Monday, August 6, 2018

WAZIRI MKUU AFUNGUA MICHEZO YA MAJESHI YA POLISI

*Awasisitiza wayatumie kwa kubadilishana taarifa za kiintelejensia

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka askari wanaoshiriki katika michezo ya Shirikisho la Majeshi ya Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki watumie mashindano hayo kama fursa ya kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kujadili namna ya kufanya operesheni za pamoja na kwa wakati mmoja.

Pia namna ya kushirikiana katika masuala ya kisheria ambayo mara nyingi yamekuwa vikwazo katika utendaji wao hasa katika shughuli za upelelezi ili kuendelea kuwatia hatiani wahalifu wanaovuka mipaka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 6, 2018) wakati akifungua michezo ya Shirikisho la Majeshi ya Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.

“Wote tunaelewa kuwa makosa yanayovuka mipaka kama vile vitendo vya ugaidi, ujangili, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha ndogo ndogo, bidhaa bandia, utakatishaji wa fedha haramu, biashara ya dawa za kulevya na mienendo ya wahalifu wanaovuka mipaka huathiri amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kanda yetu,” amesema.

Amesema uhalifu huo hauwezi kuzuiwa pasipo jitihada za makusudi na mikakati ya pamoja ya kupambana nayo, hivyo anatarajia kuwa michezo hiyo itatoa fursa ya kipekee kwa nchi wanachama kubuni mikakati mbalimbali ya kupambana na kuzuia uhalifu hasa ule unaovuka mipaka ya nchi zao.

Waziri Mkuu amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza lengo la Shirikisho la Wakuu wa Polisi la Ukanda wa Afrika Mashariki. “Hivyo tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuendeleza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambayo yameanza kuonekana katika Nchi zetu,”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka askari hao waendeleze ushirikiano huo kwa usalama wa ukanda wa Afrika Mashariki kwa sababu michezo ni moja ya nyenzo za kuleta na kuimarisha usalama na amani kwenye jamii. 

Amesema kaulimbi ya mwaka huu ambayo ni ‘Michezo katika Kukuza Ushirikiano wa Kikanda wa Polisi, Amani na Usalama”. (“Sports for Promoting Police Regional Cooperation, Integration, Peace and Security”). inajieleza yenyewe kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kuleta amani na usalama.

Ufunguzi wa mashindano hayo yanayoshirikisha nchi saba kati 14 za Ukanda wa Afrika Mashiriki ambazo ni mwenyeji Tanzania, Uganda, Kenya, Sudani, Sudani Kusini, Burundi na Rwanda yameanza leo na yanatarajia kukamilika Agosti 12, 2018.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.