Thursday, September 13, 2018

PROF. KAMUZORA - TUWAJENGEE VIJANA WETU UWEZO KIFIKRA.


Na Paschal Dotto- MAELEZO

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora ameitaka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kuwajengea na kuwaimarisha vijana katika fikra pevu ya maendeleo na hivyo kuweza kujitegemea kiuchumi kwa kufanya ujasiriamali katika maeneo yao.

Akizungumza katika mjadala na TPSF,ulioafanyika Jijini Dar es Salaam Kamuzora alisema kuwa vijana ni chachu ya maendeleo ya kesho kwa hiyo elimu kuhusu mabadiliko ya fikra inahitajika ili waweze kujitambua na kujiongoza vema kimaisha katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

“Mimi naamini kwamba tukiwapa uwezo wa kifikira na kuwaongezea maarifa vijana wetu wanaweza kuimarika zaidi kiuchumi kwa hiyo hivi mnavyofanya ni mfano bora  wa kuigwa maana mnaimarisha taifa la kesho”, alisema Prof. Kamuzora.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa hivi karibuni wataalam wanaojihusisha na “ubongo wa binadamu” katika kubadilisha fikra ni wengi kwa hiyo ni muhimu kwa TPSF kutafuta wataalam wa kutoa elimu ya fikra kwa vijana ili kujihusisha na ujasiriamali katika maeneo yao.         

“Tafuteni wataalam wa “ubongo wa binadamu” ili kuwabadilisha vijana wetu fikra, tuna vijana wengi sana, tukiweza kuwajengea mazingira mazuri katika fikra zao Tanzania ya baadaye itakuwa nzuri sana”, alisisitiza Prof. Kamuzora.

Aidha Prof. Kamuzora aliongeza kuwa TPSF isijikite zaidi katika kuwawezesha wajarisiamali wakubwa na kipekee walioko mjini, bali iende  hadi vijijini kwa wakulima wadogowadogo  ambako ujasiriamali unaanzia.

Prof.Kamuzora ameipongeza TPSF kuja na mbinu za kuwasidia vijana yenye kauli mbiu isemayo ‘Kijana Jiajiri’ ambayo inalengo la kuwapa vijana uwanja wa kujikwamua kiuchumi na kuweza kusisimama wenyewe kwenye biashara.

Mwisho.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.