Sunday, February 4, 2018

WATU WENYE ULEMAVU JITOKEZENI TUJUE MAHITAJI YENU - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watu wenye ulemavu nchini wajitokeze na kubainisha mahitaji yao ili  Serikali iweze kutambua fursa walizonazo na kuwasaidia.

Ameyasema hayo jana (Jumapili, Februari 4, 2018) wakati alipohudhuria hafla ya chakula cha mchana kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.

“Jitokezeni, hakuna sababu ya kujisikia mnyonge. Serikali hii ni yako, Rais ni wako, una shida gani? Jitokeze ili tujue wewe una fursa ipi, na tunaweza kukusaiidiaje,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua mchango wa Bw. Mengi katika uthamini wa walemavu ambapo hafla hiyo imekuwa ikifanyika kwa miaka 25 sasa na kwamba Serikali imeridhia kuanzishwa taasisi itakayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.

“Tunataka tufanye uamuzi wa kuungana na wewe, usilifanye jambo hili kama Dk. Mengi pekee, mimi napendekeza ulifanye kitaasisi, uunde taasisi kwa jina lako ambalo Serikali tumeridhia litumike, Reginald Mengi Disabled Foundation kutokana na kazi nzuri uliyoifanya,” alisema.

Waziri Mkuu alianza kwa kuchangia Sh. milioni 10 ambayo alisema itaingia pindi usajili wa taasisi hiyo utakapokamilika kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya walemavu, Bi. Stella Ikupa alisema Serikali inatambua tatizo la ajira kwa watu wenye ulemavu na imeanza kulifanyia kazi.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kushughulikia tatizo la ajira kwa watu wenye ulemavu. Tulifanya kikao na mwamvuli wa vyama vya waajiri, TUCTA na wadau wengine na kubaini sababu kadhaa zinazofanya watu hawa wakose ajira,” alisema.

“Ili kukabiliana na changamoto hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa kanzidata itakayowezesha watu wenye ulemavu na waajiri kupata takwimu za haraka. Hii ni kwa sababu waajiri walisema wanapokea barua za maombi ya ajira lakini waombaji hawajisemi kwamba wao ni watu wenye ulemavu, hali inayosababisha washindwe kuwatambua na kuwapatia ajira,” alisema.

Akifafanua, Naibu Waziri Ikupa alisema kwenye ajira za kutangazwa, changamoto nyingine iliyoelezwa na waajiri, ni ugumu wa kutambua walemavu wanakopatikana na kwamba kukamilika kwa kanzidata kutasaidia kutambua wapi walipo, na aina gani ya ulemavu walionao.

“Kukamilika kwa kanzidata kutasaidia kurahisisha mawasiliano, na pindi ajira zikitangazwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira na wale waliotoa matangazo ya kazi, itapanga jinsi ya kuwaunganisha na watu wenye ulemavu kulingana na sifa zinazohitajika na nafasi zilizotangazwa,” alisisitiza.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.