Kwa mara ya kwanza Barani Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza
kufanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Afya moja juu ya namna ya kufanya tathmini ya vimelea hatarishi vya
magonjwa kwa kutumia dhana ya Afya moja. Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalam
na wadau wa Afya moja kutoka sekta mbalimbali, hususan sekta za afya ya binadamu,
wanyama, kilimo na mazingira.
Kufuatia nchi ya Tanzania kuwa imepiga hatua
katika uratibu wa masuala ya Afya moja,
ambayo ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo
na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa
yanayoathiri binadamu, hali hiyo imechagiza kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza
barani Afrika kwa wataalam wa sekta za
Afya hapa nchini kupewa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 25-28 Machi, 2019, Jijini
Dar es salaam, yaliendeshwa na wataalamu kutoka Makao makuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Makao makuu ya
Shirika la Chakula Duniani (FAO), pamoja na Shirika linaloshughulika na Afya ya
Wanyama (IOE). Wataalamu hao wameweza kuwapa mafunzo wataalamu wa sekta za Afya
hapa nchini juu ya namna ya kufanya tathmini hiyo kwa magonjwa ya Kichaa cha
mbwa, Kimeta na Homa ya Mafua ya ndege.
Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uratibu
Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, alibainisha kuwa ushirikiano
wa wataalam na sekta za Afya kwa kutumia
dhana ya Afya Moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima. Aidha amefafanua
kuwa dhana hiyo inapunguza gharama
katika kushughulikia tishio la magonjwa
yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama na kwenda kwa
binadamu na hata mimea (mazingira) na kusababisha magonjwa na hata usugu wa
vimelea vya magonjwa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti washiriki wa mafunzo hayo wamebainisha kuwa wamekuwa wakifanya tathmini za vimelela
hatarishi vya magonjwa hapa nchini lakini tathmini hizo zimekuwa ni za kisekta
kwani hazikuwa zinazingatia ushirikiano kwa maana ya dhana ya Afya moja. Aidha
walifafanua kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuandaa nyenzo ya kitaifa ya
kufanya Tathimini kwa Dhana ya Afya Moja ambayo itawaongoza Wataalamu hususani wanapokuwa katika maeneo halisi
yanakotokea magonjwa.
Aidha, washiriki hao
walieleza kuwa Dhana ya Afya Moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea
vingi vinavyo sabababisha magonjwa kwa binadamu asilimia (60%) vinatoka kwa wanyama pori na mifugo na maambukizi
yanatokea pale binadamu anapoingilia maskani ya wanyama hao bila tahadhari.
Hata hivyo, kwa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuzingatia kuwa Bara
la Afrika hususan sehemu zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama (Congo Basin)
ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa(RVF),
Marburg na mengineyo.
Walibainisha kuwa, Kupitia matokeo ya
mwingiliano kati ya wanyama na binadamu, wadau wa afya moja wanawajibika
kupanga mikakati mbalimbali ya udhibiti, ulinzi na usalama katika kuzuia,
kujiandaa na kukabali magonjwa ambukizi. Moja ya mkakati ulioibuliwa Kitaifa na
kimataifa ni kujiandaa kwa kuwafundisha
wataalam wa sekta mbalimbali za
afya jinsi ya kufanya tathmini ya
hatari ya vimelea vya magonjwa ambukizi kwa ushirikiano.
Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya
moja nchini. Kwa kutambua umuhimu huo
Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati la Uratibu wa Afya
moja kwa kushirikiana na WHO, FAO, IOE na wadau wengine wa Afya moja waliandaa na kuratibu mafuzo
hayo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.