Tuesday, February 13, 2018

BAHARI KUU, VIWANJA VYA NDEGE VYABAINIKA KUPITISHA DAWA ZA KULEVYA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini kwamba maeneo ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege yanayotumika sana katika kupitisha dawa za kulevya.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema wafanyabiashara, wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya wameendelea kukamatwa, lengo ni kuhakikisha biashara hiyo inamalizika nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akikabidhi gari kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga  kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Amesema mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya sambamba na watumiaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.  

Waziri Mkuu amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulenya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja ilikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na dawa nyingi za kulevya.

“Niwakati wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.”

Pia Waziri Mkuu amewataka Watanzania waachane na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na  kazi ya kusambaza, kuzalisha na kutumia na watakaokamatwa wakijihusisha nayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema kwa sasa Serikali inajenga maabara ambayo itatumiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa wanazozikamata.

Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa mara wanapowabaini wafanyabiashara, watumiaji na wasambazaji wa dawa hizo. Pia wahakikishe wanawalinda vijana ili wasijihusishe na dawa za kulevya.

Kwa upande wake Siyanga aliishukuru Serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo gari, ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waachane na biashara ya dawa za kulevya. Alisema wanapambana kuhakikisha dawa za kulevya ili zisiingie nchini.

Alisema mbali na kudhibiti biashara hiyo, pia wanatoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya vikiwemo vitendo viovu vinavyofanywa na watumiaji ili wachukie na waache kutumia dawa hizo.

Pia wanafanya kazi ya kuwahudumia watu walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya, hivyo aliwaomba wananchi kutowanyanyapaa waathirika na badala yake wawapeleke katika vituo maalumu vya kutolea huduma za methadone.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.