Wednesday, March 28, 2018

MHE.IKUPA: SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA WATU WENYE ULEMAVU

Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kujikwamua katika nyanja zote na kuchangia katika maendeleo nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe.Stella Ikupa wakati wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/2019 kwa mafungu ya Taasisi zinazosimamiwa na Ofisi hiyo Mjini Dodoma.
Waziri Ikupa alieleza kuwa tayari Serikali imeanza mikakati ya kuboresha mazingira ya watu wenye Ulemavu kwa kuvifufua vyuo na vituo vyao ili kuwapa nafasi nzuri ya kujifunza katika mazingira yanayowapa uhuru na tija kulingana na aina za ulemavu walionao.
“Tayari tumeanza kuboresha mazingira ya vyuo vya ufundi ikiwemo kile cha Yombo kilichopo Mjini Dar es Salaam na Sabasaba ili kusaidia kuwapa fursa za kujifunza katika mazingira rafiki hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna kuwa na vifaa vya kutosha”.Aliongezea
Sambamba na hilo Serikali inaendelea na hatua za kuboresha mazingira ya Watu wenye ulemavu kwa kuwajengea uwezo, kuongeza wataalam wa kuwafundisha, kuwapa mafunzo maalumu yenye kuleta tija pamoja na kuwashirikisha katika fursa za maendeleo.
Aliongezea kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na vyuo mbalimbali ili kupata taarifa sahihi za mahitaji halisi ya watu wenye ulemavu yatakayosaidia kuwa na kanzidata ya kudumu yenye taarifa hizo.
“Jitihada zilizopo ni pamoja na kushirikisha Wizara ya Elimu ili kuweza kupata taarifa muhimu za watu wenye ulemavu zitazosaidia kuwa na kanzi data ya uhakika inayowatambulisha kwa idadi, aina ya ulemavu na ujuzi alionao ili kuwapa nafasi wenye sifa za kushiriki katika programu za kukuza ajira”.Alisisitiza Mhe.Ikupa
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Mhe.Amina Mollel alishauri kuwe na mikakati madhubuti yenye tija kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kutoa semina kwa watumishi wa serikali juu ya namna bora ya kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa kuzingatia mahitaji yao.
“Ifike mahali kuwe na mikakati madhubuti ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hususani kwa kuwajengea uwezo watumishi kujua namna nzuri ya kuwahudumia watu wenye ulemavu pamoja na kusaidia kuzikabili changamoto wanazokabiliana nazo”.Alisema Mhe.Mollel.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.