Saturday, March 9, 2019

AGA KHAN FANYENI MAPITIO YA GHARALAMA ZENU-MAJALIWA


SERIKALI imeutaka Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), ufanye mapitio ya gharama za afya katika hospitali ya Aga Khan ili wananchi wa kawaida waweze kumudu na kunufaika na huduma za tiba wanazozitoa.

Imeelezwa kuwa pamoja na jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya, pia inatambua mchango unaotolewa na taasisi zisizo za Kiserikali ikiwemo Hospitali ya Aga Khan katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisasa.

Hayo yamesemwa leo (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Amesema upanuzi wa hospitali hiyo ni miongoni mwa jitihada za kuwafikishia Watanzania huduma za afya katika maeneo yao na kwa ngazi zote na kwa gharama nafuu, hivyo amewataka watoa huduma wote nchini waangalie upya gharama zinazotozwa katika huduma mbalimbali hususan za matibabu. 

“Mtakubaliana nami kuwa gharama zikiwa kubwa hazitawanufaisha wananchi hususan wa kipato cha chini na wananchi hawataona unafuu wa kutibiwa nchini na nje ya nchi, hivyo fanyeni mapitio ya gharama hizo.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua gharama kubwa za uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za afya nchini hususan kwa sekta binafsi. “Lengo la Serikali kutoa misamaha ya kodi kwa baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali kama Aga Khan ni kuwezesha huduma zinazotolewa kuwa nafuu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mwitikio wa ni mkubwa na lengo lake ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya matibabu tena kwa uhakika. 

“Nitoe wito kwa taasisi zote zisizo za Serikali kuunga mkono jitihada hizi za Serikali na kuhakikisha wananchi wote wananufaika na huduma zenu kupitia mfumo huu bila kubaguliwa.”

Pia ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakamilishe majadiliano yao katika matumizi ya NHIF kwenye hospitali hiyo ya rufaa. “Dr. Konga Mkurugenzi Mkuu wa NHIF upo hapa kamilisheni mjadala.” 

Amesema nia ya Serikali ni kuona wananchi wanakwenda hapo kwenye jengo hilo zuri na wanapata huduma kupitia bima ya afya. “Ni matumaini yangu kwamba jambo hili litafanyiwa kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya pande zote mbili.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji, kuimarisha amani na utulivu, ambapo ametoa rai kwa sekta binafsi ziendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo nchini kwa kuzingatia sheria za nchi, utamaduni na mila za Watanzania. 

Awali, Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameupongeza Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan kwa upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwani unakwenda kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya kutolea huduma za afya ambapo kwa sasa imeanzisha ushirikiano na sekta ya umma na binafsi kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza. 

NayeBalozi wa Ufaransa nchini, Balozi Frederic Claiver amesema awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya Tanzania.

Pia Balozi huyo amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inatimiza mkakati wake wa kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.


(mwisho)
Read More

AGHA KHAN BADILISHENI SKELI YA MISHAHARA-MAJALIWA

*Asema lengo ni kuondoa manung’uniko kwa watumishi wa taaluma moja

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan uandae skeli ya mishahara inayofanana kwa watumishi wenye taaluma zinazofafana ili kuondoa manung’uniko baina ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Ameyasema hayo kutokana na malalamiko ya watumishi wa taasisi hiyo ambao wanadai kuwepo kwa tofauti ya mishahara kwa watumishi licha ya kuwa na taaluma moja na kufanyakazi kwenye kituo kimoja.

Hayo yalisemwa jana (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Waziri Mkuu alisema suala la maslahi kwa watumishi ni muhimu na linatiliwa mkazo na serikali hivyo uongozi wa Hospitali ya Aga Khan fanyeni mapitio ya mishahara hasa kwa watu walio katika taaluma zinazofanana.

“Serikali imeunda Tume ya Mishahara na Motisha inayofanya mapitio ya ngazi za mishahara ili kuondoa utofauti wa mishahara kwa watumishi waliosoma ngazi moja, wenye taaluma moja wanaofanyakazi kwenye kituo kimoja.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa suala la uwiano wa mishahara kwa watumishi wenye taaluma zinazofanana ni muhimu na linapaswa lifanywe kwa watumishi wote bila ya kujali kama mtumishi huyo ni Mtanzania au anatoka nje ya Tanzania. 

Awali, Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

(mwisho)
Read More

MAJALIWA AFUNGUA AWAMU YA PILI YA UPANUZI WA HOSPITALI YA AGA KHAN JIJINI DAR

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 9, 2019 amefungua awamu ya pili ya upanuzi hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam. Pichani ni jengo lililozinduiliwa.
Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akikagua chumba cha kisasa cha upasuaji wakati alipofungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam,  Machi 9, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Binti Mfalme, Zahra Aga Khan  (wapili kushoto) wakifurahia baada ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo yaJamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa,  (Agence Francaise de Developpment), Christian Yoka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipita katika maeneo ya hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salam baada ya kufungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali hiyo jijini D, Machi 9, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katika sherehe za ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. Kulia kwake ni Binti Mfalme, Zahra Aga Khan na kushoto kwake ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema. 


Read More

Friday, March 8, 2019

KIFO CHA KIBONDE NI PENGO KUBWA KWA TAIFA-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Mtangazaji Muandamizi wa kituo cha redio cha Clouds, Ephraim Kibonde ni pengo kubwa kwa Taifa, Clouds Media Group na tasnia ya habari kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 8, 2019) alipokwenda kuhani msiba wa Mtangazaji Muandamizi kituo cha redio Clouds, Kibonde kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mbezi Beach Dar es Salaam.Kibonde alifariki dunia jana alfajiri Machi 7, 2019 jijini Mwanza.

“Msiba huu umetushtua sana na ni tukio ambalo hatukulitarajia ila ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hivi karibuni sote tulimshuhudia akiongoza ratiba ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na alienda hadi Kagera kumzika.”

Waziri Mkuu amesema marehemuKibonde enzi za uhai wake ameshirikiana vizuri na Serikali katika shughuli mbalimbali, hivyo amewaomba wananchi waendelee kushikamana na kuifariji familia. “Tumuombee marehemu apumzike kwa amani.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wazazi, watoto wa marehemu pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa na subira na watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao. 


 (mwisho)
Read More

MAJALIWA ATOA POLE KWA FAMILIA YA MTANGAZAJI WA CLOUDS FM, EFRAIM KIBONDE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Mtangazaji wa Clouds FM, Efraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Samson Job Kibonde ambaye ni baba mzazi wa Mtangazaji wa Clouds FM, Ephrim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimfariji Hilda Samson Kibonde ambaye ni mama mzazi wa Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao  marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimfariji Hilda Samson Kibonde ambaye ni mama mzazi wa Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao  marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam, kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Samson Job Kibonde ambaye ni baba mzazi wa Mtangazaji wa Cloud FM, Ephrim Kibonde wakati alipokwenda nyumbani kwao marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es salaam kutoa pole kwa familia, Machi 8, 2019. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Clouds Media, Joseph Kusaga.


Read More

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWAASA WANAWAKE KUDUMISHA UPENDO NA UMOJA

NA.MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde amewaasa wanawake kudumisha upendo na umoja katika kushiriki shughuli za maendeleo nchini kwa kushikamana pamoja bila kujitenga.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 08, 2019 katika Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama.
Maadhimisho ya mwaka huu yana kauli mbiu inayosema “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”
Naibu Waziri alibainisha miongoni mwa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya wanawake ni pamoja na kukosekana kwa umoja, upendo na ushirikiano ambao unawaga katika makundi na kusababisha wanawake kutokuwa na maendeleo ya pamoja.
“Niseme ukweli japokuwa hamtaupenda kwa leo, miongoni mwa sababu zinazowakwamisha katika kuendelea ni tabia ya chuki miongoni mwenu, umbeya na makundi yasiyoleta tija za kimaendeleo,”alieeza Mavunde
Aliongezea kuwa, wanawake wanapaswa kubalidi mitazamo na tabia ambazo zinawaga na kuondoa upendo kati yao na kujikuta wanajitenga hivyo, kupunguza nguvu kazi ya pamoja katika uzalishaji na kuchangia kusuasua kwa maendeleo yao.
Aidha Mavunde alieleza kuwa, kwa kuzingatia mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo nchini ni vyema wakaishi kwa upendo na umoja ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.
“Kimsingi wanawake ni nguzo imara inayotegemewa na Taifa kwa kuzingatia uthubutu na namna Mungu alivyowapa roho ya kuvumilia na kuwaamini katika utendaji wenye uadilifu,”alisisitiza Mavunde
Aidha alieleza kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu jamii haina budi kutathmini hatua tulizofikia kama Taifa katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana na kutumia maadhimishi hayo kama fursa ya namna bora ya kukabili changamoto zinazowakabili wanawake katika kujiletea maendeleo. 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake TUCTA Bi.Rehema Ludanga alieleza furaha yake kwa mwitikio mkubwa wa Wanawake Mkoani Dodoma kwa ushiriki wao pamoja na kuipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuendelea kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa kuanzisha madawati ya jinsia ambayo yanatoa fursa za kutetea haki za wanawake nchini.
“Kipekee nawapongeza wanawake wote waliojitokeza kuiadhimisha siku hii muhimu pamoja na Serikali yetu sikivu kwa jitihada zake za kuendelea kuwaangalia wanawake na haki zao kwa kuanzisha madawati ya jinsi 422 nchini yanayotoa fursa za kusikiliza masuala yanayowakabili wanawake nchini,”alisisitiza Rehema

=MWISHO=
Read More

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWAASA WANAWAKE KUDUMISHA UPENDO NA UMOJA

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika maandamano ya kuadhimishi siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Viwanja vya Mashujaa Dodoma.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika maandamano ya kuadhimishi siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Viwanja vya Mashujaa Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde akihutubia wanawake walioshiriki wakati wa Maadhimishi ya Siku ya Wanawake Duniani Mchi 8, 2019 katia Viwanja vya Mashujaa Dodoma yenye Kauli mbiu isemayo “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu” 
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho hayo.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa maadhimisho hayo.
Kikundi cha bendi ya JUKIMSI wakionesha umahiri wao wa kuimba wakiwa katika gari maarufu kwa jina la “kijiko” wakati wa maadhimisho hayo.


Mmoja wa wanawake mahiri katika fani ya udereva wa magari makubwa (kijiko) Bi.Easther akionesha umahiri wake wa kuendesha gari hilo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa kimkoa Viwanja vya Mashujaa Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde akiangalia moja ya mfuko ulioshoinwa kwa kitengo na kikundi cha Angel kutoka Dodoma wakati wa maadhimisho hayo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde akiangalia akiangalia moja ya bidhaa ya mafuta inayotengenezwa na kikundi cha Farijika wakati akitembelea mabanda ya maonesho katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Read More

Thursday, March 7, 2019

WATUMISHI OFISI YA WAZIRI MKUU WAPANDA MITI 250 KATIKA OFISI ZAO MPYA IHUMWA DODOMA.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Nigel Msangi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa ofisi yake nje ya jengo jipya la ofisi hiyo linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakiosha mikono mara baada ya zoezi la kupanda miti katika eneo la Ofisi zao mpya katika Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Nigel Msangi (katikati mwenye shati lenye madoa meupe na meusi) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya zoezi la kupanda miti katika Ofisi zao mpya Ihumwa Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uratibu wa Maafa (Mipango na Utafiti) Bw.Bashiru Taratibu akipanda mti katika zoezi la upandaji miti 250 katika Ofisi yao mpya Ihumwa Dodoma.
Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakipanda miti aina ya Midodoma katika eneo la Ofisi zao katika Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma Machi 7, 2019.
Mtaalam wa masuala ya misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Bw.Chambo akionesha moja ya miti aina ya midodoma kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu walioshiriki katika zoezi la upandaji miti 250 katika ofisi zao mpya zinazoendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Nigel Msangi akizungumza na watumishi wa Ofisi yake wakati wa zoezi la upandaji wa miti 250 katika eneo la ofisi yao mpya katika Mji wa Serikali Ihumwa Dodoma Machi 7, 2019.
Afisa Mwandamizi (Utawala na Itifaki) Idara ya Maadhimisho na Sherehe za Taifa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Steven Magoha akipanda mti wakati wa zoezi hilo.
Msaidizi wa Ofisi Idara ya Uratibu wa shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Zuhura Omari akipanda mti wakati wa zoezi hilo.
Afisa Mwandamizi (Utawala na Itifaki) Idara ya Maadhimisho na Sherehe za Taifa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi Isabela Katondo akipanda mti wakati wa zoezi hilo.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sekta Binafsi Bw.Vedastus Manumbu akishiriki zoezi la kupanda miti katika eneo la jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Ihumwa Dodoma

Read More

Saturday, March 2, 2019

WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA WARSHA YA MAFUNZO KWA VIONGOZI NA WADAU WA MKOA WA TANGA KUHUSU MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI

NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama leo Machi 2, 2019 amefungua warsha ya mafunzo kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kuja Tanga, Tanzania.
Warsha hiyo iliwakutanisha zaidi ya wadau 70 wakiwemo viongozi Waandamizi na Watendaji Wakuu wa Mkoa wa Tanga, Wafanyabiashara wa mkoa huo pamoja na wanahabari na kufanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo ambayo itafanyika kwa muda wa siku mbili (Machi 02 na 03, 2019),Mhagama alisema Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kutumia fursa ya mradi huo katika kujiletea maendeleo yao nan chi kwa ujumla. 

“Mkutano huu wa leo ni matumaini kuwa, utaleta mageuzi makubwa ya mipango mikakati yetu ili kuangalia fursa za ujio wa mradi huu kwa kuzingatia ni moja kati ya mradi unaotarajiwa kuwa na manufaa  mengi kwa nchi katika kuzalisha ajira, kuendeleza urithishaji wa ujuzi na teknolojia pamoja na ubia kati ya makapuni ya Tanzania na wageni,”alisema Mhagama
Waziri aliongezea kuwa, inawapasa wananchi kutumia warsha hiyo kujadili na kuweka mikakati bora ya kuzitumia fursa zitakazotokana na mradi kwa kuzingatia malengo mahususi ikiwemo kujadili maendeleo ya mradi na fursa za ushiriki wa Watanzania katika ujio ya mradi pamoja na kuwa na majadiliano kati ya Sekta Bonafsi ya Umma ili kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi
Aliongezea kuwa, mradi huo utasaidia jamii kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo kwa kuzingatia kuwa, ni zaidi ya robo tatu ya Bomba hili litapita Tanzania na kuwanufaisha wananchi wake.
“Matarajio ni makubwa kwa kuzingatia mradi huu unatarajiwa kupita katika mikoa 8 ikiwemo Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga ambapo litapita katika Wilaya 24, Kata 134 na Vijiji zaidi 180 hivyo hatuna budi kuchangamkia fursa kwa kuongeza jitihada za ongezeko la ushiriki wetu,”alisistiza Mhagama
Naye Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shiga aliendelea kuhimiza watendaji wake kushiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi kama Mkoa ili kuona namna bora za kushiriki katika fursa hiyo kubwa ya kujileea maendeleo yao.
Naye Katibu Mtendaji, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi.Beng’I Issa alieleza jitihada za Baraza ikiwemo kuanzishwa kwa kanzi data ya nguvu kazi ambayo inachukua takwimu za wafanyabiashara ili kiuwatambua kwa lengo la kushirikisha katika program na kuona namba bora ya kuwashirikisha katika fursa hizo.
“Niwaombe watanzania kuendelea kujisajili katika kanzi data ya nguvu kazi ili tuweze kuwatambua, uwezo na changamoto zenu na kuwashirikisha katika miradi mbalimbali ukiwemo huu wa bomba la mafuta pamoja na kutatua changamoto hizo,” alisisitiza Beng’i
AWALI
Warsha ya mafunzo hayo imeratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa ufadhili wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kupitia BEST Dialogue Tanzania kwa lengo la kuwezesha viongozi na Wafanyabiashara wa Mkoa huo kufahamu maendeleo na fursa zitakazotokana na mradi huo.Bomba hilo la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lina urefu wa KM 1,443 kati ya hizo KM 296 zipo nchini Uganda na KM 1,147 zipo Tanzania

=MWISHO=
Read More

Friday, March 1, 2019

WAZIRI MHAGAMA AHIMIZA JAMII KUPIMA VVU


NA.MWANDISHI WETU

JAMII imeshauriwa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU ili kupata huduma mapema na kuchukua hatua muhimu ya kunendelea kulinda afya za wasio na maambukizi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama alipokuwa akizindua kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Machi 1, 2019. 

Waziri Mhagama aliwahimiza wananchi kupima VVU  ili kufanikisha mpango wa 90 tatu na kutoa hamasa kubwa kwa wanaume kuwa mstari wa mbele katika kupima afya zao,na wakina mama kisiwe kipimo chao. 

“Ili kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi nchini, asilimia 95 ya watanzania ambao hawana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI inapaswa walindwe ili wasiambukizwe na kundi la wanaume wawe mstari wa mbele kujitokeza kupima afya zao,”alisema Mhagama.

Waziri aliongezea kuwa ni vyema jamii kuendelea kujilinda ili kuepuka maambukizi mapya yanayosababisha takwimu za maambukizi nchini kuongezeka badala ya kupungua.

“Pia asilimia tano ya watanzania ambao wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI inapaswa walindwe ili asilimia hizo zisiongezeke kutokana na mpango wa 90 tatu”, alisisitiza Mhagama. 

Alisema pia kwenye asilimia hiyo 90 watakaopima na kukuta wamepata maambukizi wanapaswa kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ili kuhakikisha maambukizi mapya yanatokomezwa kabisa hapa nchini.

Aliwataka wananchi wa eneo hilo kutumia kituo hicho kwa kutunza afya zao na kuishi kwa furaha kwani kinawahusu wenye maambukizi na wale wanaohitaji kujua afya zao. 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti alisema Mirerani ndiyo sehemu inayoongoza kwenye mkoa huo kwa kuwa na watu wengi wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kulinganisha maeneo mengine katika mkoa huo. 

Alisema maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Manyara ni asilimia 2.3 na kwenye mji mdogo wa Mirerani ni asilimia 16 hivyo eneo hilo pekee ndilo linasababisha mkoa huo kuwa na asilimia kubwa za maambukizi na kuwataka wananchi kuchukua hatua za dhati za kupambana kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja kwa kuhamasisha kupima na kutumia dawa endapo unagundulika na maambukizi.

"Huu ugonjwa umekaa mahali pabaya mno, ningekuwa na jeshi kama lililojenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ningetumia kuzuia UKIMWI lakini siwezi kufanya hivyo ila niwahimize mjitokeze kwa hiari kuja kupima katika kituo hiki," alisisitiza Mnyeti. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa kudhibiti UKIMWI, Bw. Godfrey Simbeye alisema kituo hicho kimegharimu jumla ya shilingi Milioni 250 ambapo shilingi Milioni 200 ni kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Kituo na Shilingi Milioni 50, ununuzi wa samani na vifaa tiba na litahudumia watu 49,802.

Simbeye ameiomba serikali isaidie mfuko kuhakikisha kinapatikana chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa fedha kwani michango pekee haitoshelezi Mfuko huu .
Aidha amewaomba wadau wengine na wafanyabiashara kujitokeza kuchangia katika mfuko huo kupitia namba ya simu 0684 909090 ili kuendelea kudhibiti VVU na UKIMWI nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko alisisitizia umuhimu wa wananchi kushiriki na kutumia kituo hicho kikamilifu kipima afya zao na kuanza dawa kwa kadri watakavyoelekezwa na wahudumu wa afya.

Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mhe. James Ole Millya aliishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho na kuwaasa wananchi kujikinga na maambukizi mapya ya VVU ili kuendelea kuwa na afya njema na kujiletea maendeleo yao.

Mwakilishi wa watu wanaoishi na VVU  Wilayani Simanjiro, Wariandumi Kweka alisema kituo hicho kitawasaidia kwani awali walikuwa wanakwenda umbali mrefu kufuata huduma hiyo na wengi kukatishwa tamaa na hali hiyo na kuendelea kuitaka jamii kubadili mitazamo hasi juu yao na kuwapa ushirikiano na kupinga imani potofu za baadhi ya madhehebu  yanayopinga matumizi ya dawa hizo kwa imani ya  kupona bila kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo. 

=MWISHO=
Read More

WAZIRI MHAGAMA AHIMIZA JAMII KUPIMA VVU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akipokea vifaa tiba pamoja na vifaa saidizi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Biashara Banki ya NMB Bw.Filbert Mponzi wakati wa uzinduzi wa Kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akihutubia wananchi wa Mirerani wakati wa warsha ya uzinduzi wa Kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Machi 1, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akifunua kitambaa mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Machi 1, 2019. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko akihutubia wananchi wa Mirerani wakati wa warsha hiyo.
Baadhi ya wakazi wa Mirereni wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa kituo hicho.
Baadhi ya wakazi wa Mirereni wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa kituo hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akimpongeza msanii kutoka Sanaa madini group, Alex alipoimba wimbo wa kuhamasisha jamii kupima VVU wakati uzinduzi wa Kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akiangalia mtoto aliyezaliwa katika Kituo hicho Mapema mwishoni mwa wiki hii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akimpongeza Bi.Jenita Vicent mara baada ya kujifungua mtoto wa kike katika kituo hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na msimamizi wa Kituo cha Afya cha Mirerani Dkt.Hassan Ishabailu mara baada ya kuwasili na kukagua shughuli za kituo hicho Machi 1, 2019 katika Wilaya Simanjiro Mkoani Manyara.

Read More