Saturday, February 17, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA KUFUNGULIWA KWA ZAHANATI YA BUGABU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Magu, Dkt. Nindwa Maduhu ahakikishe zahanati Bugabu inafunguliwa leo.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Februari 17, 2018) wakati akiongea na watumishi na wananchi wa wilaya ya Magu katika kituo cha Afya cha Kahangara.

Alisema kama zahanati imekamilika na inavifaa vyote vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma kwa nini watumishi wasipelekwe ili wananchi wahudumiwe.

Alitoa hilo baada ya wananchi kumuomba awasaidie kufunguliwa kwa zahanati ya kijiji chao ili waweze kupata huduma za afya karibu na makazi yao.

Wananchi hao walidai kuwa kwa sasa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita tisa kufuata huduma za afya katika kituo cha Afya cha Kihangara.

Dkt. Maduhu alisema tayari watumishi walishahamishiwa katika zahanati ya kijiji hicho na leo watakwenda na kuanza kuwahudumia wananchi.

Pia Waziri Mkuu amemtaka mganga huyo kuhakikisha dawa zinazonunuliwa wilayani humo kulingana na magonjwa yanayopatikana ndani ya maeneo yao.

Kabla ya kuzungumza na wananchi na watumishi, Waziri Mkuu alikagua na kuweka jiwe la msingi la uboreshaji wa kituo cha Afya Kahangara.

Mradi wa kuboresha kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia watu 26,321 ulianza Oktoba 30, 2017 na umegharimu sh. milioni 500.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.