Sunday, October 17, 2021

Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI yatembelea Mradi wa Timiza Malengo Iramba


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Fatma Taufiq (katikati) walipotembelea kuona utekelezaji  shughuli za mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na TACAIDS, tarehe 16 Oktoba, 2021 Wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida.

Na: Mwandishi Wetu - SINGIDA

Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI imefanya ziara ya kukagua utekeleaji wa shughuli za Mradi wa kinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, mradi wa Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) unaotekelezwa katika Wilaya ya Iramba mkoa wa Singida.

Kamati ilitembelea mradi huo tarehe 16 Oktoba, 2021 ili kujionea maendeleo ya mradi huo kwa lengo la kuona namna miradi inayotekelezwa na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

Mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na kutekelezwa na Serikali kupitia Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine kama TAMISEMI, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknoloji, Taasisi ya Elimu, Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) ,TASAF, AMREF na TAYOA.

Mradi huo umetekelezwa kwa muda wa miaka 3 tangu Januari 2018 hadi Disemba 2020 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na walengwa wakiwa wasichana balehe na wanawake vijana waliopo kwenye vijiji 50 vinavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Wilayani humo.

Hadi sasa mradi umeifikia mikoa mitano ya mfano ikiwemo; Morogoro, Dodoma, Singida, Geita na Tanga ambapo wamelenga kundi la wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walio ndani ya mfumo wa shule, kuendelea na masomo na kufikia ndoto zao wakiwa salama bila maambukizi ya VVU/ UKIMWI.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatma Taufiq akizungumza wakati wa kikao cha ufunguzi alisema ni muhimu kwa Serikali kuendelea kutoa elimu na kuyafikia makundi ya wasichana balehe kwa kuzingatia ndilo kundi lililo katika hatari ya kupata maambukuzi ya VVU huku akiwaasa vijana kuitumia miradi hiyo kama chachu kujikwamua kiuchumia na kutimiza ndoto zao huku wakichangia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Tumetembeela kuona jinsi Serikali inavyotekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kundi la vijana linalotajwa kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU na UKIMIMWI yanahudumiwa ipasavyo na kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya”

Aliongezea kuwa, miradi hiyo inapaswa kufanyika kwa usahihi ili kuwa na tija katika jamii zetu na kuhakikisha inakuwekewa mipango endelevu na kuifikia mikoa yote ili kuwa na vijana wenye kujitambua na kutimiza ndoto zao.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wasichana balehe na wanawake vijana kwa wingi kwa kuhakikisa mradi huu wa Timiza Malengo unafika katika mikoa yote nchini.

“Mradi huu umeanza katika mikoa hii mitano ya mfano, ni malengo kuwafikia vijana wetu wa Kitanzania ili waweze kupatia elimu itakayowasaidia kujitambua na kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwapekelea katika maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,”Alisema Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha jamii inabadili mitazamo kuhusu kundi hili la wasichana balehe na wanawake vijana ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili wajikwamue na kuinua wengine.

Aidha aliwaelekeza watendaji wa Wilaya ya hiyo  kuhakikisha wanakuwa na kanzi data ya wanufaika hao, kusaidia uendelevu wa programu na kuhakikisha waelimisha rika wanapatiwa ushirikiano wa kutosha ili wafikie kundi kubwa lililoachwa nyuma.

“Serikali imelilenga kundi hilo kwa kuzingatia  takwimu za mwaka  2017 ambapo zinaeleza vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 40 ya maambukizi mapya na kati yao asilimia 80 ni watoto wetu wa kike, hii ni dalili kwamba lazima mapambano haya yazidishwe katika makundi haya hatarishi”alisema Waziri Mhagama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Mwenda aliishukuru kamati hiyo kutembelea na kuona utekelezaji wa programu ya TIimiza Malengo na kuendelea kuahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maeneo yote muhimu yanayohusu mradi yanaendelea vyema huku akimshukuru Waziri Mhagama kwa kutoa kipaumbele kwa wilaya hiyo na kusema wataendelea kutunza kanzi data ya wanufaika wa mradi ili matunda yanayotokana na mradi huo yasipoteee.

“Wilaya itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha kunakuwa na bajeti ya kutosha katika kuyahudumia makubdi haya muhimu kwenye jamii,”alisema Mwenda.

Wakitoa shukrani na shuhuda zao tangu kuanza kwa mradi huo wanafunzi wa shule za  sekondari za Lulumba na New Kiomboi waliishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo huku wakisema umewawezesha kuongeza hali ya ufaulu, kujikimu kiuchumi na kupata mahitaji yao kwa wakati na kuwasaidia familia zao katika mahitaji mbalimbali.

AWALI

Mradi wa timiza Malengo unahusisha ugawaji wa taulo za kike kwa wasichana walio ndani ya mfumo wa shule, kugawa kondom na kufunga visanduku vya kondom  katika maeneo husika, kutoa elimu kwa viongozi wa dini kuhusu masuala ya UKIMWI, Utoaji wa mafunzo kuhusu uandaji wa mpango rahisi wa biashara na ujasiriamali, elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi au walezi wa wasichana, kuhamasisha wasichana kupima afya zao kwa hiari kupitia huduma ya mkoba na Vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao kupitia mabonanza, kuwawezesha wasichana kwa kuwapatia ujuzi wa jinsi ya kujikinga na maambukizi pamoja na kutoa elimu kwa njia ya simu kwa kupitia namba 117/15017- bure ambapo wanapokea na kupata fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.

Read More

Friday, October 15, 2021

Rais Samia Ahutubia Taifa kilele cha Mbio za Mwenge Chato

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akilihutubia Taifa kwenye kilele cha mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru Kitaifa mwaka 2021 zilizofanyika leo Oktoba 14,2021 katika Uwanja wa Magufuli Wilayani Chato Mkoani Geita.






Read More

Rais Mwinyi: Tuilinde Amani Iliyopo Nchini


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amewaasa Watanzania kuilinda amani iliyopo nchini ili Tanzania iendelee kuwa kitovu cha amani katika bara la Afrika na mfano wa kuigwa duniani.

Hayo ameyasema leo Oktoba 14, 2021, Chato mkoani Geita katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Bikira Maria, wakati alipokuwa akihutubia wakati wa  maadhimisho ya misa maalum ya kuwaombea Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Abeid Amani Karume, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli.

Pamoja na viongozi waliopo madarakani wakiongozwa na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

” Nawashukuru viongozi wetu wa dini na waumini mbalimbali kwa kushiriki katika tukio hili maalum kwa nchi yetu kwa kuzingatia kuwa viongozi wetu walijituma katika kuijenga nchi na sisi hatuna lolote la kuwalipa kwa kutufanya kuwa na Taifa lenye haki, usawa na uhuru, hivyo sisi hatuna budi kuwaombea ili wapumzike kwa amani”. Alisema Rais Mwinyi

Aidha, alisisitiza “Pia Watanzania tudumishe utaratibu huu wa maombi ili kuiombea nchi yetu, Tanzania ni mfano pekee wa kuigwa duniani kutokana na amani iliyopo hivyo hatuna budi kuilinda”.

Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Rulenge  Ngara, Severine  Niwemgizi alisema kuwa ni jambo jema na la hekima kwa viongozi kuanza na sala na maombi kabla ya kuadhimisha sherehe za kilele cha Mwenge.

“Namshukuru, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi na Serikali kwa ujumla kwa kutupa heshima ya kusali pamoja nasi asubuhi hii” alisema Askofu Niwemgizi

Aliongeza kuwa Watanzania waendelee kuwaombea viongozi waliotangulia mbele za haki na waliopo madarakani kwa kufanya matendo mema ambayo viongozi wamekua wakiwaasa.

Read More

Thursday, October 14, 2021

Serikali Kuendelea Kuimarisha Ushirikiano wa Kimataifa katika Usimamizi wa Maafa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na Vyombo vya Habari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa hii leo Oktoba 13, 2021 Chato, Mkoani Geita. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Col. Jimmy Matamwe. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Charles Msangi. 

Na: Mwandishi Wetu: CHATO 

Serikali kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa imeendelea kuimarisha ushirikiano katika kufanikisha hatua za usimamizi wa maafa nchini ikiwa ni moja ya mikakati ya kuepusha na kupunguza maafa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Chato mkoani Geita katika Maonesho ya Wiki ya Vijana,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa kwa lengo la kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa katika mifumo ya maisha, afya, uchumi, elimu, jamii, utamaduni, miundombinu na mazingira.

Alitaja tasisisi hizo za kuwa ni Taasisi za Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa, Nchi Washirika, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika.

Aidha, Mhe Waziri Jenista alisema “Serikali ya Awamu ya Sita kwa maono chanya ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza madhara ya maafa ikiwa ni njia muhimu ya kulinda maendeleo ya kisekta ili kufikia matokeo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na utekelezaji wa Makubaliano ya Paris katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi,” alieleza Waziri Mhagama

Alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imekuwa ikiadhimisha siku hii kila mwaka kwa ajili ya kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa na kitaifa, ili kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali katika ubora zaidi pale maafa yanapotokea.

Mhe. Waziri Mhagama, aliongeza kuwa  Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kuanzisha maghala ya kuhifadhi vifaa vya huduma za kibinadamu ambayo yapo kimkakati katika Kanda sita kwa ajili ya kurahisisha upatikananji wa huduma za kibinadamu pindi maafa yanapotokea kwa kushirikiana na kamati za maafa za Wilaya na Mikoa.

Pia, kupitia ushirikiano huo kimeanzishwa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura pamoja na vifaa na muongozo kwa ajili ya uendeshaji wake. Vilevile, vikundi vya wanawake, vijana na watoto katika shule vimekuwa vikiwezeshwa ili kuboresha mifumo ya maisha katika Wilaya ambazo zimekuwa zikiathirika na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Waziri Mhagama alieleleza kuwa Serikali imeandaa mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri 20 zilizoonekana kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na maafa mbalimbali.

Sambamba na hilo, Mhe. Waziri Mhagama, alieleza jitihada za Serikali katika kupunguza madhara ya maafa yanayoendelea kujitokeza ikiwemo changamoto ya kuibuka kwa hatari ya mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona – 19 (UVIKO-19).

“Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja baina ya nchi jirani, marafiki na taasisi za jumuiya ya kimataifa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa wakati huu na siku zijazo, hivyo Serikali imepokea na inaendelea kutekeleza programu ya chanjo kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu ambao ni hatari kwa maisha na kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa nchi yetu na dunia kwa ujumla,” alisema

Sambamba na hayo Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha sera, sheria na kuandaa mikakati kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa maafa nchini.

Pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na Uwanja wa Mazaina Chato mkoani Geita  ili kupata elimu ya kukabiliana na majanga na kupunguza athari za maafa inayotolewa na wataalamu wetu ili kulinda maisha, mali na uchumi wetu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Col. Jimmy Matamwe alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi zote ili kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na maafa  pale yanapotokea na pia kuzuia viashiria vyake.

Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ilitokana na Azimio Na. 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa tarehe 21 Desemba, 2009 ambapo iliamuliwa Oktoba 13 ya kila mwaka. Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa ikiwa na lengo la Kukuza utamaduni wa kupunguza madhara ya maafa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia, kujitayarisha, kukabili na kurejesha hali kuwa bora zaidi. Kaulimbili ya mwaka huu ni kwa umoja wetu… tunaweza kuokoa dunia

Read More

Idara ya Menejimenti ya Maafa yatoa Elimu ya kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa


 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alipotembelea banda la Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa Chato, Mkoani Geita.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda akipokea maelezo kutoka kwa Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji alipotembelea banda la Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa Chato, Mkoani Geita.


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Jamal Katundu akipokea maelezo kutoka Wataalam alipotembelea banda la Idara ya Menejimenti ya Maafa katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa Chato, Mkoani Geita.




Na: Mwandishi Wetu: CHATO

Idara ya Menejimenti ya Maafa imeshiriki maonesho ya wiki ya Vijana Kitaifa wilayani Chato, Mkoa wa Geita na kutoa elimu kwa wananchi ya kuzuia na kupunguza hatari na madhara ya maafa nchini.

Katika maonesho hayo Idara hiyo ilitembelewa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imekuwa ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kupunguza madhara ya maafa kila tarehe 13 Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kukuza utamaduni wa usimamizi wa maafa kimataifa na kitaifa, ili kuzuia na kupunguza madhara ya majanga pamoja na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali katika ubora zaidi pale maafa yanapotokea.

Aidha, Idara ya Menejimenti ya Maafa imetumia fursa ya maaonesho hayo kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya maafa na mikakati ya kuepusha na kupunguza maafa nchini.


Read More

Wednesday, October 13, 2021

Majaliwa Azuru Kaburi la Hayati Dkt. John Pombe Magufuli


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishirki katika sala fupi ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwenye kaburi la marehemu, wilayani Chato, Mkoani Geita, Oktoba 12, 2021. Kushoto ni Mama Janeth Magufuli na aliyepiga magoti  ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Read More

Majaliwa: Rais Samia atoa Shilingi Bilioni 28 Ujenzi wa Miradi ya Maendeleo Geita

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Kata ya Muganza, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, Oktoba 12, 2021.


Na: Mwandishi Wetu: CHATO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 28.6 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Geita.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika makazi yao.

Aliyasema hayo jana (Jumanne, Oktoba 12, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Muganza katika wilaya ya Chato mkoani Geita. Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 16 zimepelekwa wilayani Chato.

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mkoa wa Geita kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, elimu, barabara na afya zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali inaendelea kuajiri ili kuhakikisha lengo lake la kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi linafikiwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi RUWASA wilaya ya Chato uhakikishe kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kilichotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji zinatumika vizuri na wananchi wapate huduma hiyo.

 Mheshimiwa Majaliwa alitumia aliwaagiza viongozi hao wahakikishe wanaanza kufanya utafiti ili waweze kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa  kuyasambaza kwa wananchi. Alisema haiwezekani watu wanakaa karibu na ziwa na hawana maji ya kutosha.

Awali, Mbunge wa Chato Dkt Medrad Kalemani alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo kama ujenzi wa barabara, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, vituo vya afya pamoja na miradi ya maji.

Read More

Majaliwa: Vijana Jiepusheni na Matumizi Mabaya ya Tehama

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita.


Baadhi ya Wamanchi wakimsikikliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita  Oktoba 12, 2021. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama Katiba ya Jumuyia ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru (TAUTA) wakati alipozindua wiki ya vijana kitaifa, katika uwanja wa Mazaina, Wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

Na: Mwandishi Wetu: CHATO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi hususani vijana wajiepushe na matumizi yasiyo sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama vile wizi na utapeli wa fedha unaofanywa kwa njia ya mtandao.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa vijana nchini wajiepushe na matumizi mabaya ya TEHAMA kama kujiunga na makundi yasiyofaa, kujiingiza kwenye majukwaa ya uchochezi kwani vitendo hivyo vinavuruga amani, utulivu na mshikamano wa Taifa.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 12, 2021) alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa katika Viwanja vya Mazaina wilayani Chato, Geita yenye kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni Msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji.” Pia Waziri Mkuu amezindua Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Tanzania (TAUTA).

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza maadhimisho ya wiki ya Vijana Kitaifa na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru vifanyike katika wilaya ya Chato mkoani Geita ili kumuenzi Muasisi wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere ambaye alitoa mchango mkubwa katika kulikomboa Taifa letu akiwa kijana.  

Kutokana na umuhimu huo Serikali imesisitiza matumizi sahihi ya TEHAMA kwenu vijana kwani ninyi ndio watumiaji wakubwa na wahanga wakubwa wa TEHAMA. Ni ukweli usiopingika kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.”

“Vijana wengi wamefanikiwa kutokana na matumizi sahihi ya TEHAMA hususan kwa kufanya biashara kwa njia ya mtandao. Vijana wameweza kuanzisha na kuendesha vituo vya huduma za intaneti na pia kuanzisha wakala wa huduma za kifedha kupitia mitandao ya simu.”

“Hivyo, tukitumia fursa hizi vizuri na maendeleo ya TEHAMA tuliyonayo, tutasonga mbele kwa kazi kubwa zaidi. Tunayo mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, tumieni fursa hizo za mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya halmashauri zetu kuwekeza katika miradi yenye tija kwa maendeleo yenu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka vijana watumie fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira inayoikabili dunia kwa sasa. “Tanzania tunayo ardhi ya kutosha na yenye rutuba, tuna bahari, tuna maziwa na mito mikubwa, tunayo madini pia tunayo fursa ya uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza vijana watembelee kwa wingi banda la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Foundation) lililopo katika maonesho hayo ili wakajifunze kupitia historia ya baba wa Taifa umuhimu wao kama vijana wa Tanzania katika kujenga misingi ya uzalendo, uwajibikaji na ujenzi wa Taifa.

“Umuhimu wa kujua historia ni dhahiri kabisa kwani itaongeza ari ya uzalendo, kuipenda nchi yetu na kuimarisha muungano wetu ambao asili yake ni udugu wetu. Hii ni namna bora zaidi ya kumuenzi muasisi wa Taifa letu. Ama kwa hakika Kiongozi wetu huyo alikuwa ni mzalendo na muaminifu kwa Taifa.”

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo kuhifadhi kumbukumbu ya historia na kazi za Baba wa Taifa. “Maono yake, falsafa zake, uzalendo wake na bidii ya kazi aliyoifanya Baba wa Taifa kwa Taifa hili katika uhai wake vitaendelea kukumbukwa jana, leo, kesho na kila siku katika uhai wa dunia hii.”

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema katika wiki hiyo ya vijana kitaifa imewawezesha vijana kufanya tafakuri ya kina kuhusu falsafa juu ya maono ya Baba wa Taifa kupitia kazi alizozifanya kwa Watanzania,

Pia, amesema kuwamaadhimisho hayo yamewawezesha vijana kubadilishana uzoefu katika bidhaa na huduma za kiuchumi zinazotolewa na makundi mbalimbali ya vijana nchini. “Kupitia wiki hii tumewawezesha vijana kujitambua na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.”

Kwa upande wake, Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tabia Maulidi Mwita amesema kuwa Wizara hiyo itashirikiana na vijana wate nchini wakiwemo na walioshiriki katika maonesho hayo katika kuulinda na kuudumisha Muungano kwani una faida kubwa.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda amesema wiki ya vijana imeanzishwa kwa lengo la kuwakutanisha na kuwapa nafasi vijana na wadau wa shughuli za maendeleo yao na kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali yanayowahusu kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Amesema maadhimisho hayo ambayo yalianza Oktoba 8, 2021 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14 yamehudhuriwa na vijana zaidi 1.000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambao pamoja na mambo mengine wamepata mafunzo ya aina mbalimbali yakiwemo na ya matumizi bora ya TEHAMA.

Read More

Tuesday, October 12, 2021

Waziri Mkuu Majaliwa Awasili Chato Mkoani Geita


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule (wa pili kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye ulemavu Jenista Mhagama  (wa tatu kulia) na viongozi wengine alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Chato, Geita Oktoba 11, 2021 ambapo kesho anatarajia kuzindua wiki ya Vijana Kitaifa

Read More

Waziri Mhagama: Wananchi tambueni thamani ya Mwenge wa Uhuru

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Kilele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021 na kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Viwanja vya Mazaina Wilaya ya Chato mkoani Geita.


Na: Mwandishi Wetu - CHATO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka wananchi kutambua thamani ya Mwenge wa Uhuru na kushiriki shughuli ambazo umekuwa ukihamasisha.


Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Kilele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021 na kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Viwanja vya Mazaina Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Waziri alieleza kuwa, shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 Oktoba, 2021 katika Uwanja wa Magufuli Wilayani humo huku zikiwa zimebeba kaulimbi isemayo; “TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu; Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji

Waziri Mhagama alisema, Mwenge wa Uhuru na Mbio zake umeendelea kuwa muhimu kwa taifa hadi leo kwa kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi za kisiasa, dini wala makabila yetu.

“Umuhimu huu unatokana na ukweli kwamba, misingi hii tunahitaji leo na kesho kujenga kuliko wakati wowote ule ili tuweze kujenga taifa lisilokuwa na dhuluma, unyonge, rushwa, ubaguzi, ukabila, udini wala vitendo vya kifisadi”alisisitiza.

Aidha aliongezea kuwa Mbio hizo zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, uvuvi  endelevu, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za kijamii katika maeneo yote nchini.

“Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2010-2019, jumla ya miradi 14,145 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Trilioni 8.03 ilihamasishwa, iliwekewa mawe ya msingi, na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru,”alieleza.

Aliongezea kuwa, kwa miradi ambayo imebainika kuwa na mapungufu Serikali imekuwa ikichukuliwa hatua katika sekta mbalimbali ili kuendeleza jitihada za kujiletea maendeleo.

Akieleza sababu za Mbio hizo kuwa Maalum na kuhitimishwa Wilayani Chato alisema kwa mwaka huu ni sehemu ya historia muhimu kwa nchi yetu kwa kuendelea kuenzi mchango wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuendelea kutambua na kuenzi kwa matendo.

“Sote tunafahamu kuwa, Mwenge wa Uhuru mwaka huu unakimbizwa wakati Watanzania tukikumbuka kuondokewa na Kiongozi wetu mpendwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliyefariki akiwa madarakani, ndio maana kilele cha Mbio hizi kinafanyika Chato alikozaliwa ili kumuenzi,”alisema waziri Mhagama.

Aidha Mbio za Mwenge mwaka huu zinafanyika wakati Tanzania imeweka Historia mpya tangu Uhuru ya kuongozwa na Rais Mwanamke Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndio maana Mbio hizi zilizinduliwa Mkoani Kusini Unguja-Zanzibar alikozaliwa.

Alieleza mbio hizi zimekimbizwa katika Mikoa 31 na Wilaya za Kiutawala 150 tu badala ya kukimbizwa kwenye Halmashauri za Wilaya 195 kama ilivyozoeleka. Vilevile, Vijana sita wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wameteuliwa kutoka kwenye Jeshi letu la Wananchi Tanzania tu.

Kwa upande wake Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule aliwaasa Wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo na kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali huku wakiitumia wiki hii kama fursa katika mkoa.

Alisema mkoa umejipanga kuendelea kupokea viongozi mbalimbali watakao fika kwa ajili ya shughuli hiyo huku alieleza mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Tunashukuru mkoa kupata heshima hii, na niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi kujumuika katika kuifanikisha siku hii maalum huku mkiendeleza amani, umoja na mshikamano wenu”alisema Rosemary.

Read More

Monday, October 11, 2021

Vijana waaswa kuenzi Waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa Mdahalo wa Vijana Kitaifa ikiwa ni moja ya shughuli katika kuelekea kilele cha siku ya Vijana , Mdahalo huo ulifanyika katika Shule ya Sekondari ya Chato Oktoba 10, 2021 mkoani Geita.



Na: Mwandishi Wetu - CHATO

Vijana nchini waaswa kuenzi na kuishi fikra za waasisi wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume ili waweze kuwa wazalendo sambamba na kudumisha tunu za Taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza hayo wakati wa ufunguzi wa Mdahalo wa Vijana Kitaifa uliofanyika katika Shule Sekondari Chato mkoani Geita tarehe 10 Oktoba, 2021.

Waziri Mhagama alieleza kuwa tunazo sababu za msingi za kuwakumbuka waasisi wa taifa hili ambao ni Baba wa Taifa na mwasisi wa mapinduzi ya Zanzibar hasa kwa mchango wake mkubwa usio sahaulika kwa Taifa letu.

“Mchango huu wa waasisi wetu ni vyema urithishwe kwa vizazi vilivyopo hususan vijana na vizazi vijavyo ili waweze kuwa wazalendo kwa taifa lao na wakaziishi falsafa za viongozi hao,” alieleza Waziri Mhagama.

 Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake na Sheikh Abeid Aman Karume ili waendelee kujivunia juu ya misingi ya amani na umoja iliyopo nchini.

Aidha alifafanua kuwa, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kujenga umoja wa Kitaifa na kudumisha amani ya muda mrefu tuliyo nayo leo kama Taifa.

“Baba wa Taifa, aliasisi Mwenge wa Uhuru mwaka 1961 mara tu nchi yetu ilipopata Uhuru lengo lilikuwa ni kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chombo cha kuhamasisha ujenzi wa Taifa lenye watu wenye amani, lenye watu wenye upendo, lenye watu wenye matumaini na lenye watu wenye heshima,” alisema

Pamoja na hayo alisisitiza vijana na wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuendeleza maono ya waasisi wa taifa na kuleta mageuzi ya kiuchumi yenye manufaa kwa taifa.

Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo pia kuwahimiza wananchi na wakazi wa Chato kushiriki kwenye Maonesho ya Wiki ya Vijana ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Mazaina sambamba na kushiriki kwenye kilele cha Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika Uwanja wa Magufuli Chato Mkoani Geita tarehe 14 Oktoba, 2021.  

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule alisema kuwa ni vyema vijana wakatumia fursa ya mdahao huo ili waweze kutambua vyema historia ya Waasisi wa Taifa na kutambua maudhui ya Mwenge wa uhuru ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha watanzania na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii ili wajiletee maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa, Richard Jaba akitoa salamu wakati wa mdahalo huo alisema ni heshima kubwa kwa vijana kupata fursa za kujumuika pamoja na kueleza masuala yao huku akipongeza uamuzi ya kuleta shughuli hizo katika mkoa wa Geita na kuwaasa vijana kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuendelea chukangia katika kuleta maendeleo nchini.

“Kalenda ya chama inatambua uwepo wa wiki la vijana, hivyo tunaunga mkono kwa vitendo uwepo wa mdahalo huu na tutaendelea kutoa ushirikiano kwenu pia tunashukuru kuleta shughuli hizi Geita,”alisema Jaba 

Read More