KATIBU
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim
Yonazi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa DART amesema
Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inamaliza changamoto ya usafiri
katika Jiji la Dar es Salaam, ili wananchi waweze kupata huduma bora, ya haraka
na yenye uhakika.
Akizungumza
hii mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya
usafirishaji jijini humo, Dkt. Yonazi amesema Serikali imewekeza kwa kiwango
kikubwa katika kuboresha sekta ya usafiri wa umma.
Alisema
katika ziara hiyo, kamati ilitembelea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es
Salaam (DART) pamoja na Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART)
na kujionea maendeleo ya uwekezaji uliofanywa.
“Ni
dhamira ya Serikali kuhakikisha usafiri wa Dar es Salaam unakuwa bora, wa
kisasa na unaokidhi mahitaji ya wananchi. Tumejionea miundombinu iliyowekwa na
jitihada zinazoendelea kuboresha huduma,” alisema.
Dkt.
Yonazi alibainisha kuwa tayari kampuni zimeanza kuleta mabasi mapya, hatua
itakayoliwezesha jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji yenye usafiri wa kisasa
barani Afrika. Aliongeza kuwa mabasi mengi yatatumia gesi asilia, huku Serikali
ikiwa imejenga miundombinu ya vituo vya gesi ili kuhakikisha huduma hiyo
inapatikana kwa urahisi.
Aidha,
alisema Serikali imewekeza katika mifumo ya TEHAMA itakayomwezesha mwananchi
kutumia kadi maalumu kulipia nauli bila kulazimika kupanga foleni, jambo
litakaloongeza ufanisi na kupunguza usumbufu.
Katika
hatua nyingine, aliwahakikishia wananchi kuwa mabasi yote yaliyoharibika
yatafanyiwa ukarabati na kurejea barabarani ili kuimarisha upatikanaji wa
huduma.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Bw. Said Tunda
alisema lengo kuu ni kurejesha furaha kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa
kuwapatia usafiri wa uhakika.
Pia aliwataka waendesha daladala kuendelea kutoa huduma huku Serikali ikiendelea kufanya mazungumzo nao ili kupata utaratibu bora wa ushirikiano, hususan kwa zile zilizopewa kibali cha kutumia barabara ya mwendokasi.
Hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miundombinu imara na huduma bora za kijamii.

.jpeg)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.