Saturday, July 21, 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AMPOKEA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA KOREA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye amewasili nchini leo saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai 21, 2018) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Kwenye uwanja wa ndege, Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea alipokelewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.

Pia ameambatana na ujumbe wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki Kongamano la Kibiashara baina ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business Forum) lililopangwa kufanyika kesho kutwa (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Kesho (Jumapili, Julai 22, 2018), Waziri Mkuu Lee Nak Yon atakuwa na mazungumzo rasmi ya kiserikali na mwenyeji wake pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali na pia kwa pamoja watashuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and service  passports).

Pia ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha.

Anatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.