Serikali
kupitia Ofisi ya Halmashauri ya Mtwara
Mikindani imekabidhi vifaa saidizi na kiasi cha shilingi milioni 342 ikiwa ni
jitihada ya kujikita katika utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya
wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu.
Akizungumza
katika hafla hiyo iliyofanyika Mkoani Mtwara, Mkindani leo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Nderiananga, amesema hatua hiyo ni
utekelezaji wa sera na mwelekeo wa maendeleo unaolenga kujenga uchumi jumuishi
unaowawezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji
na maendeleo ya Taifa.
Naibu
Waziri Ummy amefafanua, “Mikopo hii inalenga kuchochea na kuinua uchumi wa
chini kwenda juu sambamba na mwelekeo wa dira ya Taifa ya kujenga uchumi
shindani, jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.”
Ameongeza
kuwa, utoaji wa vifaa saidizi ikiwemo viti mwendo, magongo, fimbo nyeupe za
wasioona pamoja na taulo za kike, ni utekelezaji wa sera ya kutomwacha mtu
nyuma katika safari ya maendeleo, sambamba na maono ya kitaifa ya kujenga jamii
yenye heshima, utu na usawa wa fursa.
Kwa
upande wake Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Maendeleo ya Vijana Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka, ameweka wazi kuwa Serikali
katika jitahada za kuwakwamua wananchi kiuchumi itaendelea na utekelezaji wa
kuleta miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Mtwara ikiwemo kuboresha
Bandari ya Mtwara, ujenzi wa reli, na uboreshaji wa uwanja wa ndege pamoja na
marekebisho ya miundombinu ya Barabara.
Waziri Nanauka amehimiza, “Wanufaika wa mikopo hiyo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, na kurejesha kwa wakati ili kushirikiana katika kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.”


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.