Saturday, March 18, 2023

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA, YATEMBELEA MIRADI YA UJENZI WA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA KIWANDA CHA UCHAPAJI WA NYARAKA ZA SERIKALI.


 

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeonesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ujenzi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali Mjini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria Mhe. Joseph Mhagama, leo 18 March 2023 katika ziara ambayo ililenga kujionea kile ambacho kimepangwa kwenye bajeti ya Serikali na kuangalia hatua zilizopigwa, changamoto zilizojitokeza na namna ya utatuzi wake.

“Ziara hii imetuwezesha kupata uhalisia wa hali jinsi ilivyo, ili iweze kutusaidia wakati wa kupanga bajeti, tuwe na uhalisia wa utekelezaji miradi” alisema.

Akizungumzia kuhusu Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mhe. Mhagama amesema upo muhimu wa Idara hiyo kuwa na mifumo rasmi ya kujisimamia bajeti yake yenyewe (kama wakala) ili isaidie idara hiyo iweze kuingia katika soko shindani.

Aliongeza kusema Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ikiweza kujisimamia katika bajeti yake, itasaidia kuongeza Makusanyo mengi ambayo yanategemewa kutoka katika Idara hiyo.

Tunachangamoto kubwa sana katika utengenezaji wa nembo ya Taifa, “lazima tuwe na Mamlaka moja ya kutengeneza nembo ya Taifa na watu wengine wote waipate kupitia katika Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali, “alisema Mhe. Mhagama.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amesema anakubaliana na maelekezo ya Kamati. Wizara itatoa taarifa mbele ya Kamati hatua iliyofikia katika kuandaa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa wakala.

Naye Mhe. Ahmed Ngwali Mjumbe wa Kamati, ameshauri Idara ya Mpiga Chapa Mkuu Wa serikali Kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati mapema ili iweze kubadilishwa na kuwa wakala.

Awali Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Bwn. George Lugome amesema Utakapokamilika mradi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali itasaidia kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu ikiwa ni sambamba na kuongeza ajira na kuwa sehemu ya mafunzo kwa watu wanasomea maswala ya uchapishaji.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.