Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amewataka watumishi wa umma
kujenga tabia ya kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika
utekelezaji wa majukumu ya serikali.
Dkt. Yonazi ametoa wito huo
leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa PEPMIS
yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Ngome.
Akihimiza dhana ya kujifunza
kwa kushiriki kikamilifu, Dkt. Yonazi alinukuu kauli maarufu ya Benjamin
Franklin isemayo: “Niambie nisahau, nifundishe nitakumbuka, nishirikishe
nijifunze.”
Alisisitiza umuhimu wa
ushiriki wa kila mmoja akisema: “Tuchukue sehemu ya tatu ya kauli hiyo kwa
sababu tunachohitaji ni kujihusisha ili tuweze kujifunza zaidi na kuimarisha
utendaji wetu.”
Aidha, Dkt. Yonazi aliwataka
watendaji wote kuchangamkia fursa hiyo ya mafunzo ya PEPMIS ili kupata maarifa
mapya yatakayosaidia katika kutathmini na kuboresha utendaji kazi wao wa kila
siku.
Kwa upande wake, Bw. Mutani
Josephat Manyama – Mkufunzi wa Kitaifa wa Mfumo huo kutoka Ofisi ya Rais
(Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), alieleza kuwa mafunzo hayo
ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa umma kuhusu utekelezaji
na tathmini ya utendaji kazi wao.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo
yatawawezesha viongozi na wasimamizi kufanya tathmini sahihi ya watendaji,
jambo litakalosaidia maamuzi bora ya kiutumishi na kuongeza tija katika
utumishi wa umma.