hizo waache kutoa vibali vya ununuzi wa kahawa kwa watu binafsi wanaomiliki kampuni za kununua kahawa. “Halmashauri ndiyo mnatoa vibali vya kampuni kununua kahawa. Huu ni mwisho sasa. Hatuna mnunuzi binafsi wala hatuna kampuni binafsi, hawa wote tukutane kwenye mnada,” alisema.

Alisema hataki kuona watumishi wa Halmashauri wakionesha vibali vya kununua kahawa kama moja ya chanzo cha mapato kwenye Halmashauri hizo. “Ni marufuku kuingiza vibali kwenye mapato ya Halmashauri,” alisema.



Read More

WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA MIAKA MIWILI


*Ni wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
*Asema hataki kusikia wakijenga karibu na chanzo cha maji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambao umedumu kwa miaka miwili.

Ametoa uamuzi huo jana jioni (Ijumaa, Januari 5, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mbinga, kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Mbinga.

“Ninazo taarifa kuwa kuwa mnagombea mahali pa kujenga makao makuu ya Halmashauri hadi mnataka kujenga kwenye chanzo cha maji. Hiyo haikubaliki. Kwenye vyanzo vya maji hakujengwi miji, tena Afisa Maliasili nenda ukapande miti zaidi ili tutunze chanzo chetu,” alisema na kuamsha shange ukumbini.

Wataalamu wa Halmashauri hiyo walikuwa wakivutana na Madiwani juu ya makao makuu hayo kujengwa Ndengu (ambako ni karibu na chanzo cha maji) huku wengine wakitaka yajengwe Kigonsera kwa madai kuwa kote ni karibu na wananchi.

Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga iligawanywa Julai 2015 kwa kupata Halmashauri ya Mji wa Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na ilianza kazi Julai 2016.

Waziri Mkuu alisema Halmashauri hiyo si ya kwanza kuwa na migogoro, kwa hiyo nimeamua mjenge hapa hapa mjini Mbinga. Mkijenga huko wanakotaka hawa mtagombana na mkijenga kule nako pia mtagombana, lakini ugomvi wenu ni kwa faida ya nani? Kama si kuwaumiza wananchi mnaowaongoza ni nini?,” alihoji Waziri Mkuu.

“Miaka yote mmekuwa mkipata huduma kutokea hapa hapa kabla Halmashauri hizi hazijatenganishwa. Tumeleta fedha mara mbili, mara ya kwanza sh. milioni 500 na ya pili sh. milioni 400 lakini hazijatumika kwa sababu ya migogoro yenu isiyo na tija. Kwa hiyo, makau makuu yatajengwa hapa hapa mjini,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema kesi kama hizo zilishatokea Musoma Mjini na Vijijini, Lindi Mjini na Vijijini, Kigoma Mjini na Vijijini, na Singida Mjini na Vijijini ambako kote huko Halmashauri za Wilaya za Vijijini zimejengwa mjini na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma kama kawaida.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Naibu Waziri (OR-TAMISEMI), Bw. Joseph Kakunda afuatilie suala la sh. milioni 700 ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya mradi wa maji lakini Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imezitoa kwa kampuni ambayo haina hadhi ya kupokea kiasi hicho cha fedha.

“Tumeleta kwa ajili ya mradi wa maji lakini ninyi mkaipa kazi kampuni ambayo haina hata uwezo wa kupokea sh. milioni 500. Ninazo taarifa kuwa Halmashauri hii mmeshalipa asilimia 80 ya fedha kwa mkandarasi huyo na wala maji hayajatoka hadi leo. Naibu Waziri fuatilia na nipate taarifa,”alisema.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Nyasa ambako atazungumza na watumishi na madiwani, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, atakuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la utalii na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.

Read More

WAZIRI MKUU AKIWA ZIARANI MKOA WA RUVUMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Molam Tanzania Limited, Medappa Mg, wakati alipotembelea Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa ufafanuzi wa miche ya Kahawa,  na mkulima wa zao hilo, Bi ….wakati akikagua kitalu cha miche ya kahawa katika Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi miche ya Kahawa, Mkulima wa zao hilo, Remigius Njovu,inayotolewa bure na Kampuni ya Molam Tanzania Limited, kwa wakulima wa zao la Kahawa, baada ya kukagua kitalu cha miche ya kahawa katika Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Molam Tanzania Limited, Medappa Mg, wakati akikagua kitalu cha miche ya Kahawa katika Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akioneshwa mashine ya kukoboa Kahawa na Meneja wa Shamba la Kampuni ya Molam Tanzania Limited, Hamza Kassim, wakati alipotembelea Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia Wananchi­­, wakati alipotembelea Shamba la Kahawa la AVIV lililopo kwenye kijiji cha Lipokela Wilaya ya Songea, Mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu yupo Mkoani Ruvuma  kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Januari 5, 2018.

Read More

WAZIRI MKUU AKEMEA MADUDU USHIRIKA MBINGA

*Aagiza uchunguzi ufanyike kuanzia leo, maafisa wa MBICU, MBIFACU kikaangoni
*Apiga marufuku ununuzi wa kahawa kwa mfumo wa MAGOMA
*Aitisha kikao cha wadau wa kahawa Dodoma Jan. 14

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amebaini madudu kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika vya Mbinga (MBICU na MBIFACU) na kuagiza uchunguzi ufanyike kuanzia leo.

“Nikiondoka hapa jukwaani, viongozi wote wa zamani na wa sasa waripoti kwa Mkuu wa Wilaya, na OCD hakikisha ofisi za chama hazifunguliwi hadi kesho asubuhi (leo) kazi itakapoanza, ili wasije kubadilisha nyaraka kwenye ofisi yao. Timu yangu ya uchunguzi iko hapa Mbinga, kesho waende wote kwenye ofisi hizo,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Januari 5, 2018) wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Mbinga, kwenye viwanja vya CCM, mjini Mbinga.

“Natambua kuwa MBICU ilishakufa ikiwa na madeni makubwa na mkaunda tena MBIFACU, ambayo nayo inasuasua, lakini viongozi wote hawa watafutwe, waje waonane wa timu  yangu na waeleze fedha za chama zimeenda wapi na kama walizikopea zilifanya nini,” alisisitiza.

Alisema timu hiyo ya uchunguzi itakiangalia chama hicho na kukifumua chote, na wote wakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kinidhamu. “Tunataka MBICU na madeni yenu yaliyoko kwa Msajili wa HAZINA yajulikane, tunataka turudishe hoteli yetu, mashamba yetu na majengo yetu,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imeamua kuboresha ufanisi katika mazao matano ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaliingizia Taifa fedha za kigeni.

“Mazao haya tutayasimamia kuanzia kilimo hadi uvunaji na utafutaji wa masoko. Nimeshafuatilia mazao ya korosho, tumbaku na pamba. Na sasa nimeanza na zao la kahawa na nimeamua kuanzia huku Mbinga,” alisema.

Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha zao la kahawa katika mikoa yote inayolima zao ikiwemo Ruvuma, Mbeya, Kagera, Kigoma na maeneo mengine.

“Na nikimaliza ziara hii, nimeitisha kikao cha wadau wa zao la kahawa mjini Dodoma ifikapo Januari 14, 2018. Nimewaita Wakuu wa Mikoa, wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa ushirika, Maafisa kilimo na wadau wote kutoka mikoa yote inayolima kahawa hapa nchini, tukutane na kupeana maelekezo juu ya usimamizi wa zao hili,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kwamba kuanzia msimu ujao, zao la kahawa litauzwa kwa mnada chini ya mfumo wa ushirika. “Kuanzia msimu ujao, kahwa yote utauzwa kwa mnada, mnunuzi yeyote akitaka kununua kahawa aende kwenye mnada, tukikukuta mtu ananua kahawa kwa mkulima tutamkamata,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.

Alisema kuna watu wamekuwa wanapita na kununua kahawa kwa mfumo wa ‘magoma’ ambapo huwalaghai wakulima kwa kuwapa noti chache za sh. 10,000. “Huu mfumo wa magoma ni wa kuwaibia wananchi, hatutaki tena kuuona. Hakuna tena magoma hapa Mbinga,” alisisitiza.

“Bei ya mnada ndiyo fedha ya mkulima na sasa, Serikali tumeondoa tozo 17 kwenye zao hili kwa sababu tunataka tuone mkulima afaidike na zao hili,” alisema.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Nyasa ambako atazungumza na watumishi na madiwani, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, atakuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la utalii na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.

Read More

WAZIRI MKUU AHIMIZA KILIMO CHA KAHAWA

*Asisitiza kahawa iuzwe kwa mfumo wa ushirika

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wajikite kwenye zao la kahawa ili wawe na zao mbadala la biashara.

Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lipokela na vijiji jirani, wilayani Songea mara baada ya kukagua shamba la kahawa la Aviv Tanzania lenye ukubwa wa hekta 1,990.

“Limeni kahawa ili mpate fedha sababu zao hili ni la biashara. Kahawa ni miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo Serikali ya awamu ya tano imeamua kuyawekea mkazo ili yaweze kuongeza tija kwa wakulima na kuinua uchumi wa Taifa”.

“Tumeamua kuweka mkazo kwenye mazao matano ya pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaleta tija na kuliingizia Taifa fedha za kigeni,” alisema na kuongeza:

“Tumefanya tathmini na tumegundua udhaifu mkubwa mkubwa katika usimamizi wa mazao haya ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Halmashauri.”

Waziri Mkuu alisema ni lazima wananchi walime zao hilo na viongozi wahakikishe wananchi wananufaika za zao hilo. Hata hivyo, alionyeshwa kutoridhishwa na utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea baada ya kuelezwa kuwa kampuni ya Aviv Tanzania imezalisha miche milioni moja lakini iliyochukuliwa na kusambazwa kwa wananchi ni miche isiyozidi 200,000.

“Kampuni hii imeamua kutoa miche ya bure kwa wakulima, wamezalisha miche milioni moja lakini hadi sasa imechukuliwa 200,000 tu. Kuna miche zaidi ya 800,000, imebaki, na tena wawekezaji hawa wanatoa elimu bure ya kulima na kuitunza mikahawa yako,” alisema.

Amewataka wakulima hao watenge ekari moja hadi tatu kwa kila kaya ili waweze kulima zao hilo. “Wana Lipokela tengeni ekari moja hadi tatu za kulima kahawa, tukifanya hivyo suala la fedha kupitia kahawa litakuwa limekamilika,” alisema.

Amesema itabidi zao la kahawa liundiwe mfumo maalum wa ununuzi ambao ni wa ushirika kwa kuzingatia vyama vya msingi (AMCOS) vilivyokuwepo.
Mapema, akitoa taarifa juu ya shamba hilo, Meneja wa Aviv Tanzania, Bw. Medu Medappa alisema lengo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ni kuhakikisha wanapata shamba kubwa la kahawa aina ya Arabica nchini Tanzania lenye viwango vya kimataifa.

Alisema wamekwishatoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,000 zikiwemo za moja kwa moja na za msimu.

Alisema kampuni hiyo imeweza kuchangia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vinne jirani vya Lipokela, Lusonga, Liganga na Selekano. “Hadi mwaka 2017 tuliweza kukamilisha ujenzi wa zahanatio katika kijiji cha Lipokela, nyumba ya mwalimu katika vijiji vya Liganga na Lusonga, uchangiaji wa madawati kwenye vijiji vya Lipokela na Lusonga,” alisema.

Alisema wameweza kuanzisha scheme ya wakulima wadogo wa nje (outgrowers scheme) kwa wakulima 2,000 ambao wamegawanyika kwenye vikundi 36 katika vijiji 31 ndani ya mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Mbinga ambako atakagua miche kwenye taasisi ya TACRI, atatembelea kiwamda cha kukoboa kahawa cha Mbinga (MCCCO), kuzungumza na watumishi na madiwani na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.
Read More

Thursday, January 4, 2018

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU ATEMBELEA OFISI YA RAIS TAMISEMI KUONA MIFUMO YA TEHAMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Miundombinu ya TEHAMA Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Baltazari Kibola wakati wa warshaa kuhusu Mifumo ya TEHAMA na Takwimu inavyotegemeana Kiutendaji yaliyofanyika Tarehe 04 Januari, 2018 Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Mohamed Pawaga akizungumza jambo alipotembelewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora katika ofisi yake Mjini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora akitoa ufafanuzi wa masuala ya mifumo ya TEHAMA wakati wa Warsha iliyolenga juu ya Mifumo ya TEHAMA na Takwimu inavyotegemeana Kiutendaji yaliyofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa TAMISEMI Dodoma .

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Obey Assery akichangia hoja wakati wa warsha fupi kuhusu Mifumo ya TEHAMA na Takwimu inavyotegemeana Kiutendaji iliyoandaliwa na TAMISEMI Januari 4, 2018 Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Mohamed Pawaga akieleza umuhimu wa matumizi ya Mifumo ya TEHAMA na Takwimu kwa wajumbe wa warsha iliyoandaliwa na Ofisi hiyo Dodoma.
Daktari Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Boniface Nguhuni akijibu hoja wakati wa Warsha ya Masuala ya Mifumo ya TEHAMA iliyoandaliwa na ofisi hiyo Januari 04, 2018 Dodoma.

Read More

Tuesday, January 2, 2018

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU ATEMBELEA NYUMBA ZA TBA DODOMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Obey Assery wakati alipotembelea Mradi wa Nyumba za Kikuyu Flats zinazosimamiwa na  Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Dodoma Januari 2, 2018.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Obey Assery wakiangalia baadhi ya majengo yanayokarabatiwa kwa ajili ya Watumishi wa Serikali watakao hamia Dodoma  alipotembelea Kukagua ukarabati huo Januari 02, 2018.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Idara ya  Uratibu wa Shughuli za Serikali wa Ofisi hiyo Bw. Obey Assery kuhusu ukarabati wa nyumba za Kikuyu Dodoma alipotembelea kuangalia ukarabati wa nyumba hizo Januari 02, 2018.

Muonekano wa moja ya jengo lililokarabatiwa chini ya Usimamizi wa Wakala wa Majengo (TBA) lililopo eneo la Kikuyu Flats Dodoma

Read More