Thursday, February 22, 2018

TANZANIA YAIPONGEZA FIFA KWA KUPAMBANA NA RUSHWA

SERIKALI ya Tanzania inalipongeza Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa jitihada na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na shirikisho hilo katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kauli hiyo imetolewa leo (Alhamisi, Februari 22, 2018) na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa katika kikao chake na Rais wa FIFA Bw. Gianni Infantino kilichofanyika jijini Dae es Salaam.
“Serikali  tunaunga mkono mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo pamoja na matumizi mabaya ya fedha na ya madaraka yanayofanywa na FIFA”.
Waziri Mkuu amesema wanaunga mkono mapambano hayo ili Taifa liweze kupata mafanikio makubwa katika mpira wa miguu ikiwa ni pamoja na kupata viongozi wenye maono ya mbali katika kuendeleza mchezo huo.
Amesema FIFA ambayo ni kitovu cha mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo , hivyo Tanzania inaiunga mkono kwa kuhakikisha sekta ya michezo inatumia vizuri fedha zilizopo kwa ajili ya kuendeleza michezo.
Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inasimamia matumizi sahihi ya madaraka katika sekta ya michezo nchini ili kuleta maendeleo kwenye mpira wa miguu.
Serikali inaipongeza FIFA kwa jitihada za dhati za kuendeleza mpira wa miguu duniani kwa kuwa mipango mbalimbali ya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana wadogo wa kike na wa kiume nchini.
“Tunatambua msukumo wa FIFA wa kuendelea mpira wa miguu duniani ikiwa ni pamoja na kuboresha viwanja vya michezo pamoja na maendeleo yote wanayoyafanya katika sekta hiyo.

Pia ameishukuru FIFA kwa kuipa Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 yatakayofanyika mwakani jijini Dar es Salaam na kwamba Serikali itayasimamia vizuri na inajiandaa kwa kushinda.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemshukuru Rais wa FIFA Bw. Infantino kwa niaba ya Rais Dkt John Magufuli kwa kuendesha mkutano mkubwa wa viongozi wa mpira wa miguu duniani Tanzania. Mkutano huo ulihusisha Marais na Makatibu Wakuu wa nchi 21.
Pia alimpongeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Bw. Ahmad Ahmad kwa jitihada zake za anazozifanya katika kuendeleza mpira barani Afrika na kwamba Serikali  ya Tanzania inamuunga mkono.
Rais wa FIFA Bw. Infantino ambaye ameahidi kuisaidia Tanzania kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo aliwasili nchini leo alfajiri akiongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Bw. Ahmad Ahmad kwa ajili ya mkutano wa FIFA uliofanyika nchini Tanzania February 22, 2018.

Bw. Infantino amewasili kwa mara ya kwanza Tanzania toka awe Rais wa  FIFA na alipokelewa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dtk. Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Leodger Tenga na Rais wa TFF  Bw. Wallace Karia.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.