Saturday, February 17, 2018

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI VIWANDA VYA LAKAIRO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kuweka jiwe la viwanda vya Makampuni ya Lakairo Investment vyenye thamani ya sh. bilioni 25, ambavyo vipo katika kijiji cha Isangijo kata ya Kisesa wilayani Magu.

Ameweka jiwe la msingi la viwanda hivyo leo (Jumamosi, Februari 17, 2018) akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Viwanda hivyo  vinatengeneza steel wire, pipi, vifungashio aina ya viroba

“Nampongeza Bw. Lameck Airo mbunge wa Rorya na Mwenyekiti wa Makampuni ya Lakairo Investment kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi kupitia sekta viwanda.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda na inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika viwanda mbalimbali.

Amesema Serikali itamuunga Bw. Airo mkono ili viwanda hivyo viweze kuzalisha kwa mafanikio makubwa. Pia aliwataka wananchi nao wamuunge mkono muwekezaji huyo kwa sababu viwanda hivyo vinazalisha bidhaa muhimu na kutoa ajira kwa wananchi wengi.

Pia amewaagiza viongozi wa mkoa na halmashauri wahakikishe wanatoa kipaumbe kwa wawekezaji kwa kuwasogezea miundombinu ya huduma mbalimbali zikiwemo za maji na umeme ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Lakairo Investment, Bw. Daniel Lameck alisema mbali na ujenzi wa viwanda hivyo vinavyotarajiwa kutoa ajira 200 hadi 300, pia wanatarajia kujenga viwanda vingine vya kutengeneza mafuta ya kupaka, dawa za viatu na kusaga nafaka.

Bw. Lameck alisema mbali na mafanikio wanayoyapata pia wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa fedha kwa ajiali ya uwekezaji, ambapo alitolea mfano  mpango wao wa kutaka kujenga viwanda vingine viwili ambao umekwama kutokana na upatikanaji wa fedha.

 Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuishauri Serikali iweke mfumo rafiki kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji wa ndani ili viwanda wanavyovianzisha viwe endelevu na vipanuke zaidi.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.