Monday, February 13, 2017

MAMA MAGUFULI NA MAMA MAJALIWA ZIARANI SINGIDA

MKE wa Rais Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametoa rai kwa Wanzania kujenga tabia ya kusaidia watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu.

Wake hao wa viongozi pia wamewatahadharisha watumishi wanaofanya kazi katika vituo vya kulelea wazee wasiojiweza wahakikishe misaada inayotolewa na wadau mbalimbali inawafikia walengwa bila ya kuchakachuliwa.

Wameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 13, 2017) wakati walipotembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza na walemavu watokanao na ugonjwa wa ukoma ya Sukamahela wilayani Manyoni Mkoani Singida.

Katika kituo hicho wamekabidhi tani 7.5 za vyakula mbalimbali ukiwemo mchele, unga wa sembe na maharage, ambapo Mama Janeth amewataka viongozi wa kituo kuhakikisha chakula hicho hakichakachuliwi.

Akizungumza na wazee wa makaazi hayo, viongozi mbalimbali na wananchi wanaozunguka eneo hilo Mama Janeth amesema “Naomba chakula hiki kitunzwe vizuri na hakikisheni kinawafikia walengwa na kisichakachuliwe hii ni sadaka,”.

Kwa upande wake Mama Mary amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na kuwasaidia wazee wanaoishi katika makaazi ya kulelea walemavu na wasiojiweza nchini kwa sababu wanakabiliwa na changamoto nyingi.

“Watanzania wote popote mlipo tukumbuke kutembelea vituo vya kulelea wazee kikiwepo na hiki tulichokitembelea leo cha Sukamahela na kutoa misaada mbalimbali kkwa kadri tutakavyojaaliwa,” amesema.

Awali Mkuu wa Makazi hayo Bw. Yeremia Ngoo alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1974 chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii kwa lengo la kuwasaidia watu wenye ukoma na wazee wasiojiweza mkoani Singida.

Bw. Ngoo alisema kituo hicho chenye wakazi 62 kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa wapishi ambapo kwa sasa yupo mmoja huku mahitaji yakiwa ni wapishi wanne. Pia nyumba nyingi ni chakavu na zina nyufa.

Naye Mwenyekiti wa Wazee waishio katika makaazi hayo, Mzee Andrea Yohana aliwashikuru wake hao wa viongozi na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kusaidia watu wasiojiweza.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.