Monday, July 23, 2018

MAWAZIRI WAKUU WA TANZANIA NA JAMHURI YA KOREA WAHUTUBIA KONGAMANO LA PILI LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA KOREA - JIJINI DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Kongamano la Pili la  Biashara na Uwekezaji  Kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam Julai 23, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia katika Kongamano la Pili la  Biashara na Uwekezaji  Kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam Julai 23, 2018.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea,  Lee Nak- yon akihutubia  katika  Kongamano la Pili la Biashara  na Uwekezaji Kati ya Tanzania na  Korea kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Julai 23, 2018.

aziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - yon (kulia kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji  Kati ya Tanzania na Korea kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam Julai 23, 2018. Kushoto kwa Waziri Mkuu Majaliwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga.

Read More

Sunday, July 22, 2018

MAZUNGUMZO RASMI YA KISERIKALI KATI MAWAZIRI WAKUU WA TANZANIA NA JAMHURI YA KOREA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimina na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea ,  Lee Nak -Yon wakati mgeni huyo alipowasili kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam kwa mazungumzo rasmi ya kiserikali, Julai 22, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea,  Lee Nak - Yon  (kushoto ) wakiwa katika mazungumzo rasmi ya kiserikali kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam Julai 22, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea,  Lee Nak - Yon  (kushoto ) wakiwa katika mazungumzo rasmi ya kiserikali kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam Julai 22, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - Yon (kushoto) wakishuhudia wakati Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Augustine Mahiga  na  Makamu wa Kwanza wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Korea, Lim Sung - Nam  (kushoto) walipotia saini Mkataba  wa kuondoa Hitaji la Viza za Kusafiria kwa Watu Wenye Hati za Kusafiria za Kidiplomasia na Kikazi, kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam Julai 22, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumnza na waandishi wa habari wakati alipotoa taarifa kuhusu mazungumzo rasmi ya kiserikali kati yake na Waziri Mkuu na Korea, Lee Nak- Yon (kushoto) kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam Julai 22, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Waziri  Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak - Yon baada ya mazungumzo rasmi ya kiserikali kati yao yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es slaam, Julai 22, 2018.

Read More

Saturday, July 21, 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AMPOKEA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA KOREA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye amewasili nchini leo saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai 21, 2018) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Kwenye uwanja wa ndege, Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea alipokelewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.

Pia ameambatana na ujumbe wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki Kongamano la Kibiashara baina ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business Forum) lililopangwa kufanyika kesho kutwa (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Kesho (Jumapili, Julai 22, 2018), Waziri Mkuu Lee Nak Yon atakuwa na mazungumzo rasmi ya kiserikali na mwenyeji wake pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali na pia kwa pamoja watashuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and service  passports).

Pia ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha.

Anatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018.

Read More

WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA KOREA , LEE NAK - YON AWASILI NCHINI NA KUPOKELEWA NA WAZIRI MKUU KASSIM MAJLIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Lee Nak-Yon wakati mgeni huyo alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Kamabarage Nyerere jijini Dar es salaam kwa Ziara ya siku tatu chini Julai 21, 2018. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Lee Nak- Yon baada ya mgeni huyo kuwasili kwenye  uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam kwa Ziara ya siku tatu nchini, Julai 21, 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Lee Nak- Yon baada ya mgeni huyo kuwasili kwenye  uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam kwa Ziara ya siku tatu nchini, Julai 21, 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Jamhuri ya Korea ,Le Nak Yon wakifurahia ngoma kwenye uwanja wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Juilai 21, 2018.

Read More

Wednesday, July 18, 2018

WAZIRI MHAGAMA ATENGUA UTEUZI WA KAIMU MTENDAJI MKUU WA TaESA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Muhagama akisilikiliza hoja za baadhi ya Wafanyakazi wa  Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) wakati wa mkutano na wafanyakazi hao jinjini Dar es Salaam.

Watumishi wa Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Muhagama  wakati wa mkutano na wafanyakazi hao jinjini Dar es Salaam. 

Watumishi wa Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,  Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Muhagama  wakati wa mkutano na wafanyakazi hao jinjini Dar es Salaam. 

Read More

Tuesday, July 17, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA FAO LA USHIRIKA AFYA LA NHIF

  
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua fao la Ushirika Afya ambalo linawalenga wananchi wanaojishughulisha na kilimo kupitia ushirika.

Amezindua fao hilo jana (Jumatatu, Julai 16, 2018) kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ulowa katika kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Shinyanga.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi 20 kwa niaba ya wanachama 259 ambao wamejiunga na mpango huo. Wanachama hao wanatoka katika vyama mbalimbali vya ushirika kwenye Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.

Alisema katika kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za afya katika hospitali yoyote ile nchini, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, wameamua kuzindua mpango wa Ushirika Afya, ambao unahusisha wakulima walio katika vyama vya ushirika.

“Gharama ya kujiunga na fao hili kwa mwaka ni sh. 75,000 kwa mtu mmoja na sh. 50,000 kwa mtoto mmoja lakini unakuwa na uhakika wa kutibiwa katika hospitali yoyote ile hapa nchini,” alisema.

Alisema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania kuna vyama vya ushirika 10,522 vyenye wanachama 2,234,000 ambapo asilimia 35 ya wanaushirika huwa wanapata magonjwa ya dharura na wanakuwa hawana namna ya kupata fedha kwa haraka.

“Tunatambua wote kuwa fedha ya mkulima ni ya msimu, lakini mkulima ukiwa na kadi ya bima ya afya, utapata matibabu kokote kule hata kama huna fedha taslimu,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza kijana aliyebuni mpango huo ambaye anatoka Taasisi ya Ukuzaji wa Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Bw. Mwombeki Baregu. “Huyu kijana si mwajiriwa wa NHIF, wala siyo mtumishi Serikalini, lakini kwa sababu ya uzalendo, alikuja na huu mfumo akauelezea na kuonesha manufaa yake kwa wananchi wa kawaida, na kwa sababu Serikali yenu ni sikivu, tukaufanyia kazi na leo ninauzindua,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema kuna vyama vya ushirika takribani 10,000 ambavyo vina wanachama zaidi ya milioni 2.5 wanaojishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo pamba, korosho, tumbaku, chai na kahawa.

“Lengo letu ni kuwafikia wanachama hawa pamoja na familia zao ili kuwawezesha wapate huduma katika kipindi cha mwaka mmoja tangu siku alipochangia. Kupitia utaratibu huu, mwanachama atapata huduma za uchunguzi na matibabu katika vituo zaidi ya 6,000 vilivyosajiliwa na mfuko wetu nchi nzima,” alisema.

“Kupitia mpango huu wa ushirika afya, mwanachama atapata huduma za vipimo na matibabu mpaka ngazi ya Taifa kulingana na ushauri wa wataalam. Mfuko kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, itaendelea kutoa elimu kwa wanachama wa ushirika kwa lengo la kuongeza uelewa wa mpango huu kwa walengwa,” aliongeza.

Alisema NHIF imeufanyia maboresho mpango huo ambapo kwa sasa wameanzisha vifurushi mbalimbali ambapo mwanachama ataweza kuchagua kulingana na uwezo wake na ukubwa na hali ya familia yake.

“Vifurushi hivyo vinaanzia kwa mwanachama aliye peke yake, aliye na mwenza, aliye na mwenza na mtoto mmoja, wawili mpaka wanne. Kwa mwanachama asiye na mwenza lakini ana familia, mpango huu umeweka utaratibu wake,” alifafanua.

Akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu, Spika Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Mama Anne Makinda alisema uzinduzi uliofanyika jana umewakilisha kuzinduliwa kwa fao hilo kwenye mikoa yote nchini.

Alisema wana mpango wa kwenda kwenye mikoa yote inayozalisha mazao makuu matano ya kimkakatii ambayo ni chai, kahawa, pamba, tumbaku na korosho ili waweze kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi.
Read More

Monday, July 16, 2018

WAZIRI MKUU AMWAGIZA RPC SHINYANGA AWAKAMATE VIONGOZI TISA WA AMCOS YA USHETU

*Ni kwa upotevu wa dola za Marekani 21,000
*Wakimbia mkutano baada ya wananchi kuzomea
  
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule awakamate viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa dola za marekani 21,000 za chama hicho.

"Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani," amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 16, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambao alienda kuzindua mpango wa Ushirika Afya na NHIF.

Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.

Kamanda Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti, Bw. Shilinde Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Bw. Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.

Akiwa katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU), Bw. Emmanuel Cherehani alisoma taarifa ya Chama na alipotaja bei ya tumbaku kuwa ni nzuri, wananchi walimzomea kupinga kile alichokisema. Bw. Cherehani alikuwa akitoa mafanikio ya chama hicho, na kusema kuwa bei ya tumbaku ni nzuri.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba alisema kuna tatizo katika uteuzi (grading) wa tumbaku kwani wakulima wanalima tumbaku nzuri lakini katika upangaji bei, wanalipwa bei ndogo. “Kuna wakulima wanakidai chama cha Mkombozi kiasi cha dola za Marekani ambayo ni madai ya tumbaku waliyoiuza tangu mwaka 2014.”

Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima. "Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.”

“Tunataka ushirika unaosimamiwa na viongozi waaminifu. Kwenye ushirika kuna fedha na kuna mali za chama, kwa hiyo ni lazima tupate viongozi ambao ni waaminifu,” amesema.

“Kwa mfano, hapa Ulowa wakulima wamekuwa wakilalamikia kupewa bei ya chini wakati wakati wao viongozi wanabeba kile cha juu na kuwaumiza wakulima. Kiongozi wa KACU kasoma taarifa hapa mkaanza kuzomea, hiyo ni dalili tosha kwamba kuna tatizo la msingi,” amesema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa wakulima waachane na tabia ya kukopa pembejeo na kufunga mikataba na makampuni ya ununuzi wa tumbaku na badala yake wajiwekee akiba ili msimu wa kilimo ukianza wasirudie tena kukopa.

“Gharama za kulima ekari moja, kuweka dawa, palizi na kuchoma haizidi sh. 150,000. Wewe amua unataka kulima ekari ngapi, weka fedha zako kwenye akaunti usubiri msimu ujao. Kwenye hii biashara ya tumbaku, ukitafuta mikopo utabakia kuwa maskini kwa sababu huna nguvu ya kubishania bei. Wenzenu wanaolima korosho, wameacha kukopa na bei mnazisikia kila mwaka zinapanda,” amesema.

“Ukiwa na mazao yako utaweza kubishana na mnunuzi. Tanzania bei ya tumbaku iko chini sababu wakulima mmetufikisha hapo kwa kupitia mikopo na mikataba na makampuni ya ununuzi. Kuanzia sasa badilikeni, ili muweze kuinua bei ya zao hili muhimu, alisema.
Read More

ZIARA YA MAJALIWA WILAYANI USHETU

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasha gari alilolizindua ambalo limenunuliwa na Halmashauri ya Ushetu kwa ajili ya Idara  ya Kilimo  ya Halmashauri hiyo , kwenye kijiji cha Kangeme Julai 16, 2018.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kangeme  kwenye  Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga,  Julai 16, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Fao la Ushirika Afya ambalo litawawezesha wanaushirika kunufaika na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwenye kijiji cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga Julai 16, 2018.  Kushoto kwake ni  Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, watatu kushoto ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kangeme  kwenye  Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga,  Julai 16, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwapungia wananchi wa Kijiji cha  Kangeme katika Halmashauri  ya Ushetu mkoani Shinyanga wakati alipowasili  kijijini hapo kuhututibia Mkutano wa hadhara na  kuzindua Fao la Ushirika Afya ambalo litawazesha wanaushirika kunufaika na huduma za Mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya, Julai 16, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maeleazo kutoka kwa  Waziri  wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba. (kushoto) wakati alipokagua uuzaji wa tumbaku katika Chama  cha Ushirika cha Msingi cha Kangeme katika Halmashauri ya  Ushetu, Julai 16, 2018.  Kulia kwake  ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeloeo ya Ushirika Nchini, Dkt. Titus Kamani.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi baada ya kukagua ujenzi wa zahanati ya Ukune katika Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Julai 16, 2018.

Read More

MAJALIWA AMTAMBULISHA MKUU WA WILAYA YA KAHAMA KWA WANANCHI NA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA KITUO CHA AFYA CHA CHELA WILAYANI KAHAMA.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipoweka  jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Julai 17, 2018. Watatu kushoto ni  Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na watano kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha na watatu kulia ni Mwenyeiiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa. Kushoto ni  Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elius Kwandikwa wapili kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kakunda.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Julai 17, 2018. Kulia ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akiwatambulisha viongozi wa wilaya ya Kahama wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasalimia wananchi wa Kijiji cha Chela baada ya kuweka jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Julai 17, 2018. Wanne kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na kulia ni Mbunge wa Msalala Ezekiel Maige.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimtambulisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha  wakati alipoweka jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Julai 17, 2018. Mkuu huyo wa wilaya aliapishwa jana asubuhi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Teklack.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimtambulisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha  wakati alipoweka jiwe la Msingi la Kituo cha Afya cha Chela katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Julai 17, 2018. Mkuu huyo wa wilaya aliapishwa jana asubuhi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Teklack.

Read More

Sunday, July 15, 2018

WAZIRI MKUU: MUWAFUATE WANANCHI VIJIJINI

*Ataka watenge siku tatu hadi nne waende waliko wananchi
*Asema Serikali hii haitaki mambo ya urasimu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wote wa Serikali za Mitaa nchini watenge theluthi mbili ya muda wao wa kazi kwa kuwasikiliza wananchi na kuwahudumia.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Jukumu la watumishi ni kuwatumikia wananchi, Serikali hii hatutaki urasimu na wala hatutarajii kuwa mtatoa huduma kwa urasimu. Lugha ya ‘njoo kesho, njoo kesho’ siyo ya kwa awamu hii.”

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wana jukumu la kusimamia agizo hilo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa usafiri kwa watumishi hao ili waweze kufika vijijini kwa haraka. “Wakurugenzi wa Halmashauri simamieni zoezi hilo kwa kupanga ratiba na kutoa gari ili maafisa wanne au watano watumie gari hilo kwenda vijijini wakawahudumie wananchi.”

Amesema wananchi wengi hawana uwezo wa kusafiri kutoka vijijini hadi mijini ili kuleta matatizo yao, kwa hiyo wakifanya hivyo, watumishi watakuwa wamewapunguzia matatizo wananchi.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani humo, amewataka watumishi wa idara ya ardhi wapime ardhi kwa wingi na watoe hati mapema ili wananchi wazitumie kuongeza mitaji.

“Pimeni ardhi na kutoa hati ili wananchi wazitumie kukopa na kupata mitaji ya kujiendeleza kiuchumi. Pia muweke mipango mizuri ya ardhi ili kuepusha migogoro baina ya wananchi.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Kahama kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Read More

WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU MICHANGO YA SHULE

*Yadaiwa wazazi Kahama wanatozwa sh. 20,000 kwa kaya
  
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hakuna michango yoyote itakayokusanywa kutoka kwa wazazi kwa ajili ya shule kama haina kibali cha Mkurugenzi wa Halmashuri.

“Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli alishapiga marufuku michango ya aina hii na akatangaza mpango wa elimumsingi bila malipo. Sasa hivi zinaletwa zaidi ya sh. bilioni 20 kila mwezi kwa ajii ya kuboresha elimu ya msingi katika kila wilaya.”

Waziri Mkuu ametoa katazo hilo jana (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Taifa wa Kahama, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kahama, Bw. Jumanne Kishimba ambaye alisema kuna michango inatozwa bila kibali chochote na kwamba kila kaya inatakiwa ilipe sh. 20,000. “Michango hii itolewe kwa kibali ina iangalie uwezo wa familia kiuchumi,” alisema.

Akitoa mfano, Mbunge hiyo alisema kuna familia ina madebe matatu tu ya mahindi ukiitoza hiyo hela, manake wauze mahindi yao yote ndiyo walete ya michango ma hiyo wabaki na njaa kwa mwaka mzima. Ni vema michango hiyo izingatie kipato halisi cha kaya,” alisema,

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao juhudi mbalimbali ambazo Serikali imezichukua ili kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma za maji, umeme, elimu na afya.

Alisema ameridhishwa na ujenzi wa viwanda unaoendelea kwenye mkoa wa Shinyanga na kukiri kuwa ameguswa kuona kuna uzalishaji mkubwa wa mafuta ya kula yanayotokana na mazao ya mbegu kama pamba na alizeti wakati kuna watu wanaagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

“Nimetembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya pamba cha Kahama Oil Mills, na mwenye kiwanda ameniambia kuwa miaka yote huwa anafanya kazi kwa miezi mitatu tu lakini mwaka huu ana uhakika wa kufanya kazi kwa miezi tisa, kutokana na jinsi ambavyo wakulima wameitikia wito wa kufufua zao la pamba,” alisema.

“Jana pia nilitembelea kiwanda cha JIELONG ambacho kiko kwenye Manispaa ya Shinyanga. Na kwenyewe nimeona uzalishaji mkubwa wa mafuta ya kula ambao sijapata kuona,” alisema Waziri Mkuu.

Mapema, Waziri Mkuu alizindua kituo cha afya cha Mwendakulima ambacho kilianza kujengwa mwaka 2010 na kukamilika mwaka 2016 kwa ufadhili wa kampuni ya kuchimba madini ya ACACIA kupitia mpango wake wa Corporate Social Responsibility. 

Kampuni hiyo imejenga chumba cha wagonjwa wa nje (OPD), nyumba mbili za watumishi (2 in 1) ambazo zinakaliwa na watumishi wanne, wameweka vitanda na solar panel kwa  gharama za dola za Marekani 710,000/- (kwa exchange rate ya kipindi hicho).
Read More

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA HADHARA KATIKA MJI MDOGO WA KAHAMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Taifa Kahama, Julai 15, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ngoma wakati  alipowasili kwenye Uwanja wa Taifa Kahama   kuhutubia mkutano wa hadhara, Julai 15, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

Read More

Friday, July 13, 2018

WAZIRI MKUU: WANAUME PIMENI VIRUSI VYA UKIMWI

*Asisitiza wananchi wajiunge na Bima ya Afya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanaume wote wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakapime afya zao ili kubaini kama wameambukizwa virusi vya UKIMWI au la.

Ametoa rai hiyo jana (Ijumaa, Julai 13, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

“Napenda kusisitiza kwa akinababa wote kwamba ukimwi bado upo na wanaume hamuendi kupima, ni wagumu kwenda kupima eti kwa sababu mnawategemea wake zenu waende kupima.”

“Unamwambia mama aende kupima virusi vya UKIMWI akija na majibu ukajua hana maambukizi, wewe huku unashangilia kwamba uko salama. Hapana, nendeni mkapime kwa sababu kila mmoja na vyanzo vyake vya kupata maambukizi,” alisisitiza.

Alisema maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) katika wilaya ya Kishapu yako kwenye asimilia 2.1 ikilinganishwa na kiwango cha maambukizi ya VVU kwa mkoa mzima ambayo kwa sasa ni asilimia tano.

“Ni vema familia zikapima VVU ili mjue hali zenu na muishi kwa furaha na kama kuna mmoja ameambukizwa basi aanze tiba mara moja,” alisema Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.

Alisema katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Tanzania inatekeleza malengo ya 90-90-90 ifikapo mwaka 2020.  Lengo ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia 90 ya waliopima VVU na kugundulika kuwa wana maambukizo wapatiwe dawa za kufubaza VVU (ARVs); na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU.   

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa wilaya ya Kishapu wajiunge na bima ya afya ili waweze kupata tiba hata wakati hawana fedha.

“Halmashauri yenu imeweka kiwango cha sh. 30,000 kwa mwaka ambapo baba, mama na watoto wanne watakaojiunga na huduma hii ya afya ya jamii, watapata matibabu bure kwa muda wa mwaka mzima mahali popote.”

“Ninawaomba mjiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utakuwezesha kupata tiba siku ambayo huna hela mfukoni au nyumbani. Pia utakuwa na uhakika wa kupata matibabu bure kwenye zahanati au kituo cha afya chochote kile katika katika wilaya hii,” alisema.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Read More

WAZIRI MKUU AWAONYA VIONGOZI WAPYA WA SHIRECU

*Ataka ushirika wa sasa urejeshe matumaini ya wakulima

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wapya wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga wajipime kama wako tayari kuwatumikia wananchi na kama sivyo waachie ngazi.

Ametoa onyo hilo jana (Ijumaa, Julai 13, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani mara baada ya kukagua soko la pamba kwenye kijiji hicho, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo, aliwataka wajumbe hao wajitafakari upya na kujihoji kama wameomba vyeo hivyo kwa ajili ya kupata utajiri ama kuwatumikia wananchi.

“Napenda kusisitiza kwamba ule mfumo wa zamani wa ushirika hivi sasa haupo. Kama uliomba cheo hicho kwa ajili ya kupata utajiri, ni bora ujiondoe sasa hivi, njoo uniambie wakati bado niko kwenye ziara ya mkoa huu, tutatafuta wajumbe wengine ambao ni waaminifu,” alisema.

“Nasisitiza kwa viongozi wa AMCOS na wa SHIRECU, mmeomba vyeo hivyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na siyo kujinufaisha binafsi,” alisisitiza.

Alisema tofauti na ilivyokuwa awali, Serikali ya awamu ya tano inataka kuona ushirika wa sasa ukirejesha matumaini kwa wananchi.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zamani, ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio lakini kutokana na hali ilivyobadilika, jambo hilo lilikuwa haliwezekani. “Tunataka ushirika wa sasa ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba bora,” alisema.

Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bw. Elias Kwandikwa alisema barabara ya kutoka Kolandoto hadi Igelekelo imeshafanyiwa usanifu na kwamba Serikali ya Ujerumani imeanza mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuhusu ujenzi wake.

Alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Mwangongo waliokuwa wakisubiri kumsikiliza Waziri Mkuu.

“Kazi ya usanifu wa barabara hiyo imekamilika, tumeanza mazungumzo ya kutafuta wafadhili. Ujenzi wake ukikamilika, utakuwa umerahisisha kuunganisha mkoa huu na mikoa ya Singida, Arusha na Manyara.”

“Kutoka Shinyanga hadi Singida tutakuwa tumepunguza km. 250, wakati kutoka Shinyanga jadi Karatu tutakuwa tumepunguza km. 400 badala ya kupita kwanza Nzega, uende Singida hadi Karatu,” alisema.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Read More

MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUCHAMBUA PAMBA CHA GAKI MJINI SHINYANGA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa dini baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwangongo wilayani Kishapu, Julai 13, 2018. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama pamba inayosubiri kuchambuliwa wakati aliootembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Gaki kilichopo mjini Shinyanga Julai 13, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na watatu kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda, Gaspar Kileo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mitambo ya kuchambua pamba wakati alipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Gaki Invesiment cha mjini Shinyanga, Julai 13, 2018. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na watatu kulia ni Mkurugenzi Mtendanji , Gaspar Kileo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mbengu za pamba wakati alipotembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha Gaki Investment kilichopo mjini Shinyanga Julai 13, 2018. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho, Gaspar Kileo.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kuchambua pamba cha GAKI na kusema amevutiwa na uwekezaji uliofanywa na wamiliki wa kiwanda hicho ambao ni Watanzania.

“Ninawapongeza wazawa walioamua kujenga kiwanda hiki kwa sababu viwanda kama hivi vinasaidia kukuza kilimo hapa nchini, kiwanda hiki kinachambua pamba na kusindika mafuta,” alisema.

Ametoa pongezi hizo jana jioni (Ijumaa, Julai 13, 2018) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya GAKI Investment pamoja na wananchi waliofika kumsikiliza mara baada ya kukagua utendaji kazi wa kiwanda hicho kilichopo Manispaa ya Shinyanga.

Waziri Mkuu alisema amevutiwa na ujenzi wa kiwanda hicho kwa sababu kinatoa uhakika wa soko la pamba ikizingatiwa kwamba mikoa yote inayolima zao hilo, mwaka huu imezalisha pamba kwa wingi kuliko kawaida.

“Mwitikio wa wakulima wa zao la pamba unaonyesha kwamba bado wana imani na Serikali yao na ndiyo maana nimewaonya wajumbe wa bodi ya SHIRECU kuwa wajihoji kama kweli wameomba nafasi hizo ili kuwatumikia wananchi,” alisema.

“Msije mkadhani kuwa SHIRECU ni mahali pa kuganga njaa. La hasha! Ni mahali pa kukuza soko la pamba. Tunataka viongozi wa sasa watambue kuwa hawajaenda SHIRECU ili kushiba, lazima walete mabadiliko kwenye ushirika na kama hawawezi waachie ngazi,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi wa kiwanda hicho wafanye kazi kwa uaminifu na watunze mashine za kiwanda hicho ili kiweze kufanya kazi kwa muda mrefu.

Mapema, akitoa maelezo ya uzalishaji wa kiwanda hicho kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa GAKI Investment, Bw. Gaspar Kileo  alisema kampuni hiyo inajishughulisha na ununuzi wa pamba kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Tabora.

Alisema uchambuzi wa pamba kwenye kiwanda hicho unatumia mashine zenye uwezo wa kuzalisha marobota 400 kwa siku. “Hapa kiwandani pia tunakamua mafuta yatokanayo na mbegu za pamba na tuna uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa siku,” alisema.

Alisema ili kuunga mkono kaulimbinu ya Tanzania ya viwanda, kampuni hiyo imeamua kujenga kiwanda kingine cha kuchambua pamba wilayani Meatu.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Shinyanga kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.


Read More