Friday, February 9, 2018

WATOTO WASIRUDISHWE NYUMBANI SABABU YA MICHANGO-MAJALIWA

*Asisitiza ni kinyume na maelekezo ya Serikali

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kitendo cha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku michango ya aina yoyote isiyo ya lazima katika Elimu msingi.

Waraka huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 sambamba na maelekezo ya Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inayosisitiza utoaji wa Elimumsingi bila malipo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusu baadhi ya shule kuchangisha michango mbalimbali kutoka kwa wazazi na walezi na kusababisha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni.

Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na Serikali, ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo yamefafanuliwa.”

Akizungumzia fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2017, Serikali imetuma moja kwa moja shuleni jumla ya sh. bilioni 124.8.

“Fedha zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za Serikali. “

“Ruhusa ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi. Hata hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ashirikishe Kamati ya Shule za Msingi na Bodi kwa Shule za Sekondari. Walimu wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kukusanya taarifa kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Serikali kwa lengo la kujua hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa changamoto ya umiliki wa ardhi kutokana na baadhi ya shule kutokuwa na hati miliki, ambapo inatarajia   kuhusisha shule za Sekondari Kongwe zipatazo 89.

Amesema zoezi hilo litakapokamilika litawezesha Serikali kuandaa hati miliki kwa shule zenye umiliki wa Serikali na pia kufanya maamuzi kwa shule ambazo umiliki wake uko chini ya taasisi za dini.

Waziri Mkuu amesema kupitia zoezi hilo maeneo ya mipaka ya shule ikiwemo viwanja vya michezo vitatambuliwa na kujumuishwa kwenye ramani za shule. “Zoezi la ufuatiliaji wa umiliki wa ardhi kwa shule za msingi na shule za Sekondari zilizobaki za Serikali litaendelea kufanyika ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.”
Read More

AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI YAONGEZEKA-MAJALIWA


 *Asema rekodi hiyo haijawahi kufikiwa kwa miaka minne

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 5.91 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa takriban miaka minne kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, pia thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi imekuwa takriban dola za Marekani bilioni 8.695 ikilinganishwa na wastani wa dola bilioni 8.828 kwa miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo Waziri Mkuu ameongeza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka ni wa kuridhisha ambapo ukusanyaji wa mapato ulifikia Sh. trilioni 12.95 sawa na asilimia 82.8 ya lengo lililopangwa katika kipindi hicho.

Amesema matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali za kuhudumia wananchi na miradi ya kipaumbele ambayo ni
kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge.

Pia kugharamia Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo, kugharamia Mpango wa Ununuzi wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi na utekelezaji wa miradi ya usambazaji maji vijijini na mijini na usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA.

Miradi mingine ni ununuzi wa meli za abiria na mizigo katika maziwa, ukarabati na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya Ndege na kujenga na kuendeleza maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini.

“Hakika kwa mafanikio haya tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa uongozi wake mahiri na juhudi anazofanya za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka.”

Waziri Mkuu amesema  Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kuwa inatekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2017/2018 yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuwa na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake.

Vilevile, kuwa na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ambao utasaidia kupanua wigo na kudhibiti ukwepaji wa kodi kupitia urasimishaji wa shughuli za uchumi kwa kuwezesha ukuaji wa biashara katika sekta ndogo na za kati ambazo ndiyo mihimili wa kuzalisha ajira na kukuza uchumi.

Akizungumzia kuhusu viashiria mbalimbali vya kiuchumi, Waziri Mkuu amesema vinaonesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri na pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8.

“Hali hii inaashiria kwamba tuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la mwaka la ukuaji wa asilimia 7.0. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huo ni habari na mawasiliano, uchimbaji madini, biashara, ujenzi na uzalishaji viwandani.”
Read More

Thursday, February 8, 2018

MIGOGORO YA VIJIJI NA HIFADHI: WIZARA YA MALIASILI YAAGIZWA IRUDI KWA WANANCHI KUTOA MAJIBU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii irudi kwenye maeneo yote yenye migogoro ya mipaka na iungane na Halmashauri za wilaya ili waweze kutoa majibu kwa wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Februari 8, 2018) wakati akijibu swali la mbunge wa Urambo, Bibi Margaret Sitta wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.

Bibi Sitta alitaka kujua Serikali imeweka taratibu na mikakati gani ya kumaliza migogoro ya mipaka inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya hifadhi za misitu nchini kwa kuwa wananchi wanahitaji maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.

Waziri Mkuu amesema Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iweke vigingi kwenye maeneo yote yanayozunguka hifadhi za misitu ili kuweka alama zitakazopunguza migogoro ya kuingiliana kati ya wananchi walioko kwenye vijiji na wahifadhi kwenye maeneo ya hifadhi ya misitu hiyo.

Amesema maagizo hayo yalitolewa baada ya kugundua kuwa kuna migogoro mingi kati ya wananchi walioko katika vijiji vya jirani na misitu iliyohifadhiwa kisheria ambayo ina ramani.

“Lakini tunatambua kwamba wanapoendelea na zoezi hilo la uwekaji alama, inaweza kutokea kijiji kikajikuta kipo ndani ya mipaka ya hifadhi na inaweza kusababisha kutoelewana kati ya wanakijiji na wenye mamlaka ya hifadhi.”

“Tuliwasihi wanakijiji wakati zoezi hili linaendelea na hata kama kijiji kitajikuta kimezungukwa na hizo alama, wanakijiji watulie ili kazi ya awali ikamilike na pale kwenye mgogoro, Serikali itarudi tena kuja kuangalia mgogoro huo na kufanya tathmini ya kina.”

Amesema Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii inapofanya kazi hiyo ya kuweka vigingi lazima ishirikishe mamlaka za halmashauri na kijiji husika na wao washiriki katika zoezi hilo ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ilishaielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi izitumie ranchi za NARCO na kugawa katika vitalu ili kubaini ukubwa wa eneo iliyonayo ndipo iweze kufanya uamuzi wa kugawa vitalu hivyo kwa wafugaji.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Nkenge, Balozi Dkt. Diodorus Kamala aliyetaka kujua taarifa ya kamati iliyoundwa na Serikali kufuatilia migogoro ya ranchi zilizokuwa chini ya NARCO na wafugaji, itapelekwa lini bungeni ili iweze kujadiliwa.

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliunda tume ya kufuatilia maeneo yote ya ranchi za Taifa na kuyapima maeneo hayo lakini pia kujua ni akina nani wanayamiliki maeneo hayo, kubaini kama walipewa kihalali, na kama ni kweli wanamiliki mifugo yoyote kwenye maeneo tajwa.

Kuhusu kupelekwa bungeni kwa taarifa ya tume hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Mifugo aikamilishe na kuiwasilisha Bungeni kama taratibu zinavyotaka ili kuwawezesha wabunge na wananchi wajue dira na mwelekeo wa Serikali wa namna ya kufuga mifugo hiyo kwa njia ambazo zitawaletea tija lakini kikubwa zaidi ni kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.



Read More

WAZIRI MKUU BUNGENI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum Kagera, Bernadeta Kasabago kwenye jingo la utawala Bungeni, mjini Dodoma, Februari 8, 2018. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Gairo Ahmed Shabiby, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, katikati ni mbunge wa Bunge la Muungano (CCM) Ayoub Hashim Jaku, Februari 8, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahi jambo na  Mtangazaji Mwandamizi wa TBC, Shaaban Kisu, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Februari 8, 2018.


Read More

SERIKALI YAWATOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote inayolimwa nchini kununuliwa na tayari imeshaanza mchakato wa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 8, 2018) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Sumve, Bw. Richard Ndassa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Bw. Ndassa alitaka kujua Serikali imejipangaje kuwasaidia wananchi walioitikia wito wa kulima pamba iwapo wanunuzi watashindwa kununua pamba yote.

Mbunge huyo ameongeza kuwa mwaka jana, Waziri Mkuu aliwaita viongozi wa mikoa inayolima pamba na kuwapa maelekezo ya kwenda kufufua zao hilo ambapo wakulima waliitikia wito na mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi.

Waziri Mkuu amesema ni kweli kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Serikali iliwaita viongozi hao ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ambao walipewa maelekezo ya kwenda kuhamasisha kilimo cha zao hilo na kuwasaidia wakulima kuanzia ngazi ya awali.

Waziri Mkuu amesema Serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko.

“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo kati ya tarehe 15-17, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua pamba, ili mradi wanajihusisha na pamba,” amesema.

Ili kupata uhakika wa masoko nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) inawasiliana na mataifa mbalimbali ili kuhakikisha pamba yote iliyolimwa nchini inanunuliwa.

“Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba. Mengine ni korosho, kahawa, chai na tumbaku, yote kwa pamoja yanachangia kukuza uchumi,” amesema.

Amesema awali wakulima wa mazao makuu matano ya biashara nchini likiwemo na zao la pamba walipunguza uzalishaji baada ya kukosa usimamizi hali iliyoilazimu Serikali ichukue uamuzi wa kuyafufua kwa kuwa historia inaonyesha kwamba mazao hayo yanachangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akijibu swali kuhusu ukosefu wa dawa za kuulia wadudu ambalo Bw. Ndassa alilalamikia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuagiza dawa hizo kwa kuwa ni sehemu ya mahitaji ya kilimo cha zao la pamba.

“Wiki iliyopita niliona kwenye habari Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba akipokea chupa zaidi za milioni moja na akasema kuwa kuna dawa nyingine chupa zaidi ya milioni mbili zinakuja.”

“Ni jukumu la Bodi hiyo kuhakikisha kuwa dawa za zao la pamba, ziwe za maji au za kupulizia zinapatikana nchini na zinapelekwa kwa wakulima,” alisisitiza.

Read More

BUNGENI LEO TAREHE 08 FEBRUARI,2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkoa wa Geita Upendo Peneza, nje ya jengo la utawala la Bunge Mjini Dodoma, Februari 7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, bungeni mjini Dodoma Februari 7, 2018. 

Read More

WAZIRI MHAGAMA AKITETA NA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Bungeni mjini Dodoma Februari 8, 2018.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Bungeni mjini Dodoma Februari 8, 2018.

Read More

MAJALIWA AKIZUNGUMZA NA WABUNGE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa, Bungeni mjini Dodoma Februari 8, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Mbunge wa Kigoma  Kaskazini, Peter Serukamba kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Februari 8, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Februari 8, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji  Peter Msigwa kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Februari 8, 2018.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wabunge, Murad Sadiq wa Mvomero  (kulia), Suleiman Nchambi wa Kishapu (katikati) na Richard Ndassa wa Sumve kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Februari 8, 2018.

Read More

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKIJIBU MASWALI BUNGENI

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akijibu maswali Bungeni mjini Dodoma Februari 8, 2018.

Read More

Wednesday, February 7, 2018

BUNGENI LEO TAREHE 07 FEBRUARI,2018

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge , Kazi, Vijana, Ajira na  Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akiteta na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, Bungeni mjini Dodoma Februari 7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Bungeni mjini Dodoma Februari7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mbunge wa Hanang, Dkt. Mary Nagu, bungeni mjini Dodoma Februari 7, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuelekea kwenye jengo la utawala la Bunge Mjini Dodoma Februari 7, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Kavuu, Dkt. Pudenciana Kikwembe kwenye jengo la utawala la Bunge Mjini Dodoma, Februari 7, 2018.

Read More

Tuesday, February 6, 2018

BUNGENI LEO TAREHE 06 FEBRUARI,2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri wa Nchini, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Viana, Akira na Wende Ulemavu, Jenista Mhagama (kushoto)  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba (katikati), Bungeni mjini Dodoma Februari 6, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Capt. George Mkuchika,  Bungeni mjini Dodoma, Februari 6, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Agness Marwa, Bungeni mjini Dodoma , Februari 6, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Februari 6, 2018.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Februari 6, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Februari 6, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma Februari 6, 2018.

Read More

Monday, February 5, 2018

HABARI PICHA BUNGENI 05 FEBRUARI,2017

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mbunge wa Kiteto, Emmanuel Papian, Bungeni mjini Dodoma Februari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Bungeni mjini Dodoma Februari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Ileje, Janet Mbene  kwenye viwanja vya Bunge Mini Dodoma Februari 5, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Mji Mkongwe, Ali Saleh kwenye viwanja via Bunge Mini Dodoma Februari 5, 2018.

Read More

Sunday, February 4, 2018

WATU WENYE ULEMAVU JITOKEZENI TUJUE MAHITAJI YENU - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watu wenye ulemavu nchini wajitokeze na kubainisha mahitaji yao ili  Serikali iweze kutambua fursa walizonazo na kuwasaidia.

Ameyasema hayo jana (Jumapili, Februari 4, 2018) wakati alipohudhuria hafla ya chakula cha mchana kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.

“Jitokezeni, hakuna sababu ya kujisikia mnyonge. Serikali hii ni yako, Rais ni wako, una shida gani? Jitokeze ili tujue wewe una fursa ipi, na tunaweza kukusaiidiaje,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua mchango wa Bw. Mengi katika uthamini wa walemavu ambapo hafla hiyo imekuwa ikifanyika kwa miaka 25 sasa na kwamba Serikali imeridhia kuanzishwa taasisi itakayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

“Tunataka tufanye uamuzi wa kuungana na wewe, usilifanye jambo hili kama Dk. Mengi pekee, mimi napendekeza ulifanye kitaasisi, uunde taasisi kwa jina lako ambalo Serikali tumeridhia litumike, Reginald Mengi Disabled Foundation kutokana na kazi nzuri uliyoifanya,” alisema.

Waziri Mkuu alianza kwa kuchangia Sh. milioni 10 ambayo alisema itaingia pindi usajili wa taasisi hiyo utakapokamilika kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya walemavu, Bi. Stella Ikupa alisema Serikali inatambua tatizo la ajira kwa watu wenye ulemavu na imeanza kulifanyia kazi.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kushughulikia tatizo la ajira kwa watu wenye ulemavu. Tulifanya kikao na mwamvuli wa vyama vya waajiri, TUCTA na wadau wengine na kubaini sababu kadhaa zinazofanya watu hawa wakose ajira,” alisema.

“Ili kukabiliana na changamoto hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa kanzidata itakayowezesha watu wenye ulemavu na waajiri kupata takwimu za haraka. Hii ni kwa sababu waajiri walisema wanapokea barua za maombi ya ajira lakini waombaji hawajisemi kwamba wao ni watu wenye ulemavu, hali inayosababisha washindwe kuwatambua na kuwapatia ajira,” alisema.

Akifafanua, Naibu Waziri Ikupa alisema kwenye ajira za kutangazwa, changamoto nyingine iliyoelezwa na waajiri, ni ugumu wa kutambua walemavu wanakopatikana na kwamba kukamilika kwa kanzidata kutasaidia kutambua wapi walipo, na aina gani ya ulemavu walionao.

“Kukamilika kwa kanzidata kutasaidia kurahisisha mawasiliano, na pindi ajira zikitangazwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira na wale waliotoa matangazo ya kazi, itapanga jinsi ya kuwaunganisha na watu wenye ulemavu kulingana na sifa zinazohitajika na nafasi zilizotangazwa,” alisisitiza.

Read More

WAZIRI MKUU ASHIRIKI HAFLA YA CHAKULA NA WATU WENYE ULEMAVU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, katika hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Februari 4, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na muimbaji wa muziki wa kizazi kipya, Saida Kalori, katika hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Februari 4, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi walioshiriki katika hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Februari 4, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpatia chakula mtoto Mwahija Hassan, katika hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Februari 4, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpatia chakula mtoto Ibrahim Shaibu, katika hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Februari 4, 2018.

Read More

Saturday, February 3, 2018

SERIKALI KUIMARISHA MASOKO YA MAZAO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kupata tija.

Aliyasema hayo jana (Februari 2, 2018) wakati akikagua Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha masoko.

Alisema kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imedhamiria kuimarisha masoko  ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kujikwamua kiuchumi.

Kupitia Wizara ya Kilimo tunataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini. Wakati umefika kwa wakulima nchini kuona tija ya mazao wanayolima.”

Alitoa mfano wa zao la pamba ambalo wakulima walikuwa wanaingia mikataba na wanunuzi, mfumo ambao ulikuwa unawanyonya badala ya kuwanufaisha.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX, Bw. Godfrey Malekano alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamejipanga vyema kuanza minada ya mazao.

“Tutaanzia na zao la ufuta mwezi Mei 2018 na kuendelea na mazao mengine kwa kadiri ya misimu ya mazao hayo ilivyo.”

Alisema kufanikiwa kwa Soko la Bidhaa na Mfumo wa stakabadhi ghalani kunategemea sana msaada wa Serikali.  “Soko la Bidhaa la Ethiopia linalotajwa sana kwa mafanikio, limefikia malengo yake kutokana na mkono wa Serikali.” 

 Bw. Malekano alisema kutokana na umadhubuti wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli wanamatumaini makubwa kwamba soko hilo  litatimiza malengo yake.
Read More

Thursday, February 1, 2018

WAZIRI MHAGAMA: MUSWADA WA SHERIA YA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KUNUFAISHA WATUMISHI WA UMMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Rayal Village Dodoma Februari 01, 2018.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kupitishwa kwa muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii utasaidia kuwanufaisha watumishi wa umma kwa kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati na wenye tija.
Amebainisha hayo wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) walipokutana Mjini Dodoma katika warsha ya siku tano kuanzia Januari 29 hadi Februari 02, 2018 kujadili masuala ya wafanyakazi nchini.
Waziri Mhagama alieleza kuwa, kupitiswa kwa muswada ni moja ya utekelezaji wa takwa la Ibara ya 11 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipoona umuhimu wa kuweka mifumo ya hifadhi ili Watanzania wapate manufaa hasa siku za uzeeni.
“Maamuzi ya kuwa na Muswada huu umezingatia taratibu zote za kisheria ikiwemo Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sera ya Hifadhi ya Jamii, Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani unaoongoza katika maswala ya Hifadhi ya Jamii”.Alisisitiza Mhagama
Muswada huu umelenga kuunganisha mifuko ya Pensheni ambayo ni PSPF, LAPF, GEPF NA PPF ili kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi cha kuunganisha mifuko hiyo ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuwa na mfumo madhubuti utakaohakikisha mwanachama anapata mafao kwa wakati.
“Muswada umebainisha kuwa jumla ya mafao 7 yatakayolipwa na mfuko huo itakuwa:  Fao la Pensheni, Warithi, Ulemavu, Uzazi, Ukosefu wa Ajira, Ugongwa na Fao la kufiwa.” alifafanua Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TALGWU Bw. Tumaini Nyamhokya aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kueleza kuwa ni wakati mwafaka kwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kuunga mkono juhudi za Serikali ikiwemo kuunganishwa kwa mifuko hii kwa manufaa ya wafanyakazi wote wa umma.
“Niwaombe watumishi wa umma wote kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maslahi ya watumishi na kwa asilimia 98 muswada huu umeyapitisha mapendekezo na ushauri uliotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na kuwekwa kwenye utekelezaji.”Alisema Nyamhokya.

Naye, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Suleiman Kikingo alisema kuwa kuunganishwa kwa mifuko hiyo na kuwekwa kwa tozo ya asilimia tano kwa mfuko utakao bainika kushelewesha mafao ya mwanachama itasaidia kupunguza changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao kwa wanachama.
Read More

KATIBU MKUU ATEMBELEA KITUO CHA OPERESHENI NA MAWASILIANO YA DHARURA

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa Uboreshaji wa Taarifa za Mabadiliko ya Tabia nchi na mifumo ya utolewaji wa tahadahri za awali Alfei Daniel jinsi mfumo unavyotumika kupata taarifa za hali ya hewa na tahadhari za maafa kutoka vituo mbalimbali nchini vilivyowekwa mfumo huo.
Katibu mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora ametembelea na kukagua kituo cha operesheni ya mawasiliano ya dharura na kujua maendeleo ya kituo hicho kilichopo Ofisi ya kanda Maalumu ya jeshi la Zima moto Jijini Dar es salaam.
Akitoa maelezo ya jinsi mradi huo unavyofanya kazi, Mratibu wa Taifa wa Mradi huo Alfei Daniel, alisema Mradi huo unafuatilia dharura za maafa nchini ikiwemo Ukame na Mafuriko umefadhiliwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani UNDP, ambapo jukumu lake kubwa ni kukusanya taarifa za maafa na vyanzo vyake, kuchambua taarifa hizo, kuhamasisha, kufuatilia, kutoa tahadhari za awali na kuratibu dharura katika ngazi ya kitaifa.
Alfei alifafanua kwamba, mradi huo una vituo 36 tofauti nchini ambavyo vina wawezesha kupata taarifa popote walipo kupitia mtandao maalumu, unaosaidia kutoa tahadhari kwa wananchi wa eneo linalotarajiwa kupata maafa, ambapo mpaka sasa mradi umechukua mabonde mawili yaani bonde la Pangani na bonde la mto Ruvuma.
“Mfumo ambao umefungwa unaweza kutabiri na kutoa taarifa za maafa zinazo weza kutokea popote katika vituo hivyo kwa kutumia mtandao, kwa mfano kujaa kwa maji ambako kuna weza kupelekea mafuriko. Mfumo huu ukikamilika utaweza kuonyesha ramani na vituo vyake vyote vya hali ya hewa.” Alisema Alfei.
Aidha baada ya kupata maelezo ya mradi huo Prof. Kamuzora alishauri mradi huo ufanye jitihada kutoa elimu ya uokoaji kwa wanafunzi mashuleni na raia wote kwa ujumla, na kwa watu wasiokua na elimu ya uokoaji watahadharishwe kukaa mbali na matukio ya maafa kwani wengi wao huathirika au kupoteza maisha katika uokoaji kwa kukosa elimu hiyo.
“Ni lazima uongozi uhakikishe matumizi mazuri ya rasilimali za mradi huu na kuzuia uharibifu wa vifaa na fedha zinazotelewa na mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali kuendesha mradi huu” Aliongeza Prof. Kamuzora.
Bw. Alfei alisisitiza kuwa mfumo huo unasaidia sana TMA katika kutabiri mabadiliko ya hali ya hewa kwa uhakika wa 87%, Wizara ya maji wanaweza kupata data kwa ajili ya kukuza vyanzo vya maji, vile vile hifadhi za taifa zinapata taarifa za hali ya hewa kwa urahisi kwa ajili ya kuhabarisha watalii na kujua mienendo ya wanyama, kwa ujumla huu mfumo unasaidia upatiknaji wa taarifa.

Mradi huu wa Uboreshaji wa Taarifa za Mabadiliko ya Tabia nchi na Mifumo ya utolewaji wa tahadhari za awali ulianza rasmi mwezi Januari, 2017 kwa dhumuni hasa la kuwezesha mawasiliano ya kujitahadhari na maafa,kujiandaa na maafa, na kipindi cha maafa ambapo mawasialiana ya haraka huitajika ili kuokoa maisha na makazi ya watu. Hivyo mradi huu umeundwa ili kuwezesha mawasialiano ya saa 24 kwa siku saba za wiki.
Read More