*Awa Mtanzania wa kwanza kucheza ligi kuu ya Uingereza
*Wachezaji wengine wajifunze kupitia mafanikio yake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempongeza nahodha wa timu ya Taifa, Mbwana Samatta kwa kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Uingereza katika Klabu ya Aston Villa.
“Tunamtakia kila la kheri katika Ligi Kuu ya Uingereza ambayo ni moja ya ligi ngumu, maarufu na yenye ushindani mkubwa duniani. Nitoe rai kwa wachezaji wetu wa ndani, nao wajifunze kupitia mafanikio ya Samatta kwa kuongeza bidii, nidhamu na kiu ya maendeleo.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) wakati akiahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 bungeni jijini Dodoma.Amesema sanaa na michezo imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa na hata katika kutengeneza ajira.
“Kwa mfano, kwa mwaka 2018/2019 sekta hiyo ilichangia asilimia 0.29katika ukuaji wa pato la Taifa. Niwapongeze wasanii wetu kwa kuendelea kulitangaza vema Taifa letu na fursa zake na hivyo, kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia utalii na uwekezaji.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzipongeza timu za wanawake za umri wa miaka chini ya 20 (U-20) na 17 (U-17) kwa kuendelea kufanya vema kuelekea kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2022.
“Wakati timu ya Wanawake U-20 ikipata ushindi wa nyumbani na ugenini dhidi ya Uganda,timu ya wanawake U-17 nayo iliiondosha Burundi kwenye mashindano kwa jumla ya magoli 6-1,” amesema.
Pia, Waziri Mkuu ameipongea timu ya KilimanjaroQueenskwa kuchukua ushindi wa pili wa mashindano ya CECAFA.
“Kwa mafanikio hayo ya soka nchini kwa Wanawake na Wanaume, nalipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa usimamizi mzuri bila kumsahau mlezi wa timu za Wanawake, Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji wa timu ya Taifa chini ya miaka 20 (wavulana) ambao walifanikiwa kuwa mabingwa wa michuano ya mpira wa miguu kwa CECAFA yaliyofanyika nchini Uganda.
Kadhalika, Waziri Mkuu amempongeza Kelvin John, mshambuliaji hatari chipukizi kwa kusajiliwa na timu ya GENK ya Ubelgiji kwenye kikosi chao cha U-20, ambapo kwa sasa anasomeshwa nchini Uingereza ikiwa ni maandalizi ya kuchezea kikosi cha kwanza.
Kwa upande wa ndondi, Waziri Mkuu amesema nako tumeendelea kufanya vizuri. “Nitumie nafasi hii kumpongeza bondia wetu Salim Mtango ambaye Januari 31, 2020 alimtwanga bondia Surriya Tatakhun kutoka Thailand kwa Technical Knock Out(TKO). Tanga inaendelea kutoa mabondia wazuri, endeleeni kutufikisha hapo.”
Pia, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Bunge ambayo ilishiriki Michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki Kampala, Uganda kuanzia Desemba 8 -18, 2019 na kupata medali tano za dhahabu.
Amesema katika michezo hiyo, timu ya Bunge ilifanikiwa kupata jumla ya medali 18 ambazo kati yake, medali za dhahabu zilikuwa tano, fedha 10 na shaba tatu. “Nitumie fursa hii kuipongeza Timu ya Bunge kwa mafanikio hayo pamoja na kulitangaza vema Bunge letu huko nje.”
Wazri Mkuu amewataja wabunge walioshinda medali za dhahabu ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Yosepher Komba na Mheshimiwa Rose Tweve.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua juhudi za Bw. Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo na fujo isiyoumiza katika kutangaza nchi, vivutio vya utalii pamoja na lugha ya Kiswahili.
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza wanamichezo pamoja na wasanii ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi sambamba na kujipatia kipato.
“Nyote mtakubaliana nami kuwa kwa sasa michezo na sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato hususan kwa vijana. Aidha, nisisitize kuwa michezo ni kinga na tiba kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na unene uliopitiliza.”
Kutokana na faida hizo, Waziri Mkuu ameendelea kutoa rai kwa wananchi washiriki kikamilifu katika michezo na kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mfumo bora wa kisera na kisheria ili kuhakikisha sekta ya michezo inakua na kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.