Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William
Lukuvi, amemfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, salamu za pole kufuatia ajali ya kufukiwa kwa mafundi katika
Mgodi wa Dhahabu wa Nyandolwa, iliyotokea tarehe 11 Agosti 2025 katika Mkoa wa
Shinyanga.
Waziri
Lukuvi ameeleza kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali
hiyo, na kwa niaba ya Rais Samia, ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa
wao katika tukio hilo la kusikitisha. Aidha, ameeleza kuwa Serikali itagharamia
kikamilifu gharama za mazishi kwa waathirika wa ajali hiyo pamoja na matibabu
kwa waliofikwa na tukio hilo.
Akizungumza
na wanandugu wa marehemu na wale waliokwama mgodini, Mhe. Lukuvi amewatia moyo
na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu.
Ametoa wito kwa timu za uokoaji kuongeza juhudi na kasi ya uokoaji ili kuwaokoa
mafundi waliokwama kwa haraka na usalama zaidi.
“Tunaamini
kuwa kazi kubwa imefanyika lakini bado tunahitaji jitihada zaidi. Serikali
inatambua uzito wa tukio hili na itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa
kuhakikisha kila jitihada zinafanyika kwa ufanisi,” amesema Lukuvi.
Kwa upande
wake, Msimamizi wa Mgodi huo, Fikiri, ameiambia Serikali kuwa ndani ya kipindi
cha siku tatu hadi nne zijazo, zoezi la kuwaokoa wahanga waliokwama litakuwa
limekamilika. Ameeleza kuwa vifaa vya kutosha vimeletwa eneo la tukio na
wataalamu wanaendelea na kazi kwa umakini mkubwa kuhakikisha mafanikio ya
haraka.
Kabla ya
kuwasili katika eneo la mgodi, Mhe. Lukuvi alifanya ziara katika Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambapo alipokea taarifa ya kina kuhusu
maendeleo ya sekta ya madini katika mkoa huo pamoja na hali ya sasa ya shughuli
za uokoaji zinazoendelea katika mgodi wa Nyandolwa.
Akizungumza
kwa niaba ya ndugu wa wanasubiri waliofukiwa na kifusi Bw.Furaha Enock
aliishukuru Serikali kwa namna ilivyoratibu zoezi na inavyowahudumia katika
kipindi chote toka tukio kutokea na kueleza kuwa imefanya jambo la kipekee, la
heshima na la uungwana kuwashika mkono na kuhudumia kwa hali na mali na
kuwasihi wanandugu kuendelea kuwa na utulivu.
"Kipekee
ninaipongeza Serikali Yetu imetufanyia wema na imetupa faraja kwa namna
wanavyoratibu tukio zima, tunakosa neno zaidi ya Asante sana kwa Rais Dkt.
Samia pamoja na uongozo wake wote," alisema Enock
AWALI
Ziara ya
Waziri Lukuvi ni sehemu ya juhudi za Serikali za Uratibu na kutoa maelekezo kwa
karibu katika kipindi hiki cha majonzi, huku ikilenga kuimarisha utendaji wa
shughuli za uokoaji na kuhakikisha haki na heshima kwa waathirika wote wa ajali
hiyo.