Wednesday, February 11, 2026

SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKISHWAJI JAMII YA WATU WASIOONA KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII, KIUCHUMI NA KIUTAMADUNI ILI KUONGEZA TIJA.


Serikali inatambua Breli si mfumo pekee wa kusoma, bali ni nyenzo ya kufungua milango ya elimu, ujuzi, ukarimu wa jamii, na ushiriki kamili wa kijamii.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu (SBUU) Mhe. Ummy Nderiananga kwa niaba ya Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Mhe. William Lukuvi leo Jijini Dodoma huku akieleza kuwa Mfumo huo umebadilisha maisha ya mamilioni ya wasioona na wenye uoni hafifu duniani kote ikiwemo Tanzania.

“Kwa kutambua mchango wa Jamii ya Wasioona katika maendeleo ya taifa letu, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wasioona kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati na Mipango inayojumuisha huduma na teknolojia ya breli pamoja na kuimarisha elimu jumuishi kwa kuanzisha na kuendeleza shule na vituo maalum kwa wanafunzi wasioona, pamoja na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya Breli, vitabu maalum na teknolojia saidizi” amefafanua Mhe. Waziri.

Aidha, Serikali imetenga madirisha maalum ya huduma kwa watu wenye ulemavu katika vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za uchunguzi, tiba na utengamao kwa watu wenye ulemavu wakiwemo wasioona.

Vilevile, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kubuni na kutekeleza miradi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, mafunzo ya ujuzi na ajira kwa watu wasioona.

“Tunapoadhimisha kilele cha Siku ya Kimataifa ya Breli Duniani nitoe wito kwa kila mwananchi, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kiraia pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha mazingira jumuishi, kuondoa vikwazo vya kijamii na kimazingira, na kuweka mifumo wezeshi itakayohakikisha Ustawi na Maendeleo ya jamii ya wasioona yanatimizwa kikamilifu. Kwa kufanya hivyo, Taifa letu litaendelea kujenga jamii yenye usawa, haki na mshikamano, inayothamini mchango wa kila mmoja bila ubaguzi” ameomgeza Mhe. Nderiananga

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli huadhimishwa tarehe 12 Februari ya kila mwaka kwa lengo la kutoa nafasi kwa mataifa yote kutafakari kuhusu mchango na nafasi ya teknolojia ya Breli katika kuwawezesha watu wasioona kushiriki kikamilifu katika elimu, ujuzi na maendeleo ya taifa. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Teknolojia ya Breli Husaidia Kuchochea Maendeleo kwa Wasioona na Ujenzi wa Taifa” na kwa Tanzania maadhimisho hayo yatafanyika katika Halmashauri zote na kwa ngazi ya Kitaifa yatafanyika mkoani Tanga. 

 

Breli ni mfumo ulioasisiwa na ndugu Louis Braille, ambaye alibuni njia ya maandishi inayowawezesha watu wasioona kusoma, kuandika na kupata elimu na habari kwa usawa na wale wanaoona. Mfumo huu unawapa watumiaji wa Breli fursa sawa za kushiriki katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kifikra. Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Breli.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.