WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule mbalimbali nchini kusoma kwa bidii na wasikubali kushawishika.
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka sheria kali kwa wote watakaobainika kukatisha masomo ya watoto wa kike kwa kuwapa ujauzito au kuwaozesha.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Oktoba 04, 2017) wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana na WAMA Sharaf.
Shule ambayo ipo wilayani Lindi inamilikiwa na Taasisi ya WAMA ambapo inasomesha watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira magumu.
Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wa kike kuhakikisha wanatumia muda wao vizuri kwa kusoma kwa bidii na hatimaye watimize malengo yao.
Amesema ni vema wanafunzi hao wakatumia vizuri fursa hiyo ya elimu wanayoipata shuleni hapo kwa kusoma kwa bidii na wafuate ratiba itakayokuwa inapangwa.
“Nawasihi mtumie muda huu kusoma kwa bidii ili muweke msingi imara ya kujenga maisha yenu ya baadae. Msikubali kushawishika na kukatisha masomo yenu.”
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mbunge wa Kuteuliwa alisema shule hiyo inasomesha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kutoka mikoa yote nchini.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.