Friday, February 9, 2018

WATOTO WASIRUDISHWE NYUMBANI SABABU YA MICHANGO-MAJALIWA

*Asisitiza ni kinyume na maelekezo ya Serikali

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kitendo cha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku michango ya aina yoyote isiyo ya lazima katika Elimu msingi.

Waraka huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 sambamba na maelekezo ya Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inayosisitiza utoaji wa Elimumsingi bila malipo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusu baadhi ya shule kuchangisha michango mbalimbali kutoka kwa wazazi na walezi na kusababisha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni.

Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na Serikali, ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo yamefafanuliwa.”

Akizungumzia fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2017, Serikali imetuma moja kwa moja shuleni jumla ya sh. bilioni 124.8.

“Fedha zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za Serikali. “

“Ruhusa ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi. Hata hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ashirikishe Kamati ya Shule za Msingi na Bodi kwa Shule za Sekondari. Walimu wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kukusanya taarifa kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Serikali kwa lengo la kujua hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa changamoto ya umiliki wa ardhi kutokana na baadhi ya shule kutokuwa na hati miliki, ambapo inatarajia   kuhusisha shule za Sekondari Kongwe zipatazo 89.

Amesema zoezi hilo litakapokamilika litawezesha Serikali kuandaa hati miliki kwa shule zenye umiliki wa Serikali na pia kufanya maamuzi kwa shule ambazo umiliki wake uko chini ya taasisi za dini.

Waziri Mkuu amesema kupitia zoezi hilo maeneo ya mipaka ya shule ikiwemo viwanja vya michezo vitatambuliwa na kujumuishwa kwenye ramani za shule. “Zoezi la ufuatiliaji wa umiliki wa ardhi kwa shule za msingi na shule za Sekondari zilizobaki za Serikali litaendelea kufanyika ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.