Wednesday, March 27, 2019

UJENZI WA MJI WA SERIKALI WAKAMILIKA KWA 99%-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema nia ya dhati ya Rais Dkt. John Magufuli ya kujenga upya mji wa Serikali imetekelezwa baada ya mji huo kukamilika kwa asilimia 99.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Machi 27,2019) alipotembelea mji mpya wa Serikali unaojengwa katika eneo la Mtumba, Jijini Dodoma. Majengo ya wizara 20 yamekamilika.

Katika ziara yake hiyo, Waziri Mkuu ametembelea na kukagua majengo ya Wizara 13, ambapo amesema ameridhishwa na hatua za ujenzi zilizofikiwa katika maeneo mengi.

Hata hivyo katika maengo hayo ya wizara 13 aliyoyatembelea, Waziri Mkuu, alibaini kasoro kwenye mlango wa kuingilia katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemuagiza mkandarasi anayejenga jengo hilo auondoe na aweke mwingine kwa kuwa mbao zilizotumika zipo chini ya kiwango na haupendezi.

Kadhalika, kuhusu ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ambayo bado haikamilika, Waziri Mkuu amemuongezea siku 10 mkandarasi na kumtaka akamilishe.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu wahakikishe kazi iliyosalia ambayo ni ya kuboresha mazingira ya nje ya ofisi hizo iwe imekamilika ifikapo Apriri 15, mwaka huu. Mji huo unatarajiwa kuzinduliwa na Rais Dkt. Magufuli.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema ujenzi wa mji huo ulianza Desemba mwaka jana na ulitarajiwa ukamilike Februari mwaka huu lakini utakamilika Mei mwaka huu.

Waziri Jenista alisema ujenzi wa majengo ya wizara tatu ambayo hayajakamilika ikiwa ni pamoja na OR-TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Wenye Ulemavu yatakamilika Mei mwaka huu.

 (mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.