Saturday, July 7, 2018

WAZIRI MKUU: SERIKALI HAITANUNUA MADENI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kununua madeni yaliyosababishwa na mikopo ya kibenki kwenye vyama vikuu vya ushirika nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.

“Serikali ya awamu ya tano hatuna biashara ya kununua madeni ya vyama vikuu, kulikuwa na tabia ya watu wa ushirika kukopa na hali ikiwa mbaya wanakimbilia Serikalini. Serikali hii hatuna biashara hiyo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema anazo taarifa kwamba Chama Kikuu cha mkoa wa Kagera (KCU) kimekopa fedha Benki ili kiweze kulipa deni la mwaka 2014. “Nimeambiwa KCU wamekopa fedha benki ili kulipa deni la mwaka 2014, hii inaingia akilini kweli? Mnakopa fedha kulipa deni la zamani, ni kwa nini msiwatafute waliosababisha deni na kuwachukulia hatua?,” alihoji.

“Ninyi mlikuwa watu sita ambao mlikubaliana kama viongozi, mlienda kukopa kuzidi uwezo mlionao. Leo hii ni kwa nini serikali ije kulipa wakati mmetumia ninyi?,” aliuliza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tatno inasisitiza masuala ya ushirika kwa sababu imeamua kuwahudumia wananchi kuanzia ngazi ya chini kuanzia pembejeo, dawa hadi masoko.

“Tunataka tuondoe utaratibu wa chama kikuu kukopa fedha benki ili kikanunue mazao. Vyama vingi vimetengeneza hasara, leo hii vyama vikuu vina madeni. Hii ni kwa sababu mlikopa fedha benki wakati hata hamjui mna kilo ngapi ambazo zimevunwa.

“Fedha mnachukua nyingi na hata ikibaki hamrudishi benki. Riba anadaiwa mkulima kupitia kilo anazouza, deni anapelekewa mkulima na kuanza kukatwa kwa kila kilo. Hatutaki tena utaratibu huu. Kuanzia sasa, AMCO ndiyo itaratibu na kukusanya mazao ya kila mwanachama kwa sababu yenyewe inajua ina wanachama wangapi, wana ekari ngapi na wanatarajia kuvuna kilo ngapi,” amesema.

Amesema ili kuondokana na utaratibu wa vyama vikuu kukopa benki, Serikali imepiga marufuku utaratibu huo na badala yake wanunuzi wataenda kununua mazao kwenye vyama vya msingi kupitia minada na watatakiwa kuwa wameingiza fedha kwenye vyama vya msingi (AMCOS) ndani ya siku tatu.

“Tulishasema mwisho uwe ni msimu huu, yasijirudie tena haya mambo ya kukopa benki.  Mnunuzi akipata mnada, ndani ya siku tatu, anatakiwa awe amehamisha fedha kwenda kwenye akaunti ya AMCOS husika,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema mfumo wa ushirika bado unakabiliwa na changamoto ya upotoshaji na maewagiza maafisa ushirika wakasimamie suala hilo kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakulima.

“Leo hii tunakabiliwa na changamoto kubwa kupitia uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi za Mazao Ghalani, Kuna watu wanapita wakipotosha kwamba serikali inawakopa wakulima mazao yao.”

“Nendeni mkawaelimishe wakulima kwamba mtu akipeleka mazao yake ghalani siyo kwamba anakuwa tayari ameuza, bali anayaweka pale na kujua ana kilo ngapi, amapewa risiti na kusubiri bei iwe nzuri wakati wanunuzi wakibishana. Hela ikilipwa, anapewa hela yote kulingana na mzigo wake,” alisema.

Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa Jumamosi ya kwanza ya Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ushirika kwa ulaji wa uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma.”


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.