WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ni vema viongozi
wa vyama vya siasa nchini wakaonesha mfano wa kuendesha siasa za
kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha watanzania na siyo
kuwatenganisha.
“Hivyo
basi, tudumishe utulivu, amani, mshikamano pamoja na ustaarabu wetu wa
Kitanzania katika kipindi chote cha kampeni na Uchaguzi Mkuu ili
kulifanya Taifa letu kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa
barani Afrika na duniani kwa ujumla.”
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni
hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma.
Pia, Waziri Mkuu amewasihi
Watanzania washiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kufuata
sheria, kanuni na taratibu za Nchi. “Hakuna kiongozi aliyewahi kupata
sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha mifarakano.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura kwa awamu ya pili linatarajiwa kuanza Aprili 5, 2020 na kukamilika
Juni 26 2020.
“Zoezi
hili litaenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wapiga kura katika
daftari hilo. Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili waweze kutumia haki
yao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.”
Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020 nchini.
Amesema
pamoja na mambo mengine, maandalizi hayo yanahusisha Zoezi la Kuboresha
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika nchi nzima. Awamu ya
kwanzailizinduliwa tarehe 18 Julai, 2019 Mkoani Kilimanjaro na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Uboreshaji
wa daftari hili ulihusisha uandikishaji wa wapiga kura wapya ambao
wametimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo ifikapo siku ya
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; urekebishaji wa taarifa za wapiga kura
walioandikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ufutaji wa taarifa
za Wapiga Kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura.”
Amesema katika zoezi hilo, jumla ya wapiga
kura 10,285,732 wameandikishwa na kati yao, wapiga kura wapya ni
7,043,247, walioboreshewa taarifa zao ni 3,225,778 na wapiga kura
waliofutwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutokana na kupoteza
sifa ni 16,707.
Wakati huo huo, Wazirti Mkuuamesema
Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba liidhinishe
jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo.
Vilevile
Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000
kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.