Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya
Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Mololo Noah
akiongoza kikao cha Kuthibitisha Muongozo wa Utekelezaji wa dhana
ya Afya Moja. Kikao hiki kilihusisha washiriki kutoka sekta ya Afya, Mifugo,
Mazingira, Wanyamapori, BAKITA na mashirika ya Umoja wa Kimataifa. Kikao
kilifanyika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya regency Mkoani Singida
Tuesday, June 27, 2023
MUONGOZO WA UTEKELEZAJI WA DHANA YA AFYA MOJA WAJADILIWA
Saturday, June 24, 2023
KATIBU MKUU DKT. YONAZI AHIMIZA WATUMISHI KUWA NA TABIA YA KUPIMA AFYA .
Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu amewakumbusha
watumishi wa ofisi yake kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara
ili kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuyafikia
malengo ya Serikali.
Ametoa kauli hiyo
wakati akifungua kikao chake na watumishi wa ofisi hiyo kilichofanyika Jijini
Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu huyo
amesema upo umuhimu wa kujizoeza kupima afya hususan kwa magonjwa sugu
yasiyoambuiza kwani yameendelea kuwa changamoto hasa kwa watu wenye umri
mkubwa.
“Ni muhimu tumepata
fursa ya kukumbushwa kupima afya zetu, hii ni changamoto inayotukabili, hivyo
ni muhimu kuzingatia ushauri wa afya na masharti ya namna ya kuboresha masuala
yanayohusu afya zetu, “alisema Dkt. Yonazi
Pamoja na hilo
aliwakumbusha watumishi kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuendelea
kutekeleza majukumu wakiwa wenye afya na kuwa na matokeo chanya.
Aidha aliutumia
mkutano huo kuwaasa watumishi hao kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu
yao ya kila siku huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa
umma.
“Mkutano huu ni sehemu
ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo tulianza kuiadhimisha tarehe
16 Juni, 2023 na leo ndio kilele.Wiki hii tunaitumia kutafakari namna
tunavyotekeleza majukumu yetu kwa kipindi kilichopita, kujadili namna ya kutoa
huduma bora kwa jamii ya Watanzania, kujifunza mbinu mpya na kuibua changamoto
zinazotukabili katika kutekeleza majukumu yetu kwa lengo la kuzitafutia
ufumbuzi,”alisisitiza
Pia aliwahimiza
Watumishi kuendela kufanya kazi kwa upendo na kuheshimiana kwani kwa kufanya
hivyo wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa amani.
“Ni falsafa yangu
kuona watu ninaowaongoza wanafanya kazi kwa upendo na kushirikiana, ni lazima
kuhusiana na kuwa na mashirikiano mazuri, napenda kufanya kazi na watu
wanaoheshimiana na wenye amani siamini kama mtu anaweza akafiri vizuri iwapo
hana amani ndani”alisisitiza Dkt. Yonazi
Akitoa neno la shukrani
Mwenyekiti ya TUGHE wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Numpe Mwambenja alipongeza
uwepo wa mkutano huo huku akieleza kuwa ni nyenzo muhimu kwa kuongeza motisha
kwa watumishi wa umma, na imeonesha kujali na kuendelea kuleta umoja kazini.
“Mkutano huu umekuja
wakati sahihi na muda sahihi, tunawapongeza viongozi wetu kuendelea kutuweka
pamoja na kutukumbusha kupendana, kushirikiana na kuishi kwa amani, hili
tumelithamini sana na tunaahidi hatuta waangusha tutachapa kazi na kuendele
kuhudumia jamii ya Watanzania na kuitumikia nchi yetu kwa ujumla,”alisema
Numpe.
Tuesday, June 13, 2023
MEJA JENERALI MBUGE “TUIMARISHE USHIRIKIANO KUKABILI MAJANGA”
Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha
ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha
wananchi wanaishi katika mazingira salama.
Kauli hiyo imetolewa
Mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua
kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo
wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.
Meja Jenerali Mbuge
amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwingiliano wa binadamu, wanyama na
mazingira ambao husababisha kutokea kwa magonjwa mbalimbali
yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya
kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia
na kukabiliana na majanga hayo.
“Tunahuisha mwongozo
huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usimamizi wa
Maafa. Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa
kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya
magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na
mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.
Ameongeza kuwa kwa
mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa husisitiza yakiwemo Shirika la
Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni
(WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu
ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta
mbalimbali ili kuwa na mikakati na sera za pamoja katika kuimarisha
afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.
“Ili kutekeleza dhana
ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na
utendaji katika ngazi zote. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao
walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki
utauhuishwa na kutafsiriwa,” Ameeleza.
Aidha amebainisha kuwa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina
wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya Afya Moja kwa kuzingatia
Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.
6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja
2022-2027.
Thursday, May 25, 2023
SERIKALI KUZINGATIA MAFUNGU MAALUM YA FEDHA KWA WAVIU KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2023/24
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amesema utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na vipaombele vingine inazingatia pia mafungu ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) katika kila Wizara na Taasisi.
Ameyasema hayo mapema katika Ukumbi wa Waziri Mkuu Bungeni Dodoma alipokutana na kufanya
mazungumzo na Uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI
(NACOPHA).
Mhe. Mhagama, aliendelea
kusema kuwa hii ni namna ambavyo Serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kwa dhati kusaidia
utekelezaji wa Afua za masuala ya UKIMWI nchini, kwa kuzingatia maeneo muhimu
ikiwemo masuala ya lishe bora, dawa za kupunguza makali ya virusi na
kuhakikisha mambo mengine yanayochangia ustawi wao kupatikana.
Akizungumzia suala la Sera ya
Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 Mhe. Mhagama alisema kuwa kuna kila Sababu ya
Sera hiyo kufanyiwa mapitio na maboresho kwani ni ya muda mrefu na kuona, namna
gani sekta zote zinaweza kushiriki katika suala hili ili kuweza kuyafikia
malengo ya dunia ya kupunguza vifo, maambukizi na unyanyapaa ifikikapo 2030.”
Niwahakikishie kwamba sisi kama Serikali tunaweza kusimamia kufikia malengo
haya ya dunia”Alisisitiza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
NACOPHA Mwalimu Leticia Mourice alimpongeza Mhe. Waziri Jenista kwa uteuzi wake
na pia kumshukuru kwa juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI,
aidha aligusia kuhusiana na maandalizi ya Mdahalo wa Kitaifa kuhusu uhimilivu
wa mwitikio wa jamii katika mwitikio wa Taifa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Sambamba na hilo alizungumzia
kuhusu, uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Taifa, ambao unalenga utekelezaji wa
NMSF5 (Mpango Mkakati wa Tano wa Kitaifa wa Kudhibiti UKIMWI) na alisisitizia umuhimu
wa ushirikiano, katika kujenga mwitikio wa kijamii katika mapambano dhidi ya
UKIMWI, akitolea mfano maeneo kadhaa muhimu ikiwemo Uhimilivu wa Kisera.
Awali, akizungumza katika
mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA Bw. Deogratius Rutatwa, aliishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuipongeza Serikali ya watu wa
Marekeni (PEPFAR/USAID) kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha shughuli za
mwitikio wa UKIMWI za NACOPHA na wadau wote wanaotekeleza suala la UKIMWI na
kusema kuwa kuna haja ya kuwepo kwa mkakati endelevu na uhimilivu.
Wednesday, May 17, 2023
WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 27
Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Dkt Selemani Jafo wakati wa Bunge la 12 Mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti linaloendelea Jijini Dodoma.
NAIBU WAZIRI NDERIANANGA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 27
Saturday, May 13, 2023
WILAYA YA IGUNGA KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI. AFDP
Halmashauri ya Wilaya ya
IGUNGA iliyopo Mkoani Tabora imetajwa kuwa miongoni mwa Wilaya nchini
itakayonufaika na programu ya kuendeleza Kilimo na uvuvi (AFDP) inayofadhiliwa
na Mfuko wa Kimataifa wa kuendeleza Kilimo IFAD.
Hayo yameelezwa mapema leo na
Mratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Bw.
Salim Mwinjaka alipokuwa na mazungumzo na kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya IGUNGA, wataalam pamoja na ujumbe kutoka AFDP ulipokuwa katika ziara
ya kikazi ya kutembelea maeneo yatakayoteleza programu hiyo.
Bw. Mwinjaka alisema kuwa
Wilaya ya IGUNGA ni miongoni mwa Wilaya itakayopata fedha za utekelezaji
wa programu hiyo kupitia wizara ya
Kilimo Kwa mwaka wa fedha 2324, "na Kwa mwaka wa fedha unaofuata Kwa
kuzingatia maandali ya Mpango wa mapato na matumizi ya bajeti kuwekwa vizuri,
fedha hizo zitakuja Moja Kwa Moja katika Wilaya husika."Alifafanua
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa
ushirika wa umoja wa wafugaji wa samaki Igunga (UWASAI) uliopo katika kata ya
Mwamapuli Bw. Francis Mgaragu, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na
Uvuvi chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Kwa
kuwaletea mradi huo "mradi tumeupokea Kwa mikono miwili tunahaidi
ushirikiano, na tunahaidi kuwa tutatekeleza mradi Kwa malengo
yaliyokusudiwa." Alisema
Friday, May 12, 2023
MRADI WA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI KUTATUA CHANGAMOTO ZA UFUGAJI VIUMBEMAJI CHATO.
Imeelezwa kuwa Mradi wa
kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unakwenda kutatua changamoto wanazokumbana
nazo wafugaji VIUMBEMAJI katika kituo Cha Rubambagwe kilichopo Wilayani
Chato,mkoani Geita.
Hayo yameelezwa Leo na Dkt.
Nazaeli Madala, Mkurugenzi wa ukuzaji viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi.
Dkt. amesema kituo Cha Rubambagwe kipo katika UJENZI
ambapo, Nia na madhuni ya kituo hiki ni kuhamasisha, kuendeleza na kusimamia
ukuzaji viumbe Maji,Kwa maana Ufugaji wa samaki kwa mabwawa na vizimba katika
ukanda wa ziwa Victoria.
Alisema kuwa, kituo kitakwenda
kutoa mafunzo ya utengenezaji wa chakula cha samaki,Ufugaji na ulishaji sahihi
wa samaki, wafugaji watafundishwa pia namna ya kutengeneza chakula Cha samaki
Kwa kutumia malighafi za asili, kutakuwa na majengo ambayo yatawezesha wafugaji
wanaotoka mbali kukaa hapo wakati wa mafunzo, sambamba na hilo, kutakuwa na
kiwanda kidogo Cha kutengeneza chakula cha samaki.
Aliongeza kusema kuwa kituo
pia kitazalisha vifaranga vya samaki ili kuweza kutatua changamoto ambazo
wafugaji wanakutana nazo "kutakuwa na kitotoleshi ambacho kitakuwa na uwezo
mkubwa sana wa kuzalisha vifaranga ambavyo vitakwenda kuwezesha vitotoleshi vya
sekta binafsi kupata wazazi "Alifafanua
Akiongea na ujumbe huo, Bi.
Sifa Buguni mmoja wa wafugaji wa samaki
Rubambagwe Chato alibainisha changamoto kubwa mbili walizokumbana nazo kabla ya mradi huu
kukamilika kuwa ni pamoja na uhaba wa upatikanaji wa mbegu na chakula cha
kulisha samaki.
Awali, ujumbe huu wa IFAD
ulifika ofisini Kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara
ambapo alisema ni wakati sasa kwa wakazi wa Mkoa wa Geita kujikita katika
katika shughuli za kilimo na ufugaji wa viumbemaji na kwa uwekezaji wa uhakika
kuweza kuwekeza katika sekta hizo kama wanavyowekeza katika sekta ya madini.
Ujumbe kutoka IFAD, wataalam
na Mratibu wa Programu hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu
Bw. Salim Mwinjaka wapo katika ziara ya ukaguzi wa maeneo yanayotekelezwa mradi
huo
Thursday, May 11, 2023
PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI ITACHANGIA KULETA UHAKIKA NA USALAMA WA CHAKULA NCHINI - DKT. BATILDA
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe.
Balozi Dkt. Batilda Buriani amesema, Programu ya AFDP itasaidia upatikanaji wa
mbegu za mazao zinazoweza kuhimili na kukabiliana na athari zitokanazo na
mabadiliko ya tabianchi. Aidha mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa Programu ya kuendeleza
Kilimo na Uvuvi nchini AFDP italeta uhakika wa usalama wa Chakula upatikanaji
wa ajira katika maeneo inapotekelezwa programu hiyo, pamoja na kuinua pato la
mwananchi mmoja mmoja na Taifa Kwa ujumla.
Mheshimiwa Balozi Dkt. Batilda
ameyasema hayo mapema alipokutana na ujumbe kutoka IFAD walipokuwa katika ziara
ya Usimamizi wa utekelezaji wa programu hiyo ya kuendeleza Kilimo na uvuvi
(AFDP).
Akielezea kuhusu sekta za
kilimo na ufugaji Mheshimiwa Balozi Dkt Batilda ameelezakuwa mkoa wa Tabora ni
maarufu kwa kilimo Cha zao la Tumbaku na Ufugaji wa nyuki.
Kwa Upande wake mtaalamu wa
Tathmini na Ufuatiliaji wa programu hiyo Bw. Bernard Ulaya akielezea utekelezaji wa Programu hiyo mkoani
Tabora, programu hiyo ameeleza kuwa programu hiyo inaendeleza kituo cha
kuzalisha vifaranga vya samaki kilichopo Mwamapuli wilayani Igunga, shamba la
kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo la Wakala wa Mbegu (ASA) )lililoko Kilimi
katika wilaya ya Nzega, na Wilaya ya
Uyui itapewa nafasi ya kuendeleza mnyororo ya Alizeti, Mahindi na
maharage.
Thursday, May 4, 2023
VIONGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA KWA WELEDI UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA KILIMO NA UVUVI
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala
ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka watendaji wa Mikoa, Wilaya
na Halmashauri kusimamia vizuri utekelezaji wa Programu ya Kilimo na Uvuvi
katika maeneo yao kwani ni sekta muhimu katika uchangiaji wa uchumi na usalama
wa chakula nchini.
Ameyasema hayo mapema leo Jijini Dodoma, katika warsha
ya utambulisho na uelewa wa Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa
watendaji wa Mikoa na Halmashauri.
Dkt. Yonazi amesema kuwa Serikali imeona kuna ulazima wa
kuwepo kwa usalama wa mbegu katika kilimo hivyo kupitia Wakala wa Mbegu za
Kilimo nchini ASA imeweza kuwekeza mbegu kwa wingi ili kuyafikia maono ya
serikali.
“Serikali imeendelea kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa
mbegu bora ambapo hadi kufikia Aprili 2023, jumla ya tani 49,962.35 za mbegu
bora zimepatikana sawa na asilimia 26.68 ya mahitaji ya tani 187,197 kwa
mwaka,”alisema Dkt. Yonazi.
Aliongezea kuwa, serikali imejitahidi kuweka nguvu katika
upatikanaji wa mbegu hizo ili kuhakikisha
uwepo wa usalama wa chakula nchini, na kwa upande wa sekta ya uvuvi
imehakikisha kunakuwa na manufaa ya rasilimali zilizopo katika sekta hiyo kwani
bado hazijatumika vizuri.
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ina mpango wa kununua
meli zitakazotumika katika uvuvi wa kina kirefu cha bahari na hivyo kuweza
kuongeza lishe na hatimaye nchi kunufaiika na rasilimali za uvuvi.
Aliendelea kufafanua kuwa, Programu hii pia, itahusisha
ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na upanuzi wa
vituo vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki cha Kingolwira Morogoro.
“Lazima tushirikishe wadau ili tupeleke elimu ya kuweza
kuzalisha vifaranga na kujenga mabwawa, natoa msisitizo kwa viongozi wa mkoa
kuwa kuna jukumu la usimamizi, tuhakikishe tunasimamia vizuri mradi huu,
kushauri na kuutekeleza kwa wakati.” Alisisitiza Dkt. Yonazi
Awali, akiongea wakati wa Ufunguzi wa Warsha hiyo Bw. Paul
Sangawe Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, alisema lengo la programu hii kwa
upande wa sekta ya uvuvi, ni kuendeleza ufugaji wa viumbe maji pamoja na kuanza
uvuvi wa bahari kuu.
“Tunatazamia katika program hii meli zitanunuliwa kwa
matumizi ya pande zote mbili za Muungano na kuwezesha nchi yetu kwa mara ya
kwanza kufanya uvuvi katika bahari kuu ili kuweza kutumia rasilimali tulizonazo
kwa ufanisi, lakini vile vile uzalishaji wa mbegu pamoja na usambazaji, na
kuhakikisha fedha ambazo za mkopo ambazo tumepewa kutoka shirika la IFAD
takribani dola 58.8 milioni,zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija katika
utelezaji wa program hii.” Alisisitiza
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchumi na
Uzalishaji toka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Afisa Kilimo Mkuu Dkt. Rehema Mdendemi
amesema programu hii ya maendeleo ya kilimo na uvuvi itaenda kuboresha maisha
ya wakulima na wavuvi , na kujitosheleza kwa usalama wa chakula na kuleta ajira
hivyo program hii ni ya muhimu kwa serikali na wanachi kwa ujumla.
Wednesday, May 3, 2023
NEC YAANZA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU 2025
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo
katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa kuzingatia utaratibu na
vigezo.
Hayo yamesemwa leo
Bungeni Jijini Dodoma na Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akijibu maswali
ya baadhi ya wabunge walioomba
majimbo yao yagawanywe.
Amesema muda utakapofika, Tume
itatoa tangazo rasmi kwa wadau wote wa uchaguzi juu ya kuanza kwa machakato wa
ugawaji wa majimbo ili wadau wawasilishe maoni na maombi yao na hivyo
kushughulikiwa kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa kikatiba.
Mhe. Ummy amesema majimbo
mengi yameomba kugawanywa lakini mambo yanayotazamwa ni pamoja na ukubwa wa
ukumbi wa jimbo, idadi ya wabunge wa viti maalumu na jiongrafia za maeneo
yaliyoomba kugawanywa.
Friday, April 28, 2023
WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 15
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf
Mkenda na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Pauline Gekul Wakati wa Bunge la 12 Mkutano wa 11Kikao cha 15 Mjini
Dodoma.
Wednesday, April 26, 2023
SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 59 YA MUUNGANO MWAKA HUU YAFANYIKA KILA MKOA
Kilele cha sherehe za
Maadhisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwaka huu
yamefanyika kiaina yake, ambapo kila mkoa unaadhimisha kwa kutelekeza maelekezo
mahsusi ya Serikali.
Mkurugenzi wa Kitengo
ya Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na
Uratibu Bw. Batholomeo Jungu ameyamesema hayo jana wakati ziara maalum ya
Kamati ya Kitaifa ya maadhimisho hayo mwaka huu ilipotembelea na kukagua
utekelezaji wa maelekezo mahsusi kwa Ofisi za Serikali Jijini Dodoma.
Bw. Jungu alisema kuwa
kwenye mikoa ndipo kwenye wananchi hivyo shughuli hizi kufanyika katika mikoa
zinaleta chachu ya uzalendo kwa wananchi sababu kila mtu anapata nafasi ya
kushiriki kuanzia kwenye uzinduzi wa miradi, mashindano ya insha kwa wanafunzi,
michezo mbalimbali, usafi wa mazingira na maswala mengine muhimu.
"Watu wapo katika
kila mkoa, hivyo tukio hili la kushirikisha wananchi linaleta tija kwa jamii
kwa kuona ni sehemu ya maadhimisho haya kwa vitendo,"alisisitiza Jungu.
Kwa Upande wake Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bi. Mary Maganga aliseme
Kila mwaka tarehe 26
mwezi Aprili hututumika kama kumbukumbu ya sherehe za Muungano wa Iliyokuwa
Tanganyika na Zanzibar, uliyofanya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo
kaulimbiu ya Mwaka huu inasema “ Umoja wetu na Mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza
uchumi wetu.”
Katibu Mkuu Masanja
alitumia fursa hiyo kueleza namna ofisi yake ilivyotekeleza maelekezo mahsusi
ikiwemo kulipamba jengo la ofisi hiyo na kuweka picha za viongozi wakuu wa nchi
pamoja na waasisi wa taifa leo
Tuesday, April 25, 2023
WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 13
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na
Waziri wa Ardhi Nyumba Maendeleo na Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Mary Masanja Wakati wa Bunge la 12 Mkutano wa 11Kikao cha 13 Mjini Dodoma.
Monday, April 24, 2023
WAZIRI MHAGAMA KATIKA KIKAO CHA BUNGE CHA 12
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza Mhe.
Jaji Dkt. Eliezer Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakati wa Bunge la 12
Mkutano wa 11Kikao cha 12 Mjini Dodoma.
Tuesday, April 18, 2023
WATAALAM WAJADILI KUHUSU MPANGO HARAKISHI WA UPATIKANAJI WA RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA.
SERIKALI imefanya uwekezaji
mkubwa na maboresho katika sekta ya Afya yanayokwenda sambamba na uwepo wa
rasilimali watu itakayotoa huduma zenye ubora ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Mipango ya Rasilimaliwatu katika sekta ya Afya Bw. Issa
Mmbaga kutoka Wizara ya afya wakati wa mawasilisho yaliyohusu upatikanaji wa
rasilimali watu katika sekta ya Afya, kwenye kikao cha wataalam kilichofanyika
Jijini Dodoma.
Bw. Mmbaga alisema kuwa,
baadhi ya maboresho yaliyofanywa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita katika
sekta hiyo ni pamoja na ujenzi wa hosptali mpya, ongezeko la vifaa tiba na
kuboreshwa kwa miundombinu iliyopo katika eneo la huduma.
“Maboresho haya yamesababisha
mahitaji ya ziada ya watumishi katika sekta hii hivyo serikali ina mikakati
maalum ya kuhakikisha kunaupatikanaji wa kutosha wa wataalam ili kuwa na sekta
ya afya yenye nguvu na uwezo wa kutoka huduma bora za afya”. Alisema Bw.
Mmbaga.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Sera na Program Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.
Crispin Musiba, amesema kuwa, uzalishaji wa madaktari na wataalamu wengine
katika sekta ya Afya umekuwa mkubwa zaidi kiasi kwamba, idadi kubwa ya wataalam
hao wapo nje ya ajira.
“Kwa hivyo ili kupunguza
muonekano wa wataalam hao kuwepo nje ya Ajira, tumeita kikao hiki ili kuweza
kuwa accommodate wataalam hao katika kupata ajira, na kikao hiki kimetoka na
maazimio nane (8) ambayo tumepeana muda wa mwezi mmoja ili yaweze kukamilishwa
na kuwasilishwa katika ngazi za juu.” Alisisitiza
Naye Mkurugenzi wa Afya kutoka
Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapalagwe alisema, ipo haja ya kuendelea kuwa
na program za elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii hususan
katika masuala ya huduma za kiafya ikiwemo zile za kibingwa zinazotolewa pamoja
na kuwa na mikakati madhubuti ya tafiti mbalimbali zitakazoweza kusaidia kujua
rasilimali iliyopo katika masuala ya afya.
“Maendeleo yaliyopo katika
sekta ya afya, hayatazaa matunda ikiwa hatutaendelea kutoa elimu kwa umma kwa
upana wake na kuwa na mikakati ya makusudi inayolenga kuboresha kada
hii,”alisema Dkt. Ntuli
Kikao Hicho kilihusisha
wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Utumishi,
Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu.
=MWISHO=
Sunday, April 16, 2023
SERIKALI YADHAMIRIA KUENDELEA KUZINGATIA MASUALA YA UTAWALA BORA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema
serikali imeridhia kuwa kifungu maalumu cha bajeti kwa ajili ya kuendesha
baraza la Vyama Vya Siasa ili kuweza kufanya shughuli zake kwa ufanisi.
Kauli hiyo imetoloewa wakati
wa Ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Vyama Vya Siasa kilichofanyika Mjini Dar es
salaam . Amesema serikali Imepitisha Bajeti ya shilingi Billioni Shilingi 1,586,662,000.00 kwa ajili ya kuendesha
baraza la Vyama Vya Siasa kwa Mwaka wa fedha 2023/24.
“Kwa kuwa sasa Mhe. Rais Dkt.
Samia Sulluhu Hassan ameamua kutenga fedha ya kuendesha baraza, naomba vikao
vyote vya kikatiba vya baraza la vyama vya siasa vikae kwa kwa mujibu wa ratiba
ikiwa ni pamoja na vikao vya kamati kwa kufuata kanuni na sheria.”
Ameongeza kusema baraza la
vyama vya siasa lipewe nafasi ya kukutana serikali ili kujadiliana kuhusu mambo
mabalimbali yanayohusu ustawi wa Demokrasia Nchini.
Iko miradi ya kimkakati hapa
nchini, kuna kila sababu viongozi wa vyama vya siasa na baraza la vyama vya
siasa wapate nafasi ya kuangalia miradihiyo , kwa sababu tunapofika kwenye
masuala ya maendeleo ya nchi na ustawi nchi hakuna chama.
“kuna nafasi ya viongozi wa
vyama vya siasa kutushauri vizuri zaidi kwa ustawi wa wananchi, “alisema Waziri
Mhagama.
Aidha tunahitaji kutengeneza programu
maalumu ya mafunzo kwa ajili ya viongozi wetu wa vyama vya siasa, ili tuendele
kuimarisha Demokrasia ya vyama vingi
chini, hatuwezi kufanikiwa kama viongozi wetu hawataendana na mabadiliko yanayoyendelea
kwenye ulimwengu wa sasa.
Katika hatua nyingine Waziri
Mhagama ameomba migogoro ya vyama imalizwe ndani ya vyama, tunauwezo wa
kuimaliza sisi wenyewe, tujenge uwezo wa kutizama matatizo yetu ndani ya chama
na kuyamaliza ndani ya vyama vyetu.
Waziri amehimiza viongozi wa
vyama vya siasa, kuzingatia sheria za matumizi na mapato ya fedha.
Waziri Mhagama ametumia fursa
hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan
kwa kuboresha mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
“Mhe.
Rais alipoingia madarakani aliasisi ” 4r” ambazo ni (reconcilian, resiliance,
reform and rebuilding) kwa kiswahili ni maridhiano, ustamilivu, mageuzi na mabadiliko
hii ikiwa ni kwa lengo la kutoa mwongozo wa jinsi ambavyo siasa za nchi yetu
zinapaswa kuwa.”
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Siasa Juma Ally Khatibu, ameomba mfaunzo ya siku tatu mara tu baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
ili kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ” 4r”
Mafanikio
ya kikosi kazi katika Mkutano ule uliofunguliwa Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan Jijini Dodoma ambao ni zao
la Baraza la Vyama Vya Siasa, ni pamoja na kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya
vyama vya siasa, mafanikio mengine ni
kuundwa kwa Tume ya Rais ya kuangalia namna
ya kuboresha Taasisi za Haki jinai.
Thursday, April 13, 2023
BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU IMEZINGATIA VIPAOMBELE MUHIMU KATIKA MASUALA YOTE YA URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI
Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri
Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu imezingatia vipaombele muhimu katika maeneo yote yanayoratibiwa na Ofisi
hiyo ili kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija kwa Taifa.
Ametoa kauli hiyo mapema leo
wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Mwaka wa
fedha 2023/24 wakati wa Kikao cha Bunge
la 12 Mkutano wa 11 Kikao cha sita Mjini Dodoma.
Waziri Mhagama amesema pamoja
na mambo mengine, Bajeti ya Mwaka huu ya Ofisi ya Waziri Mkuu imezingatia
masuala muhimu ikiwemo la Uratibu wa shughuli za Serikali kwa kueleza tayari
ofisi hiyo umeunda Idara ya ufuatiliaji
na Tathimini ya utendaji wa serikaliambapo itawezesha kuwa na taarifa sahihi za
utekelezaji wa Shughuki za Serikali.
Akizungumzia kuhusu Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Waziri Mhagama amesema, Mamlaka
imefanya kazi ya kutosha katika maeneo
yote manne ya kimkakati ya kupambana na dawa za kulevya, kupunguza uingizaji wa
dawa za kulevya, kufanya ukaguzi katika maeneo yanayofanya biashara ya kemikali
bashirifu na kufanya maboresho ya sheria na kuteketeza mashamba mengi ya bangi
nchini.
Aliongeza kwa kusema kuwa, Mamlaka imefanya vizuri katika
kutoa elimu ya uelewa kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya.
“Tumefanya vizuri katika
kupunguza athari za madhara ya dawa za kulevya kwa waathirika, na huduma ya za
kutibu urahibu wa dawa za kulevya na bado tunaendelea kufanya mashirikiano ya
nchi, kikanda na kimataifa ili kukabiliana na jambo hili mtambuka.”Alisisitiza
Kwa Upande wa suala la Sera ya lishe, Waziri amesema Wizara ya Afya
kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, itakuja na Mkakati wa kuwa na Sera ya
lishe, UKIMWI na Janga la matumizi ya Dawa za kulevya.
Pamoja na hilo, Waziri
alieleza kuwa ofisi yale inasimamia Dawati la Afya Moja linaloshughulikia
uratibu wa magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,
ili kuweza kukabiliana nayo na kuangalia usalama wa wananchi.
Aidha alitumia nafasi hiyo
kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu
Hassan, kwa kwa falsafa yake ya kuliwezesha Taifa kuwa na ustahimilivu na
kuleta mabadiliko makubwa ya kiuongozi, kidemokrasia, kiuchumi na mahusiano ya
kimataifa na kuwataka wabunge
kuunga mkono falsafa hiyo.
Friday, April 7, 2023
WAZIRI MHAGAMA NA SIMBACHAWENE WAKABIDHIANA OFISI
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi
wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati
wa hafla ya makabidhiano kati ya aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene na aliyekuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista
Mhagama mara baada ya uteuzi uliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan Aprili 01 mwaka 2023.
Waziri Mhagama
amesema dhamira ya mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha anatimiza
wajibu wake kikamilifu katika kuwahudumia wananchi mahali na kwa nafasi yoyote
anayopangwa kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizopo.
“Mara zote dhamira ya
mtumishi wa umma Nchini ni kuhakikisha kila unapopangwa unafanya kazi kwa
nguvu zako zote pamoja na utii na kuwa tayari kutumikia Taifa mahali
popote kwahiyo kurudi kwangu hapa najihesabu ni sehemu yenu pia kama mtumishi
wa umma,” Amesema Mhe. Jenista.
Pia amebainisha kwamba
Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ina jukumu la kuratibu shughuli za Serikali haiwezi
kufanikiwa ikiwa watumishi wake watashindwa kujidhatiti na kufanya kazi kwa
moyo kwa kuzingatia mazingira husika.
“Msingi wa tija katika
utendaji wa kazi Serikalini unatutaka kuwa na uratibu mzuri
unaozingatia sera, miongozo na kanuni zilizopo kwa kuzingatia jukumu kubwa la
Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu shughuli zote za Serikali na tuna jukumu la
kusimamia Bunge kama mhimili mwingine ndani ya Nchi hivyo bila kuwa na
ushirikiano hatutafikia malengo tunayokusudia,” Ameeleza.
Kwa upande wake Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kumuamini na kumpa fursa ya kulitumikia Taifa pamoja na
watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji
wa majukumu yake.
“Nitumie nafasi hii
kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini kuendelea kuwatumikia
wananchi katika nafasi hii na watumishi pia nawashukuru kwa ushirikiano
mlionipatia na kuwezesha kufanikisha shughuli za uratibu kwa kipindi chote,”
Ameshukuru Mhe. Simbachawene.
Naye Katibu Mkuu Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Mhe.
Simbachawene kwa utumishi wake mwema katika Ofisi hiyo.
Aidha ametumia nafasi
hiyo kumkaribisha Mhe. Waziri Mhagama katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuahidi
kumpa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananachi.
Sunday, April 2, 2023
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. DKT, SAMIA SULUHU HASSAN AMEWAPISHA MAWAZIRI WAWILI LEO BAADA YA KUFANYA MABADILIKO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Jenista Mhagama kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 02 Aprili, 2023
Saturday, March 25, 2023
SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YAKABIDHI MISAADA YA KIBINADAMU KWA SERIKALI YA MALAWI
Balozi wa Tanzania
Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole ameshiriki katIka zoezi la kukabidhi
misaada ya Kibinadamu kutoka Tanzania kwa Serikali ya Malawi ili kusaidia
wahanga wa Kimbunga Freddy.
Balozi amekabidhi
misaada hiyo ya kibinadamu inayojumuisha Mablanket, Mahema, Unga wa Mahindi kwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo katika Mji wa Blantrey Nchini
Malawi mapema.
Balozi Polepole
alibainisha kuwa wa watanzania, na watu wa Malawi ni jamii moja, na Nia
ni kuendekeza umoja uliojengwa na waasisi wa Nchi zetu.
" Msaada
huu wa kibinadamu utasaidia, katika jitihada za kurejesha matumaini na
ustawi kwa ndugu zetu Wananchi wa Malawi", Alisisitiza Balozi Polepole.
Aliongeza kusema kuwa
ana imani na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioenda
Nchini Malawi watashirikiana na wenzao Wanajeshi wa Malawi,
kuhakikisha kwamba misaada iliyotolewa inawafikia Wahanga wa Kimbunga
Freddy.
Aidha, Tanzania imetoa madawa ya binadamu, ambayo yataweza
kusaidia kwenye maeneo ambayo vituo vya afya vimeathirika. Hizi zote ni
jitihada za kusaidia Nchi ya Malawi katika kurejesha huduma za afya.
"Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Msaada aliotoa kwa Nchi ya Malawi, kwa
uwezeshaji wa fedha na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(Wahandisi wa Medani) ambao watasaidia katika kurejesha hali ya miundo mbinu
Nchini Malawi," alisema Balozi.
Kwa upande wake Waziri
wa Mambo ya nje wa Nchi ya Malawi Mhe. Nancy Tembo amesema ameshukuru Nchi ya
Tanzania kwa Msaada wa kibinadamu iliowapatia, ambao umefika katika wakati
muafaka.
“Msaada huu ni muhimu
kwetu kwa sababu tunao Wanachi wengi ambao makazi yao yameharibika, na
tunahitaji msaada wa kila mtu ili kuhakikisha wahanga wa Kimbunga Freddy
wanapatiwa huduma za msingi kwa wakati,” alisema Waziri Nancy
Aliongeza kusema
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamekuja kutusaidia na wataungana na
askari wetu wa Nchini Malawi katika kurudisha miundo mbinu iliyoharibika katika
hali ya kawaida.
“Nachukua fursa hii
kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia katika
wakati ambao tunahitaji msaada sana, janga hili ambalo limeathiri Nchi ya
Malawi, limegharimu maisha ya watu, na limeharibu miundo mbinu” alisema Waziri
Nancy.
Naye Mkurugenzi
Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu Luteni Kanali Selestine
Masalamado ametoa pole kwa wananchi wa Malawi kwa Maafa ya Kimbunga Freddy.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa
kuratibu swala la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wahanga wa Kimbunga
Freddy Nchini Malawi, ambapo kwa awamu ya kwanza helikopta mbili kutoka Jeshi
la Wananchi wa Tanzania zilisafiri kuja Malawi kufanya kazi za wokozi,
lakini msaada wa pili ilikuwa ni msaada wa fedha kwa serikali ya Malawi na tatu
ni kutoa msaada wa kibinadamu kwa Wahanga wa Kimbunga Freddy.
Thursday, March 23, 2023
MISAADA ILIYOTOLEWA NA SERIKALI YA TANZANIA KWA WAHANGA WA KIMBUNGA FREDDY YAVUKA MPAKA KUELEKEA NCHINI MALAWI.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na
Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu,
Luteni Kanali Selestine Masalamado ameongoza ujumbe wa kutoka Nchini Tanzania
kupeleka misaada ya unga, mahindi, mablanketi, mahema na madawa mbalimbali
ambayo yatasaidia wahanga wa Kimbunga Freddy kilichotokea nchini Malawi.
Luteni Kanali Masalamado amesema
hayo wakati Msafara wa magari ya jeshi la Wanachi wa Tanzania yakivuka mpaka wa
Kasumulu wilaya ya Kyela kuelekea Mji wa Blantyre Nchini Malawi.
“Natoa pole kwa ndugu zetu,
wananchi wa Malawi tuko nao katika hali hii ngumu,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa kikosi
Luteni Kanali George Kamya amesema wanasikitika kwa yale yaliyotokea nchini
Malawi baada ya kupigwa na Kimbunga Freddy.
“Katika kuitikia hilo serikali
ya Tanzania imetoa msaada kuwasaidia wenzetu waliopata na haya Majanga,”
alisema
Kwa upande wake Mkuu wa
Msafara Luteni Kanali George Kamya amesema wanasikitika kwa yale yaliyotokea
nchini Malawi baada ya kupigwa na Kimbunga Freddy.
“Katika kuitikia hilo serikali
ya Tanzania imetoa msaada kuwasaidia wenzetu waliopata na haya Majanga,”
alisema
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya
ya Karonga Nchini Malawi Mhe. Roderick Mateauma ameishukuru serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na kusema kwamba msaada huo utasaidia kupunguza athari
kwa wahanga na inaonesha mahusiano ya karibu yalipo kati ya nchi hizo mbili.
Saturday, March 18, 2023
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA, YATEMBELEA MIRADI YA UJENZI WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA KIWANDA CHA UCHAPAJI WA NYARAKA ZA SERIKALI.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya
Utawala Katiba na Sheria imeonesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa na Ujenzi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali
Mjini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria Mhe. Joseph Mhagama,
leo 18 March 2023 katika ziara ambayo ililenga kujionea kile ambacho kimepangwa
kwenye bajeti ya Serikali na kuangalia hatua zilizopigwa, changamoto
zilizojitokeza na namna ya utatuzi wake.
“Ziara hii imetuwezesha kupata
uhalisia wa hali jinsi ilivyo, ili iweze kutusaidia wakati wa kupanga bajeti,
tuwe na uhalisia wa utekelezaji miradi” alisema.
Akizungumzia kuhusu Idara ya
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mhe. Mhagama amesema upo muhimu wa Idara hiyo kuwa
na mifumo rasmi ya kujisimamia bajeti yake yenyewe (kama wakala) ili isaidie idara
hiyo iweze kuingia katika soko shindani.
Aliongeza kusema Idara ya
Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ikiweza kujisimamia katika bajeti yake, itasaidia
kuongeza Makusanyo mengi ambayo yanategemewa kutoka katika Idara hiyo.
Tunachangamoto kubwa sana
katika utengenezaji wa nembo ya Taifa, “lazima tuwe na Mamlaka moja ya
kutengeneza nembo ya Taifa na watu wengine wote waipate kupitia katika Ofisi ya
Mpiga Chapa wa Serikali, “alisema Mhe. Mhagama.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi
ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George
Simbachawene amesema anakubaliana na maelekezo ya Kamati. Wizara itatoa taarifa
mbele ya Kamati hatua iliyofikia katika kuandaa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha
Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa wakala.
Naye Mhe. Ahmed Ngwali Mjumbe
wa Kamati, ameshauri Idara ya Mpiga Chapa Mkuu Wa serikali Kufanyia kazi
mapendekezo ya Kamati mapema ili iweze kubadilishwa na kuwa wakala.
Awali Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali Bwn. George Lugome amesema Utakapokamilika mradi wa Kiwanda cha
Uchapaji wa Nyaraka za Serikali itasaidia kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu
ikiwa ni sambamba na kuongeza ajira na kuwa sehemu ya mafunzo kwa watu
wanasomea maswala ya uchapishaji.
Tuesday, March 14, 2023
WAZIRI SIMBACHAWENE “TUTUMIE RASILIMALI ZILIZOTOLEWA KUFANYA KAZI”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George
Simbachawene, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kutumia rasilimali zilizotolewa
kufanya kazi kwa bidii na ufanisi.
Mhe.Simbachawene ameyasema
hayo mapema leo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Baraza la
Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichokutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa
bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na makisio ya matumizi ya fedha kwa
mwaka wa fedha 2023/24.
Aliendelea kusema kuwa, Baraza
la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu sana mahala pa kazi kwani ni kiunganishi kati
ya Menejimenti na Watumishi, na alibainisha kuwa, Serikali inazingatia sana
suala la Wizara na Taasisi zake kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwani,
yanaanzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za
Idara, Taasisi na Wizara ili kuweza
kusimamia kazi na rasilimali watu.
Alibainisha kuwa mabaraza haya
yana majukumu ya kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa
ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, masilahi ya wafanyakazi na kusimamia
haki na ustawi katika sehemu za kazi. Wajibu wa mabaraza haya kama vyombo vya
ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu
na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya
utendaji wa kazi yenye tija, staha na upendo.
Ameshauri menejimenti kupitia
baraza hilo la wafanyakazi, kuwa na utaratibu mzuri wa kuwapongeza wafanyakaki
wanaotekeleza majumu yao kwa uweledi, ”kuna watumishi ambao kufaya kazi kwa
weledi na biidii, na kuwahudumia wananchi kwao ni kama sehemu ya ibada.”
Alifafanua
Aliendelea kusema kuwa
Utumishi wa umma wa zama hizi ni watu wenye ueledi,wasomi na wenye wasifu mkubwa,lakini
wanashindwa kuuonesha kutokana na mazingira kutokuwa rafiki,aliwaasa watumishi
wa ofisi hiyo kufanya kazi ya umma kwa bidii.”Jukumu kubwa kwa ninyi viongozi
ni kuwahudumia wadogo ili waweze kuleta matoke.”alisema Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi aliwashukuru watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kutekeleza majukumu yao na kusimamia shughuli mbali mbali za serikali kwa
kujituma na kwa ufanisi mkubwa.
Thursday, February 23, 2023
TANZANIA YA KWANZA KUSAINI MKATABA WA KITUO CHA HUDUMA YA DHARURA CHA MAAFA MIONGONI MWA NCHI ZA SADC
Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini
mwa Afrika SADC, kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu
na oparesheni za dharura za kanda.
Akizungumza
mapema hii leo wakati wa hafla ya utiaji Saini iliyofanyika Jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene
amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati
ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.
Aliongeza
kuwa, Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni
kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda
ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa
Filipe Nyusi tarehe 21 Juni, 2021.
“Lengo
la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya
kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli
za usimamizi wa maafa.” Alifafanua.
Aliendelea
kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati
ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi;
Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu
Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida
uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na
Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John
Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana
mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.
Awali
mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto,
alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na
jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri
itavyowezekana.
“Natoa
Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea
nchi 11 kusaini mkataba huu” Alifafanua Dkt Matto.
MITANDAO YA KIJAMII
Popular Posts
-
Na. OWM, Dodoma. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, imefanya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria Na.5 y...
-
Wataalamu wa Afya moja wakiwa katikapicha ya pamoja wakati wa mkutano wa wataalamu wa Afya moja uliojikita katika ulinzi na usalama...
-
Na. OWM, ARUSHA Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri...
-
Washiriki wa Mkutano wa mwaka wa Wataalamu wa Maabara wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa mwaka kwa wataalam wa maabara w...
-
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia sukari, alipotembelea kiwanda cha Kilombero Sugar, kilichopo katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Mo...
-
TAMOBA wafanya wasilisho la mfumo maalum wa kielektroniki wa ulinzi na usalama wa Bodaboda na BajajiKampuni ya Tanzania Motorcycle and Bajaj Association (TAMOBA) imefanya wasilisho maaluum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mfumo maalum wa ...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, ambaye ndiye anayesimamia Kamati ina...
-
*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sik...
-
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akipokea maelezo ya namna mashine zinavyochakata mifuko chakavu na ...
-
Katika kuhakikisha malengo ya kutatua masuala ya ajira na kazi, yanafikiwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Mhe. Samia Suluhu H...


.jpg)
.jpg)










%20(1).jpg)








