Wednesday, April 1, 2020

VIJIJI 9,001 NCHINI VIMEUNGANISHIWA UMEME -MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kutekeleza Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) ambapo vijiji vilivyounganishiwa umeme nchini vimeongezeka kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015 hadi vijiji 9,001 mwezi Machi 2020. 

Amesema kuwa jumla yataasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, dini, mashine za kusukuma maji na huduma za biashara zimenufaika na mradi, hivyo mafanikio hayo pamoja na mengine makubwa yaliyopatikandani ya kipindi cha takriban miaka mitano yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi wa Taifa na kijamii kwa ujumla.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika,tarehe 20 Novemba 2015 wakati akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia na kuwajali.

Waziri Mkuu amesema katika kutekeleza azma hiyo, ujenzi wa miundombinu muhimu ya kiuchumi hususan ya usafiri na usafirishaji sambamba na uimarishaji wa huduma muhimu za kijamii ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano.

Amesema ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania na urejeshwaji wa mali za ushirika mfano, NCU, SHIRECU ni kati ya hatua za msingi zinazochukuliwa na Serikali katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Waziri Mkuu amesema hatua nyingine ni pamoja na urejeshwaji wa mali za Mamlaka ya Mkonge Tanzania, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, ulinzi wa maliasili na rasilimali za Taifa pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Elimu, Afya na Maji.

“Katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia miradi hiyo muhimu ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa ambao hadi Machi 2020 umetumia sh. trilioni 2.96 na kukamilika kwa asilimia 75 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na asilimia 28 kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora.”

Amesema utekelezaji wa mradi huo umewezesha utoaji wa zabuni zenye thamani ya sh. bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640, ajira zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam zimezalishwa na kati ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5 ikilinganishwa na asilimia 53.5 ya wageni.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia gharama kubwa katika kujenga miundombinu hiyo wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kulifanya Taifa kuwa na uchumi imara wa kujitegemea na wenye kuhimili ushindani. Fedha hizo pia zimekuwa chanzo cha ajira na zabuni kwa Watanzania zinazowasaidia kuongeza kipato.

“Mradi huu utakapokamilika utaongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi pia utachochea ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda, utalii na biashara. Vilevile, mradi huu utakuwa chanzo cha ongezeko la mapato ya Serikali yatakayosaidia katika kuboresha maslahi ya watumishi na huduma za kijamii kama vile afya, elimu na maji.”

Vilevile, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere linalotarajiwa kuzalisha Megawati 2,115, hadi Machi 2020 mradi huo umegharimu sh. trilioni 1.28 na umekamilika kwa asilimia 10.74. 

Amesema kukamilika kwa bwawa hilo kutalihakikishia Taifa letu umeme wa uhakika na wa nafuu zaidi. Aidha, ongezeko hilo la uzalishaji wa umeme litawezesha shughuli za uzalishaji viwandani kuwa za uhakika, tija, ufanisi na gharama nafuu zaidi. “Vilevile, mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme badala ya kuni.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi mahiri na thabiti wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa.

Wakati huo huo, Wazirti Mkuuamesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba liidhinishe jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

(MWISHO)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.