Home
All posts
Saturday, February 17, 2018
WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI VIWANDA VYA LAKAIRO
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kuweka jiwe la viwanda vya Makampuni ya Lakairo Investment vyenye thamani ya sh. bilioni 25, ambavyo vipo katika kijiji cha Isangijo kata ya Kisesa wilayani Magu.
Ameweka jiwe la msingi la viwanda hivyo leo (Jumamosi, Februari 17, 2018) akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Viwanda hivyo vinatengeneza steel wire, pipi, vifungashio aina ya viroba
“Nampongeza Bw. Lameck Airo mbunge wa Rorya na Mwenyekiti wa Makampuni ya Lakairo Investment kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi kupitia sekta viwanda.”
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda na inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika viwanda mbalimbali.
Amesema Serikali itamuunga Bw. Airo mkono ili viwanda hivyo viweze kuzalisha kwa mafanikio makubwa. Pia aliwataka wananchi nao wamuunge mkono muwekezaji huyo kwa sababu viwanda hivyo vinazalisha bidhaa muhimu na kutoa ajira kwa wananchi wengi.
Pia amewaagiza viongozi wa mkoa na halmashauri wahakikishe wanatoa kipaumbe kwa wawekezaji kwa kuwasogezea miundombinu ya huduma mbalimbali zikiwemo za maji na umeme ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Lakairo Investment, Bw. Daniel Lameck alisema mbali na ujenzi wa viwanda hivyo vinavyotarajiwa kutoa ajira 200 hadi 300, pia wanatarajia kujenga viwanda vingine vya kutengeneza mafuta ya kupaka, dawa za viatu na kusaga nafaka.
Bw. Lameck alisema mbali na mafanikio wanayoyapata pia wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa fedha kwa ajiali ya uwekezaji, ambapo alitolea mfano mpango wao wa kutaka kujenga viwanda vingine viwili ambao umekwama kutokana na upatikanaji wa fedha.
Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuishauri Serikali iweke mfumo rafiki kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji wa ndani ili viwanda wanavyovianzisha viwe endelevu na vipanuke zaidi.
Friday, February 16, 2018
MAJALIWA AKAGUA MASHAMBA BORA YA PAMBA KATIKA VIJIJI VYA KILYABOYA NA SOLWE WILAYANI KWIMBA
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua shamba la pamba la Bw. Dotto Masomi (kushoto) katika kijiji cha Solwe wilayani Kwimba Februari 16, 2018, Kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Kwimba Mtemi Simon Msafiri. |
WANANCHI WAMKATAA MKUU WA WILAYA MBELE YA WAZIRI MKUU
Wametoa ombi hilo leo (Ijumaa, Februari 16,
2018) walipozuia msafara wa Waziri Mkuu alipowasili katika Ofisi za Halmashauri
ya wilaya Kwimba zilizopo Ngudu kwa ajili ya kuzungumza na watumishi akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Wananchi
hao walimkataa mkuu wao wa wilaya Bw. Msafiri kupitia ujumbe wa mabango 17,
ambapo Waziri Mkuu amewataka wananchi hao wawe watulivu wakati Serikali
inafanyia kazi malalamiko yao.
Wananchi
hao wanadai kwamba Mkuu huyo wa Wilaya anatabia ya kuamrisha polisi wawakamate
kwa kisingizio cha uzururaji na kisha wanawekwa mahabusu, ambapo baada ya muda
wanatolewa na kwenda kulima kwenye shamba lake.
Waziri Mkuu
amesema Serikali inahitaji kila mtumishi atambue majukumu yake na ayatekeleze.
“Hakuna atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza nanyi mnatakiwa kutenda
haki kwa kuwatumikia wananchi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mkuu huyo wa wilaya Bw. Msafiri,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba Bibi Pendo Malebeja na
wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli wanatekeleza majukumu yao ipasavyo
na kuwatumikia wananchi.
“Mkurugenzi katika kipindi chako chote cha utendaji kuanzia
mwaka 2013 hadi leo, fedha nyingi za Serikali zilizoletwa Kwimba zimepotea na
hazijulikani zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika na muda wote huo
Halmashauri imekuwa inapata hati chafu.”
Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya
wilaya ya Kwimba wabadilishe mienendo yao na wawatumikie vizuri wananchi pamoja
na kuishi nao vizuri.
ZIARA YA MAJALIWA WILAYANI KWIMBA
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimtwika ndoo ya maji, Esther Balele baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa kijiji cha Igumambogo wilayani Kwimba Februari 16, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimtwika ndoo ya maji , Scolastica Odiria baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa kijiji cha Igumambogo wilayani Kwimba Februari 16, 2018. |
WAZIRI MKUU AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI WA KAMPUNI YA PALIMON
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU
mkoa wa Mwanza Mhandisi Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya
Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa mradi wa maji wenye thamani ya
sh. bilioni 2.06 wilayani Kwimba.
Ametoa agizo leo (Ijumaa, Februari 16, 2018) wakati akizungumza
na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba.
Mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha
Mei 28, 2014.
Waziri Mkuu amesema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha
mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo amemtaka kamanda
wa TAKUKURU kutafuta popote alipo na kumuhoji.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya wananchi wa vijiji
vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji
vyao. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na
wao wapate huduma ya maji.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya
maendeleo kulipana posho.
“Fedha zinazopelekwa si za kulipana posho ni za maboresho na
Serikali inataka wananchi wahudumiwe wasipate shida.”
Waziri Mkuu amesema watumishi wahakikishe wanawahudumia
wananchi ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za
maendeleo.
Amesema wilaya hiyo imegeuka kama shimo la kuteketeza fedha
za Serikali kwa sababu miradi mingi inayotekelezwa haikamili, hivyo ameitaka
ijipange. Alitolea mfano sh. milioni 94 za ujenzi wa mradi wa kliniki ya mifugo
ambayo haijakamilika na fedha zimekwisha.
Awali, Waziri Mkuu alifungua mradi wa maji
wa kijiji cha Igumangobo kilichopo katika Tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba.
Chanzo cha maji hayo ni ziwa Victoria.
WAZIRI MKUU AKEMEA VITENDO VINAVYOHARIBU UBORA WA PAMBA
*Awataka wasiweke
mchanga wala maji ili kuongeza uzito
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewataka wakulima wa pamba kutochanganya pamba na mchanga au maji kwa
sababu watakosa wanunuzi.
Pia amesema Serikali
itapambana na watu wote wanaotaka kuvuruga zao hilo, hivyo amewataka wakulima waendelee
kuwa na imani na Serikali yao.
Waziri mkuu alitoa
kauli hiyo jana (Ijumaa, Februari 16, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi wa wilaya ya Kwimba.
“Wakulima msichezee
pamba kwa kuichanganya na chochote ili kuiongezea uzito kwa sababu mtaharibu sifa
nzuri ya pamba ya Tanzania ndani nan je ya nchi.”
Alisema kumekuwa na
tabia ya baadhi ya wakulima wasiokuwa waaminifu ambao kabla ya kuipeleka pamba sokoni
wanachanganya na maji au mchanga.
Waziri Mkuu alisema Serikali
imeanza kuona tija tangu ilipoagiza Maofisa Kilimo katika mikoa inayolima pamba
wasimamie kilimo hicho kuanzia ngazi za awali.
Akizungumzia kuhusu suala la wanunuzi wa pamba, Waziri Mkuu alisema
tayari Serikali imeweka
mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote kununuliwa.
Kuhusu suala la bei alisema
wataangalia katika soko la Dunia na kisha watawashawishi wanunuzi wanunue kwa bei
nzuri itakayowanufaisha wakulima.
Alisema
Serikali itaendelea kusimamia zao hilo kuanzia hatua za maandalizi ya shamba
kwa kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko.
Awali,
Waziri Mkuu alitembelea mashamba ya mfano ya pamba katika kijiji cha Kilyaboya
na Igumangobo ambapo alisema ameridhishwa mashamba hayo.
Pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi
wa zahanati ya kijiji cha Kadashi, mradi ambao ulioibuliwa na Diwani wa Kata ya
Maligisu, Bw. Tabu Mapembe.
Kata ya Maligisu yenye vijiji vine
ina zahanati moja tu, kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutasaidia
kupunguza tatizo la utoaji wa huduma za afya.
IDARA YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI YAENDESHA KIKAO CHA TATHIMINI NA UFUATILIAJI JUU YA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.
Thursday, February 15, 2018
WATENDAJI TENGENI MUDA WA KUWAHUDUMIA WANANCHI-MAJALIWA
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa Buchosa wakati alipoingia kwenye uwanja wa michezo wa Nyehunge wilayani Sengerema kuhutubia mkutano wa hadhara Februari 15, 2018. |
| Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa Buchosa wakati alipoingia kwenye uwanja wa michezo wa Nyehunge wilayani Sengerema kuhutubia mkutano wa hadhara Februari 15, 2018. |
Na mwandishi wetu |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji na wakuu wa
idara mbalimbali kuhakikisha wanatenga muda na kwenda vijijini kuwahudumia
wananchi.
Amesema wananchi hususani waishio maeneo ya vijijini
wanachangamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi na watendaji hao.
Aliyasema hayo jana (Alhamisi, Februari 15, 2018)
alipozungumza kwa nyakati tofauti na watumishi na wananchi katika kata ya
Nyehunge na Ibisabageni wilayani Sengerema akiwa katika ziara ya mkoa wa
Mwanza.
Alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa lengo
la kuwaondolea kero mbalimbali zinazowakabili, hivyo hakuna sababu ya watendaji
kukaa maofisini.
“Watumishi wanawajibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo
yao hasa vijijini kwa sababu si kila mwananchi anauwezo wa kufuata huduma
katika ofisi zenu na atakayeshindwa kufanya hivyo hatutomvumilia.”
Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali inawawezesha watumishi
wake kwa kuwapatia vitendea kazi kama usafiri ili waweze kuwahudumia wananchi
ipasavyo.
Alisema kwa sababu ya kutotekeleza wajibu wao ipasavyo
kumekuwa na kero na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na hivyo kusababisha
wananchi kuwasilisha kero na malalamiko hayo wakati wa ziara za viongozi wakuu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wananchi
wanaofanya kazi katika kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao ya nafaka cha Doto
Alex Posho Meel kuwa waaminifu.
Waziri Mkuu alisema wafanyakazi hao wanatakiwa wawe
waaminifu na wafanye kazi kwa bidii ili kukiwezesha kiwanda hicho kuendelea na
uzalishaji.
MADIWANI WA BUCHOSA WAMKATAA MKURUGENZI WAO MBELE YA WAZIRI MKUU
MADIWANI wa
Halmashauri ya Buchosa wilayani
Sengerema wamemuomba Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aondoke na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,
Bw. Cyprian Luanda baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Wametoa ombi hilo leo (Alhamisi, Februari 15,
2018) katika kikao cha Waziri Mkuu na watumishi Halmashauri ya Buchosa akiwa
katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu baada ya kupokea ombi hilo
alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella kwenda katika halmashauri
hiyo na kufanya kikao cha pamoja kati ya Madiwani, Mkurugenzi na watumishi ili
kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.
Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la hospitali ya Halmashauri ya
Buchosa wilayani Sengerema, ambapo ujenzi wake hadi kukamilika unatarajiwa
kugharimu sh. bilioni 10.55.
Pia Waziri Mkuu amezindua madarasa manne ya
Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Secondari ya Nyehunge
wilayani Sengerema na kuwata wanafunzi wasome kwa bidii.
Waziri Mkuu amesema wanafunzi hao wanatakiwa
wasome sana kwa sababu Rais Dkt. John Magufuli amewaondolea wazazi
michango ya hovyo ili wao wapate fursa ya kusoma.
Pia amewasisitiza walimu wasijiingize katika
masuala ya michango ili wajikite na masuala ya taaluma. Kama kuna
michango kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi yote sasa itafikishwa kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri.
Amesema awali wanafunzi walikuwa wanatumika kama
njia ya kutengeneza fedha, ambapo wazazi au walezi wanaposhindwa kutoa michango
hiyo watoto wao walikuwa wanarudishwa nyumbani. Waziri Mkuu amesema kila
mwezi Serikali inapeleka moja kwa moja shuleni sh. bilioni 20.8 kwa ajili ya
kugharamia Elimumsingi bila malipo.
MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI LA HOSPITALI YA HALMASHAURI YA BUCHOSA
Tuesday, February 13, 2018
WAZIRI MKUU AZINDUA MPANGO MKAKATI WA AFYA MOJA
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13, 2018) wakati akizindua mpango mkakati huo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, ambapo amesema dhana ya Afya Moja inafaa kutumika zaidi katika nchi zinazoendelea.
Waziri Mkuu amesema mbali na mpango kufaa kutumika katika nchi zinazoendelea pia hata kwa nchi zinazokaribia maeneo ya wanyama pori kama Tanzania kutokana na kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa rasilimali.
Amesema kwa upande wa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuwa Bara hilo, lina sehemu nyingi zinazokaribia mapori makubwa ya wanyama kama Bonde la Mto Kongo, ambalo mazingira yake yamekuwa ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Marburg na mengineyo.
Waziri Mkuu amesema kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na wadau wengine wa Maendeleo, imeendelea kutekeleza agenda ya Afya Moja nchini tangu mwaka 2013 ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza mjini Arusha na Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
“Utekelezaji wa Mpango huu unakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2015-2020) ya kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora itakayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali ambayo ni muhimu sana katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda.”
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama alisema uzinduzi wa mkakati huo ni ngao tosha kwa nchi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa.
Alisema pamoja na kutekeleza kanuni za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ambazo zinahitaji ushirikiano wa sekta mbalilmbali kwa kutumia dhana ya afya moja, mpango mkakati huo unaleta msukumo katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali kudhibiti magonjwa.
Bibi Jenista alisema uratibu wa afya moja unakwenda sambamba na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (IOE) na Shirika la Kimataifa la Chakula la Kilimo (FAO) ambayo yanashirikiana katika kudhibiti magonjwa yanayoambukiza na usugu wa dawa.
BAHARI KUU, VIWANJA VYA NDEGE VYABAINIKA KUPITISHA DAWA ZA KULEVYA-MAJALIWA
WAZIRI MKUU AKABIDHI GARI KWA MAMLAKA YA KUPAMBAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Friday, February 9, 2018
WAZIRI MKUU KUZINDUA MPANGO MKAKATI WA AFYA MOJA NA DAWATI LA URATIBU AFYA MOJA NCHINI
![]() |
| "Afya moja ni dhana inayojumuisha sekta ya binadamu,wanyama pori na wafugwao na mazingira katika kujiandaa,kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri sekta hizo " |
SERIKALI YAFANIKIWA KUREJESHA MALI ZA NCU, SHIRECU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kurejesha mali tisa kati ya 10 za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambazo zilichukuliwa kinyume cha taratibu na kuagiza watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.
Amesema mali moja iliyobakia bado inafanyiwa uchunguzi na mali mbili za Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) nazo pia zimepatikana lakini bado ziko kwenye hatua ya makabidhiano.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
Waziri Mkuu amezitaja mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) zilizorejeshwa kuwa jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd. maarufu kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa wa Stesheni; kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil Mill, kilichopo katika eneo la Igogo; na jengo na viwanja vya Ashock Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.
Nyingine ni majengo ya kilichokuwa kiwanda cha mkonge na dengu kilichopo eneo la Igogo kwenye kiwanja namba 41 na 79; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 80, kitalu “D”; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 110, kitalu “D” na ghala moja katika kiwanja namba 104, kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo.
“Mali nyingine zilizorejeshwa ni jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja namba 8 Kitalu “K”; jengo moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja namba 24, Kitalu “K” na jengo lililopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”,” amesema Waziri Mkuu.
Kwa upande wa mali za SHIRECU, Waziri Mkuu amezitaja mali zilizopo kwenye hatua ya makabidhiano kuwa ni ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya ghorofa tatu iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, jijini Dar es Salaam.
“Katika kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa vyama vya ushirika, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu mikataba mibovu ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU). Vilevile, tunachunguza kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vilivyosinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara na kwamba juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri wenyewe katika sekta ya kilimo.
VIWANJA ZAIDI YA 15,000 VIMEPIMWA DODOMA- MAJALIWA
*Kuanza kuuzwa Machi 30, mwaka huu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Dodoma imekamilisha upimaji wa viwanja vipya zaidi ya 15,000 na vitaanza kugawiwa Machi, 30 mwaka huu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.
“Kutokana na agizo la Serikali la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, mahitaji ya viwanja hadi Februari 2018 yalikuwa ni viwanja 24,602.Manispaa ya Dodoma hivi sasa inatekeleza mkakati wake wa kuzalisha viwanja 30,000 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Tayari upimaji wa viwanja vipya 15,316 umekamilika na vitaanza kugawiwa kuanzia tarehe 30 Machi 2018,” amesema Waziri Mkuu.
Amelieleza Bunge kwamba kiasi kilichobaki cha viwanja 14,684 kitakamilika ifikapo Juni, 2018 na wananchi watauziwa viwanja hivyo kwa bei elekezi itakayotolewa na Manispaa hiyo.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi na watumishi wa umma watakaohitaji viwanja kufuata taratibu za maombi ya viwanja pindi vitakapotangazwa rasmi na kusisitiza kuwa zoezi la kubadilisha hati zilizotolewa na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kupata hatimiliki za miaka 99 linaendelea. “Wenye hati za CDA mnasisitizwa kuendelea na taratibu za kuzibadilisha,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema jumla ya watumishi 3,829 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali tayari wamehamia Dodoma akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ofisi yake walihamia rasmi Dodoma tarehe 15 Desemba, 2017 kama ilivyopangwa,” amesema.
Kuhusu mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kuifanya Dodoma iwe na ukanda wa kijani (Green Belt) kupitia mpango wa kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya msitu wa Mahomanyika wenye ukubwa wa hekta 2,000; msitu wa Chimwaga Nzuguni (hekta 300) na msitu wa Mbwenzelo (hekta 3,500) pamoja na vilima vya Image na Nyankali.
“Katika kutimiza malengo hayo ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, Serikali imeendelea kutoa elimu ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu hususan miti adimu ya asili na makao ya wanyamapori mbalimbali katika kata nane za Ipala, Nzuguni, Kikombo, Ng’ong’ona, Chahwa, Zuzu, Hombolo na Kikuyu Kaskazini ambapo kila kata imepewa lengo la kupanda miti isiyopungua 40,000,” amesema.
Kuhusu zoezi la upandaji miti, Waziri Mkuu amesema miche 34,000 yenye thamani ya sh. milioni 34 ilitolewa bure katika kata mbalimbali na kupitia mradi wa TASAF miche mingine 138,000 inaendelea kusambazwa kwa wananchi. “Kwa sasa, Manispaa ya Dodoma inaendelea na maandalizi ya kuotesha miche mingine 200,000 kwa ajili ya msimu ujao,” ameongeza.
Ametumia fursa hiyo kuwashukuru Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bonde la Wami Ruvu, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma wamefanikisha upandaji wa miche 79,000 katika maeneo ya UDOM, Mzakwe, Iseni Park, Nala na Mahomanyika.
Katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinaandaa miche ya kutosha na kuweka utaratibu wa kila kaya kupanda na kutunza miti isiyopungua mitano.
“Taarifa za utendaji na maendeleo za Halmashauri zote zioneshe mafanikio yaliyopatikana kutokana na zoezi la upandaji miti. Utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, utapimwa kutokana na uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao,” amesisitiza.
Subscribe to:
Posts (Atom)
MITANDAO YA KIJAMII
Popular Posts
-
Na. OWM, Dodoma. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, imefanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 y...
-
Wataalamu wa Afya moja wakiwa katikapicha ya pamoja wakati wa mkutano wa wataalamu wa Afya moja uliojikita katika ulinzi na usalama...
-
Na. OWM, ARUSHA Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri...
-
Washiriki wa Mkutano wa mwaka wa Wataalamu wa Maabara wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara w...
-
TAMOBA wafanya wasilisho la mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama wa Bodaboda na BajajiKampuni ya Tanzania Motorcycle and Bajaj Association (TAMOBA) imefanya wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa ...
-
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia sukari, alipotembelea kiwanda cha Kilombero Sugar, kilichopo katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Mo...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ambaye ndiye anayesimamia Kamati ina...
-
*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sik...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo ya namna mashine zinavyochakata mifuko chakavu na ...
-
Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu H...
Formulir Kontak
Contributors
Powered by Blogger.






