Wakala
wa Serikali wa Uchapishaji Tanzania (TGPA) leo umepokea ugeni wa watu 24 kutoka
Shirika la Uchapishaji la Uganda (Uganda Printing and Publishing Corporation –
UPPC) waliowasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kubadilishana
uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchapishaji wa serikali.
Ujumbe
huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UPPC, Profesa Joackim
Buwembo, ukijumuisha wajumbe wa bodi, Mpigachapa Mkuu wa Serikali ya Uganda,
Profesa Sudi Nangoli, pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali za shirika
hilo.
Kwa
mujibu wa taarifa za TGPA, ziara hiyo imelenga kujifunza na kubadilishana
uzoefu katika uchapishaji wa nyaraka za serikali, hususan Gazeti la Serikali,
pamoja na uchapishaji wa nyaraka zenye alama za usalama (security printing).
Katika
ziara hiyo, pande zote mbili zimefanya vikao vya kitaalamu na majadiliano
yaliyolenga kuimarisha mifumo ya uchapishaji, kuongeza ubora wa huduma na
kuzingatia viwango vya usalama katika uchapishaji wa nyaraka nyeti za serikali.
Aidha,
TGPA na UPPC zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uchapishaji, kuandaa
mafunzo kwa watumishi wao, pamoja na kuanzisha utaratibu wa kubadilishana
uzoefu kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuimarisha mahusiano ya kitaasisi kati
ya Tanzania na Uganda.
Ziara hiyo ni
sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuendeleza ushirikiano wa kikanda katika sekta
ya uchapishaji wa serikali na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa kuzingatia
viwango vya kimataifa.


EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.