Thursday, February 15, 2018

MADIWANI WA BUCHOSA WAMKATAA MKURUGENZI WAO MBELE YA WAZIRI MKUU


MADIWANI wa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Cyprian Luanda baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Wametoa ombi hilo leo (Alhamisi, Februari 15, 2018) katika kikao cha Waziri Mkuu na watumishi Halmashauri ya Buchosa akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu baada ya kupokea ombi hilo alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella kwenda katika halmashauri hiyo na kufanya kikao cha pamoja kati ya Madiwani, Mkurugenzi na watumishi ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.

Awali, Waziri Mkuu  aliweka jiwe la msingi la hospitali ya Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema, ambapo ujenzi wake hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 10.55.

Pia Waziri Mkuu amezindua madarasa manne ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Secondari ya Nyehunge wilayani Sengerema na kuwata wanafunzi wasome kwa bidii.

Waziri Mkuu amesema wanafunzi hao wanatakiwa wasome sana kwa sababu Rais Dkt. John Magufuli amewaondolea wazazi michango  ya hovyo ili wao wapate fursa ya kusoma.

Pia amewasisitiza walimu wasijiingize katika masuala ya michango ili wajikite na masuala ya taaluma. Kama kuna michango kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri.

Amesema awali wanafunzi walikuwa wanatumika kama njia ya kutengeneza fedha, ambapo wazazi au walezi wanaposhindwa kutoa michango hiyo watoto wao walikuwa wanarudishwa nyumbani. Waziri Mkuu amesema kila mwezi Serikali inapeleka moja kwa moja shuleni sh. bilioni 20.8 kwa ajili ya kugharamia Elimumsingi bila malipo.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.