Friday, March 1, 2019

WAZIRI MHAGAMA AHIMIZA JAMII KUPIMA VVU


NA.MWANDISHI WETU

JAMII imeshauriwa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU ili kupata huduma mapema na kuchukua hatua muhimu ya kunendelea kulinda afya za wasio na maambukizi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama alipokuwa akizindua kituo cha kutolea huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara Machi 1, 2019. 

Waziri Mhagama aliwahimiza wananchi kupima VVU  ili kufanikisha mpango wa 90 tatu na kutoa hamasa kubwa kwa wanaume kuwa mstari wa mbele katika kupima afya zao,na wakina mama kisiwe kipimo chao. 

“Ili kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi nchini, asilimia 95 ya watanzania ambao hawana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI inapaswa walindwe ili wasiambukizwe na kundi la wanaume wawe mstari wa mbele kujitokeza kupima afya zao,”alisema Mhagama.

Waziri aliongezea kuwa ni vyema jamii kuendelea kujilinda ili kuepuka maambukizi mapya yanayosababisha takwimu za maambukizi nchini kuongezeka badala ya kupungua.

“Pia asilimia tano ya watanzania ambao wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI inapaswa walindwe ili asilimia hizo zisiongezeke kutokana na mpango wa 90 tatu”, alisisitiza Mhagama. 

Alisema pia kwenye asilimia hiyo 90 watakaopima na kukuta wamepata maambukizi wanapaswa kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ili kuhakikisha maambukizi mapya yanatokomezwa kabisa hapa nchini.

Aliwataka wananchi wa eneo hilo kutumia kituo hicho kwa kutunza afya zao na kuishi kwa furaha kwani kinawahusu wenye maambukizi na wale wanaohitaji kujua afya zao. 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe.Alexander Mnyeti alisema Mirerani ndiyo sehemu inayoongoza kwenye mkoa huo kwa kuwa na watu wengi wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kulinganisha maeneo mengine katika mkoa huo. 

Alisema maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Manyara ni asilimia 2.3 na kwenye mji mdogo wa Mirerani ni asilimia 16 hivyo eneo hilo pekee ndilo linasababisha mkoa huo kuwa na asilimia kubwa za maambukizi na kuwataka wananchi kuchukua hatua za dhati za kupambana kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja kwa kuhamasisha kupima na kutumia dawa endapo unagundulika na maambukizi.

"Huu ugonjwa umekaa mahali pabaya mno, ningekuwa na jeshi kama lililojenga ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ningetumia kuzuia UKIMWI lakini siwezi kufanya hivyo ila niwahimize mjitokeze kwa hiari kuja kupima katika kituo hiki," alisisitiza Mnyeti. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa kudhibiti UKIMWI, Bw. Godfrey Simbeye alisema kituo hicho kimegharimu jumla ya shilingi Milioni 250 ambapo shilingi Milioni 200 ni kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Kituo na Shilingi Milioni 50, ununuzi wa samani na vifaa tiba na litahudumia watu 49,802.

Simbeye ameiomba serikali isaidie mfuko kuhakikisha kinapatikana chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa fedha kwani michango pekee haitoshelezi Mfuko huu .
Aidha amewaomba wadau wengine na wafanyabiashara kujitokeza kuchangia katika mfuko huo kupitia namba ya simu 0684 909090 ili kuendelea kudhibiti VVU na UKIMWI nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko alisisitizia umuhimu wa wananchi kushiriki na kutumia kituo hicho kikamilifu kipima afya zao na kuanza dawa kwa kadri watakavyoelekezwa na wahudumu wa afya.

Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mhe. James Ole Millya aliishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho na kuwaasa wananchi kujikinga na maambukizi mapya ya VVU ili kuendelea kuwa na afya njema na kujiletea maendeleo yao.

Mwakilishi wa watu wanaoishi na VVU  Wilayani Simanjiro, Wariandumi Kweka alisema kituo hicho kitawasaidia kwani awali walikuwa wanakwenda umbali mrefu kufuata huduma hiyo na wengi kukatishwa tamaa na hali hiyo na kuendelea kuitaka jamii kubadili mitazamo hasi juu yao na kuwapa ushirikiano na kupinga imani potofu za baadhi ya madhehebu  yanayopinga matumizi ya dawa hizo kwa imani ya  kupona bila kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo. 

=MWISHO=


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.