Friday, February 16, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI WA KAMPUNI YA PALIMON

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa mradi wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 2.06 wilayani Kwimba.

Ametoa agizo leo (Ijumaa, Februari 16, 2018) wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba. Mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha Mei 28, 2014.

Waziri Mkuu amesema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo amemtaka kamanda wa TAKUKURU kutafuta popote alipo na kumuhoji.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya wananchi wa vijiji vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji vyao. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na wao wapate huduma ya maji.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya maendeleo kulipana posho.

“Fedha zinazopelekwa si za kulipana posho ni za maboresho na Serikali inataka wananchi wahudumiwe wasipate shida.”

Waziri Mkuu amesema watumishi wahakikishe wanawahudumia wananchi ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za maendeleo.

Amesema wilaya hiyo imegeuka kama shimo la kuteketeza fedha za Serikali kwa sababu miradi mingi inayotekelezwa haikamili, hivyo ameitaka ijipange. Alitolea mfano sh. milioni 94 za ujenzi wa mradi wa kliniki ya mifugo ambayo haijakamilika na fedha zimekwisha.


Awali, Waziri Mkuu alifungua mradi wa maji wa kijiji cha Igumangobo kilichopo katika Tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba. Chanzo cha maji hayo ni ziwa Victoria.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.