WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Arusha Chini, wilayani
Moshi, mkoani Kilimanjaro na kukagua baadhi ya miundombinu ya kiwanda pamoja na
mashamba.
Akiwa kiwandani
hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba hivi sasa msimu wa uzalishaji umefungwa na
kiwanda kinafanyiwa matengenezo ambapo alishuhudia baadhi ya mitambo ikiwa
imefunguliwa na kufanyiwa ukarabati.
Akitoa taarifa
juu ya matengenezo hayo mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kiwanda hicho, Bw. Pascal
Petiot alimweleza Waziri Mkuu kwamba kiwanda hicho kimefungwa kwa zaidi ya wiki
sita ili kujiandaa na msimu ujao wa uzalishaji ambao uko karibuni kuanza.
“Hivi sasa ni
kipindi cha mvua, tumefunga msimu wa uzalishaji na tunaendelea na ukarabati wa mitambo
ili kujiandaa na msimu ujao. Kila mwaka ni lazima tufunge msimu kwa kipindi
kifupi, ili kufanya ukarabati kama huu,” alisema.
Akiwa kiwandani
hapo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuta mafundi wakifanya matengenezo katika
sehemu mbalimbali za kiwanda. Hata hivyo, alionyeshwa mtambo wa kuzalisha umeme
wa kiwanda hicho (boiler) ambao unatumia mabaki ya miwa yaliyokwisha kamuliwa
juisi (bagasse) ambayo huchomwa na kuchemsha maji ili kupata mvuke unaosukuma
jenereta.
“Tunatumia
mabaki ya miwa badala ya kuni, joto linalozalishwa linafikia nyuzijoto 450 na
kuweza kuzalisha megawati 17.5 wakati kiwanda kikiwa kinafanya kazi. Matumizi
yetu kwa ajili ya kiwanda, makazi ya watumishi na vijiji vya jirani yanafikia
megawati 12, na tunawauzia TANESCO megawati 4 ambazo wanaziingiza kwenye gridi
ya Taifa,” alisema Bw. Jaffari Ali Omari ambaye ni Afisa Utawala Mtendaji.
Bw. Omari
alimweleza Waziri Mkuu kwamba umeme unaozalishwa na kiwanda hicho ni mwingi
kuliko unaozalishwa na mabwawa ya Hale na Nyumba ya Mungu yakijumuishwa kwa pamoja.
“Hale inazalisha megawati nane na Nyumba ya Mungu inazalisha megawati tatu,”
alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho,
Bw. Robert Baissac alisema uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho umepanda
kwa asilimia zaidi ya 200 tangu wachukue kiwanda hicho mwaka 2000.
Alisema wakati
wanaanza, kiwanda kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa mwaka na wakati
wanakinunua walitakiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100 kwa kufikisha tani
72,000 za sukari. “Tuliweza kuvuka lengo hilo tangu mwaka 2007 na hivi sasa tumeweza
kuzalisha tani 111,800 katika msimu uliopita,” alisema.
“Tunatumia
mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na majaribio hapa hapa kiwandani. Tunatumia
mbolea na njia za umwagiliaji ili kuhakikisha hadhi ya miwa yetu ni ya
kuridhisha, na inayoweza kutupatia kiwango kikubwa cha sukari,” alisema.
Akitoa maoni ya jumla, Waziri Mkuu
aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho wafanye kazi kwa bidii na kujituma na
kuhakikisha wanaongeza tija katika uzalishaji wao.
“Msisitizo wa
Serikali ni kuwasihi Watanzania tubadilike, tuchape kazi ili tuweze kuongeza
tija mahali pa kazi,” alisema Waziri Mkuu.
Alikuwa akijibu
hoja ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi kiwandani hapo (TASIWU), Bw. Bilal
Omar Mchomvu ambaye aliomba Serikali iangalie uwezekano wa kuondoa makato ya
kodi kwenye bonasi na overtime wanazolipwa
na kiwanda hicho.
Kuhusu haki za
wafanyakazi kiwandani hapo, Bw. Mchomvu alimweleza Waziri Mkuu kwamba chama cha
wafanyakazi kina mahusiano mazuri na menejimenti ya kiwanda na kwamba kila
miezi mitatu wanakutana na wafanyakazi hao kama sheria inavyotaka.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.