Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba,
amesema zoezi la uokoaji wa watu walionasa kwenye jengo lililoporomoka Jumamosi
ya Novemba 16, 2024 Kariakoo kwenye Mtaa wa Congo na Mchikichi Jijini Dasr es
Salaam, litaendelea tena kwa saa 24 za ziada baada ya saa 72 za kawaida za
kiwango cha kimataifa kumalizika.
Bw. Makoba ameyasema hayo,
wakati akizungumza na waandishi wa habari Kariakoo kwenye eneo la tukio, ambapo
amesema kuongezeka kwa saa hizo 24 za ziada, ni agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alilolitoa kupitia kwa
Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, katika kikao cha tathmini kuhusu zoezi
hilo la uokoaji ambapo amelitaka jeshi la zimamoto na uokoaji, kuendelea na
shughuli hiyo ili kunusuru uhai wa watu ambao bado wamekwama kwenye jengo hilo.
“Tukiwa kwenye kikao cha
tathmini cha kazi inayoendelea, moja ya ajenda iliyozungumzwa ni kuhusiana na
utaratibu wa uokoaji, kulianza kutokea maneno kwenye mitandao ya kijamii kwamba
baada ya masaa 72 kwa kawaida kwa viwango vya kimataifa, zoezi la uokoaji
kwenye maeneo kama haya linabadilika, na wanaanza kutumia mashine pale
inapolazimu, sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan muda huu ametoa maelekezo
kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, na maelekezo hayo yaje kwa kikosi
chetu cha Zimamoto na Uokoaji kwamba zoezi hili liendelee kwa saa zingine 24 za
ziada, ni kwamba wasisitishe, kabla ya kubadili hatua yoyote, kwa hiyo zoezi
hili linaendelea, halitasitishwa kama ambavyo wananchi wengine wameanza kuwa na
hofu” amesema Bw. Makoba.
Amesema lengo ni kuhakikisha
maisha ya watu walioko kwenye jengo hilo yanalindwa na kwamba hakuna kifusi
kitakachowaangukia.
“Imempendeza Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwamba, tutaendelea kutumia mbinu ambazo zilikuwa
zikitumika za weledi na ustadi zaidi katika kuhakikisha kwamba, kwanza
tunaridhika kwamba hakuna ambaye aliyepo hai atasumbuliwa au ataangushiwa
kifusi huko chini, au kwa namna yoyote ile itamkuta ili kumsababishia kupoteza
maisha, baada ya masaa 24 tutatangaza utaratibu unaofuata” amesema Bw. Makoba.
Zoezi la uokoaji wa watu
walionaswa kwenye jengo lililoporomoka linaendelea kwa kasi kubwa kwa siku ya
nne sasa ambapo Serikali inafanya jitihada zote kuhakikisha hakuna madhara
yatakayowapata watu walionasa kwenye jengo hilo.