Na. OWM, MOROGORO
Afya Moja ni dhana
inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu , wanyamapori, mifugo na
mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri
binadamu ,wanyamapori na mifugo.
Kwa kutambua umuhimu wa Afya moja nchini, sekta za
Afya zenye kujumuisha wataalam wa sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya
wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wametakiwa kuanza kutekeleza
majukumu yao kwa kuzingatia dhana hiyo ili uimarishaji wa Afya ya binadamu uwe
wa Ufanisi na matokeo bora.
Akiongea wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja kutoka
Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika ya
serikali na ya Kimataifa, mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019,
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Matamwe Jimmy, amefafanua
kuwa tayari wataalamu hao wanao Mkakati wa kuzileta pamoja Sekta za Afya kwa ajili ya kuzuia, kukinga na
kuthibiti madhara na magonjwa yanayoikumba nchi yetu, yaani magonjwa ambukizi
kati ya wanyama na binadamu pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa hivyo ni
wakati wa kutekeleza mkakati huo kwa kuitumia dhana ya Afya moja.
“Ninaamini kwamba, wote mnafahamu kuhusu tishio kubwa la magonjwa kama
vile homa ya bonde la ufa, kwenye nchi za Afrika Mashariki , virusi vya Ebola
Afrika Magharibi, kusambaa kwa kiasi kikubwa cha ugonjwa wa mafua ndege,
(HPAI), matatizo ya kupumua yanayosababishwa na virusi vya Corona, mlipuko wa
homa ya Lassa huko Africa Magharibi na homa ya Zika huko Amerika ya Kusini, kwa
hiyo mifano michache magonjwa hayo yamekuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu
na wanyama duniani kote.” Amesisitiza Kanali Matamwe.
Wakiongea
wakati wa warsha hiyo wataalamu wa sekta za Afya hizo wamebainisha kuwa tayari wamekubaliana mfumo wa kutoa taarifa na kuhuisha
utekelezaji wa mpango mkakati wa afya moja nchini.
Tarehe 13 Februari 2018,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa
alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa
na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini. Kwa kutambua
umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati
la Uratibu wa Afya moja kwa kushirikiana na USAID na Chemonics
International wameandaa mkutano wataalam hao.
MWISHO.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akieleza jambo wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019. |
Mtaalamu wa Afya moja toka sekta ya Afya ya Mifugo, Dkt. Joseph Masambu akichangia juu ya umuhimu wa dhana ya Afya moja nchini wakati wa warsha ya maafisa viungo wa Afya moja mjini Morogoro leo tarehe 26, Februari, 2019. |
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.